Mwongozo wa Kimataifa wa Mwenendo na Maadili/Kamati ya Uratibu/Mkataba

This page is a translated version of the page Universal Code of Conduct/Coordinating Committee/Charter and the translation is 100% complete.
Outdated translations are marked like this.
Universal Code of Conduct

Kamati ya Kuratibu ya Mwongozo wa Kimataifa wa Mwenendo na Maadili(U4C), inayoakisi jumuiya nzima ya kimataifa, ni muundo wa utekelezaji wa kujitolea kufanya utekelezaji wenye usawa na thabiti wa UCoC.

Ni chombo chenye usawa na vyombo vingine vya juu vya ufanyaji maamuzi kama vile Kamati za Usuluhishi za NDA na Wasimamizi. U4C huamua kama kumekuwa na hitilafu ya kimfumo ya kikundi cha Wikimedia au jumuiya katika kutekeleza UCoC. Kamati hutoa uhakikisho wa ubora wa nyenzo za mafunzo zinazohusiana na UCoC, na inasimamia ukaguzi wa jumuiya wa kila mwaka wa UCoC na Miongozo ya Utekelezaji (EG).

Mkataba huu unaelezea upeo na madhumuni ya U4C, uteuzi wake, majukumu ya uanachama, taratibu za kimsingi, pamoja na sera na mfano.

1. Kusudi na Upeo

1.1. Kazi

Upeo wa U4C ni pamoja na:

  • Ripoti za ufuatiliaji wa ukiukaji wa UCoC. U4C inaweza kufanya uchunguzi zaidi na kuchukua hatua pale inapofaa.
  • Kuzingatia hali ya utekelezaji wa UCoC kwenye majukwaa ya Wikimedia mtandaoni na nje ya mtandao, kama ilivyoidhinishwa na Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Wikimedia mnamo mwaka 2020.
  • Kupendekeza mabadiliko yanayofaa kwa UCoC na Mwongozo wa Utekelezaji wa UCoC kwaajili ya Shirika la Wikimedia Foundation na jumuiya kuzingatia kama sehemu ya mapitio ya kila mwaka ya UCoC.
    • U4C haiwezi kubadilisha hati yoyote yenyewe kama yenyewe.
  • Kusaidia Shirika la Wikimedia Foundation na wadau wengine katika kushughulikia kesi zilizo chini ya mamlaka yao, pale kunapokuwa na maombi ya kufanya hivyo.

1.2. Majukumu

U4C ina majukumu yafuatayo:

  • Hushughulikia malalamiko na rufaa katika hali zilizoainishwa katika Miongozo ya Utekelezaji, ikijumuisha vitu vifuatavyo lakini sio hivyo tu:
    • Ukosefu wa uwezo wa kujitawala wa ndani wa kutekeleza UCoC;
    • Maamuzi thabiti ya ndani ambayo yanakinzana na UCoC;
    • Kukataa miundo ya kujitawala ya ndani na timu kutekeleza UCoC;
    • Ukosefu wa rasilimali au ukosefu wa nia ya kushughulikia maswala ambayo yanazuia utekelezwaji wa kutosha wa UCoC kupitia michakato ya kujitawala ya ndani;
  • Kufanya uchunguzi wowote muhimu ili kutatua malalamiko na rufaa zilizotajwa;
  • Kutoa rasilimali kwa jamii kuhusu mbinu bora za UCoC, kama vile nyenzo za mafunzo ya lazima, uhakikisho wa ubora wa nyenzo za mafunzo zinazoundwa na wanaharakati na mashirika ambayo yanapita zaidi ya nyenzo za msingi za mafunzo za UCoC ambazo U4C yenyewe inasimamia, na rasilimali nyingine inapohitajika;
  • Kutoa tafsiri ya mwisho ya Miongozo ya Utekelezaji ya UCoC na UCoC kama mahitaji hayo yatatokea, kwa ushirikiano na miundo ya utekelezaji ya wanajamii;
  • Kutathmini ufanisi wa utekelezaji wa UCoC na kutoa mapendekezo ya kuboresha.

Nyongeza ya hapo juu:

  • U4C haitachukua kesi ambazo hazihusishi ukiukaji wa UCoC, au utekelezaji wake.
  • U4C inaweza kukabidhi mamlaka yake ya mwisho ya kufanya maamuzi isipokuwa katika hali ya masuala mazito ya kimfumo. Majukumu ya U4C yanaelezwa katika muktadha wa miundo mingine ya utekelezaji katika 3.1.2 ya Miongozo ya Utekelezaji ya UCoC.

1.3. Uanachama

U4C itajumuisha wanajumuiya 16 wanaopiga kura na hadi wanachama wawili wasio wapiga kura walioteuliwa na Shirika la Wikimedia Foundation. Kila mwanachama anayepiga kura anatimiza muhula wa miaka miwili, isipokuwa uchaguzi wa kuapishwa (ona 3.2).

Shirika la Wikimedia Foundation linaweza kuteua hadi wanachama wawili wasiopiga kura na kuchagua wafanyakazi wa ziada wa usaidizi kama ilivyoombwa na U4C.

1.4. Mgongano wa Kimaslahi

Washiriki wa upigaji kura binafsi wa U4C hawalazimiki kujiuzulu kutoka kwenye nyadhifa zingine (km. msimamizi wa eneo (sysop), mwanachama wa ArbCom) lakini hawawezi kuajiriwa kama wafanyakazi au wakandarasi na Shirika la Wikimedia Foundation au mashirika yanayohusiana na Shirika wala hawawezi kuwa wanachama wa Bodi ya Wadhamini ya Wikimedia Foundation.

2. Uchaguzi na Masharti

2.1. Ustahiki wa Mwanachama

Kila mwanachama na mgombea lazima:

  • Kuzingatia UCoC.
  • Awe na angalau umri wa miaka 18 na atie saini makubaliano ya Usiri kwa taarifa zisizo za umma (NDA) na Shirika la Wikimedia Foundation punde tu atakapochaguliwa.
  • Awe hajazuiwa kwenye mradi wowote wa Wikimedia wala kuwa na marufuku inayoendelea ya tukio katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Wagombea ambao wamezuiwa wanaweza kukata rufaa kwa Kamati ya Uchaguzi, ambao wanaweza kutoa ruhusa maalum.
  • Waweze kutambulisha hadharani mradi au miradi yao ya wiki za nyumbani na kanda wanayotokea.
  • Wawe wanakidhi mahitaji mengine yoyote ya ustahiki yaliyobainishwa wakati wa mchakato wa uchaguzi.
  • Awe mwanachama aliyesajiliwa kwenye angalau mradi mmoja wa Wiki kwa angalau siku 365 zilizopita na awe na mabadiliko yasiyopungua 500.

Kamati ya Uchaguzi itakuwa na mamlaka ya mwisho ya kuamua ikiwa wagombea wanatimiza masharti ya kustahiki.

2.2. Mgawanyo wa Viti

2.2.1. Mgawanyo wa Kikanda

Ili kuhakikisha U4C inawakilisha utofauti wa harakati, wawakilishi wanane, na mwakilishi mmoja kutoka kila kanda watachaguliwa kwa mgawanyo wa kikanda. Kulingana na utaratibu wa kikanda wa Shirika la Wikimedia Foundation, mgawanyo wa kikanda utakuwa kama ifuatavyo:

  • Amerika ya Kaskazini (Marekani na Kanada)
  • Ulaya ya Kaskazini na Magharibi
  • Amerika ya Kusini na Caribbean
  • Ulaya ya Kati na Mashariki (CEE)
  • Nchi za Kiafrika za Kusini mwa Jangwa la Sahara
  • Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini
  • Mashariki, Kusini Mashariki mwa Asia na Pasifiki (ESEAP)
  • Asia ya Kusini

2.2.2. Jumuiya kwa ujumla =

Wawakilishi nane kutoka Jumuiya kwa ujumla watachaguliwa.

2.3. Masharti

Uanachama wa U4C utakuwa wa kipindi cha miaka miwili, isipokuwa uchaguzi wa kwanza.

Kwa uchaguzi wa kwanza, Wagombea wa Kanda watahudumu mihula ya miaka miwili na wajumbe wote watahudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

2.4. Chaguzi

Uchaguzi wa kila mwaka wa kuchagua wapiga kura wa U4C utaangaliwa na U4C na kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi, kwa ushirikiano na U4C. Kwa uchaguzi wa kwanza, U4CBC itachukua nafasi ya U4C.

Wagombea watalazimika kukidhi mahitaji ya uanachama yaliyotajwa katika kifungu cha 2.1.

Uchaguzi wa kuapishwa wa U4C utafanyika haraka iwezekanavyo, kufuatia kukamilika kwa mchakato wa uidhinishaji wa Mkataba wa U4C.

Mchakato wa Uchaguzi unafuata ratiba ifuatayo:

  • Kubainisha tarehe ya uchaguzi, ratiba yake na idadi ya viti vya kikanda na vikubwa vya U4C angalau mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa uchaguzi.
  • Kufunguliwa kwa mchakato wa uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi
  • Kipindi cha uteuzi - Mapendekezo yanakubaliwa wakati huu
  • Kipindi cha uhakiki wa wagombea
  • Kipindi cha Maswali na Majibu - Watahiniwa watajibu maswali kutoka kwa jamii
  • Kipindi cha kupiga kura - Wapiga kura wanaostahiki wanaweza kuwapigia kura wagombea

2.5. Mchakato wa Kupiga Kura

  • Upigaji kura unafanywa kwa kura ya siri, huku wapiga kura wakionesha uungaji mkono, kupinga na kura zisizoegemea upande wowote kwa kila mgombea.
  • Wapiga kura wanaweza kuwapigia kura wagombea kutoka kanda zote.
  • Kura za zisizopigia upande wowote hazitahesabiwa.
  • Ustahiki wa wapiga kura utaamuliwa na Kamati ya Uchaguzi.
  • Mgombea lazima awe na asilimia 60 au zaidi ya kura za wanaomuunga mkono/(wanaomuunga mkono + wanaompinga). Baada ya sifa hii:
    • Kwa kila mgombea idadi ya wapinzani itatolewa kutoka kwenye idadi ya wafuasi. Wagombea walio na tofauti kubwa zaidi watachaguliwa kwa kila kiti.
    • Iwapo watahiniwa wawili wana tofauti sawa basi asilimia inayokokotolewa kwa wanaomuunga mkono/(wanaomuunga mkono + wanaompinga) itatumika kama kivunja-mfungamano.

Baada ya kipindi cha kwanza cha U4C, U4CBC itavunjwa na U4C itaanza kazi mapema iwezekanavyo.

2.6. Nafasi wazi

Ikiwa kuna kiti kitupu, iwe kwa sababu ya kujiuzulu, kuondolewa, au hakuna mgombea aliyechaguliwa kwa kiti cha eneo husika katika uchaguzi, U4C inaweza kukiacha kiti hicho kitupu na kujaza nafasi hiyo kwa muda mfupi wakati wa uchaguzi ujao, au U4C inaweza kuitisha kikao maalum. Namna nyingine ya ziada katika hali ya kujiuzulu au kuondolewa ni kwamba U4C inaweza kuteua mwanachama ambaye aligombea ndani ya uchaguzi wa hivi karibuni zaidi na kupata angalau 60% ya uungwaji mkono.

Wanachama wanaojaza kiti kilicho wazi watatumia muda uliosalia wa kiti wanachojaza.

3. Taratibu za Ndani

U4C inaweza kuunda au kurekebisha taratibu zao za ndani ili mradi tu ziko ndani ya uwezo wao. Kunapaswa kuwa na usawa na kutopendelea miongoni mwa wanachama katika michakato ya kikundi. Wakati wowote inapofaa, U4C inapaswa kualika maoni ya jumuiya kuhusu mabadiliko yaliyokusudiwa kabla ya kuyatekeleza.

3.1. Sera ya Ndani na Mfano

U4C haiundi sera mpya na haiwezi kurekebisha au kubadilisha UCoC na Miongozo yake ya Utekelezaji. U4C badala yake inatumika na kutekeleza UCoC kama inavyofafanuliwa na upeo wake.

Maamuzi ya awali yanaweza kutiliwa maanani kwa kiwango tu ambacho yanabaki kuwa muhimu katika muktadha wa sasa, kwani sera za jumuiya, miongozo na kanuni hubadilika kadri muda unavyopita.

U4C, hata hivyo, inaweza kupendekeza mabadiliko kwenye UCoC na Miongozo ya Utekelezaji kwa Shirika la Wikimedia Foundation na jumuiya kuzingatia kama sehemu ya mchakato wa ukaguzi wa kila mwaka unaoandaliwa na U4C.

3.2. Mwenendo wa wanachama wa U4C

Wanachama wa U4C wanapaswa:

  • Kushiriki kikamilifu katika kazi ya U4C, na waijulishe U4C mwanzoni mwa kutokuwepo kwao katika ushiriki kwenye U4C.
  • Kujibu kwa wakati mwafaka kuhusiana na mwenendo wao.
  • Kudumisha usiri wa taarifa za kibinafsi zinazoshirikishwa na U4C, ikijumuisha mawasiliano ya kibinafsi na taarifa za kibinafsi zisizo za umma.
  • Kudumisha uhusiano wa kindugu na wanachama wenzao wa U4C na kufanya kazi kwa tija ili kutatua mizozo baina ya watu.
  • Kuzingatia dhana kwamba hakuna mwanachama wa U4C aliye na nguvu zaidi au mwenye nguvu ndogo kuliko mwanachama mwingine yeyote.
  • Kujitahidi kutenda kwa njia ya uwazi, ukitoa maelezo ya maamuzi yao inapowezekana huku ukihifadhi usiri ufaao.
  • Kuwa na ujuzi kuhusu sera za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mwongozo wa Kimataifa wa Mwenendo na Nidhamu, na unapaswa kufanya kazi ili kupata ujuzi wa sera na utamaduni wa ndani kwa kazi yoyote ambayo U4C inashughulikia.

Mwanachama yeyote wa U4C ambaye anakiuka mara kwa mara au kwa kiasi kikubwa matarajio yaliyoainishwa hapo juu anaweza kusimamishwa au kuondolewa kwa azimio la kamati ya umma. Azimio hili la kamati ya umma lazima liungwe mkono na theluthi mbili ya wanachama wote wa U4C, bila kujumuisha yafuatayo katika mchakato wa kupiga kura:

  • Mwanachama wa U4C anayekabiliwa na kusimamishwa au kuondolewa, na;
  • Mwanachama yeyote wa U4C ambaye hajibu ndani ya siku 30 kwa majaribio yoyote ya kuomba maoni yake kuhusu azimio hilo kupitia mbinu zote zinazojulikana za mawasiliano ya maandishi.

3.3. Uwazi na Usiri

Malalamiko yatakayokubaliwa yataripotiwa hadharani kwenye Wiki na angalau taarifa ndogo.

Kazi iliyoamuliwa itaripotiwa hadharani kwenye wiki, ikitaja majina ya akaunti, miradi, tarehe na maelezo ya kesi ya msingi. Ikiwa maelezo yoyote hayafai kwa ripoti za umma kwa sababu ya faragha au sababu za kisheria, ripoti zitaficha kwa kupanua maelezo au hata kuondoa taarifa husika kadri itakavyofaa.

Ikiwa mwanachama wa U4C atakiuka makubaliano ya usiri, ni muhimu kushughulikia suala hilo kupitia hatua zinazofaa za ndani za kinidhamu, ikiwa ni lazima. Ukiukaji wa Sera ya Faragha, Ufikiaji wa sera ya data ya kibinafsi isiyo ya umma, Sera ya CheckUser na sera ya Uangalizi pia huchunguzwa na Tume ya Ombuds. Kamati ifanye uchunguzi ili kubaini kama uvunjaji huo ulikuwa wa makosa au makusudi. Kamati inaweza kupendekeza kwa Shirika la Wikimedia Foundation kubatilisha makubaliano ya usiri ikiwa uchunguzi utabaini kuwa jambo husika limethibitishwa.

3.4. Akidi

U4C inaweza kuketi na idadi yoyote ya wanachama, lakini hakuna uamuzi au kura inayoweza kuchukuliwa na Kamati isipokuwa akidi ya 50% (wanachama 8) ya wanachama wanaopiga kura (wanachama 16) imefikiwa. Iwapo hakuna akidi, U4C itaendelea kufanyia kazi masuala ambayo hakuna kura inahitajika na kuitisha uchaguzi maalum ukihitajika.

3.5. Kamati ndogo ndogo

Kamati ya Ujenzi ya U4C inapendekeza kwamba angalau kamati ndogo mbili ziundwe ndani ya U4C wakati wa kuunda. Kamati ndogo moja ya kuzuia, mafunzo na ripoti zinazohusiana na kazi ya U4C na kamati ndogo ya pili ya kukagua na kushughulikia kesi.

3.6. Usaidizi wa Kimuundo

Kazi fulani inaweza kuhitaji usaidizi fulani wa kimuundo. U4C inaweza kuunda kamati ndogo au kuteua washiriki kwa kazi au majukumu fulani kadri itakavyofaa kushughulikia kazi ya U4C.

Shirika la Wikimedia Foundation litatoa zana kwa Kamati ili kuisaidia kukamilisha kazi yake (k.m. zana salama za mawasiliano, wiki ya kibinafsi, n.k). Shirika linaweza kuteua wafanyakazi wa ziada kadri itakavyoombwa na U4C.

3.7. Zana

Kamati inaweza kuchukua hatua zote inazoona zinafaa na zinazolingana ili kuzingatia mamlaka yake na kushughulikia kushindwa kwa utaratibu wa kutekeleza UCoC ipasavyo kulingana na mwongozo wa utekelezaji na sera hii. Hii ni pamoja na kuunda au kuomba haki za mtumiaji kwa wanakamati au wajumbe wake wa usimamizi (zana za Wiki za ndani/kitandawazi na MediaWiki), zana za usaidizi kama vile orodha za utumaji barua na wiki ya kibinafsi, na zana zingine kama vile Mfumo wa Kuripoti Matukio ya Kibinafsi ili kusaidia shughuli za U4C, itakayoundwa na kusimamiwa na Shirika la Wikimedia Foundation na wasimamizi wakati wa muda wa wanachama wa U4C.

Haki zozote zinazotolewa kwa madhumuni ya kamati ya U4C lazima zitumike tu kwa vitendo vya U4C, uchunguzi na kesi za dharura isipokuwa ziwe na haki zingine za usimamizi zinazotolewa kutoka kwa michakato ya ndani au ya kimataifa.

3.8. Kukataa

Mwanachama wa U4C anaweza kujiepusha na kazi yoyote, au kipengele chochote cha kazi, kwa maelezo au bila maelezo, na inahitajika kufanya hivyo pale mgongano wa kimaslahi unapotokea. Hali hii inaweza kusababisha mwanachama wa U4C kushiriki katika majadiliano kuhusu kazi, lakini si mchakato wa kupiga kura.

Mwanachama yeyote wa U4C anayeshiriki katika nafasi yake ya uwanachama wa U4C kuhusu kazi kutoka kwa mradi au mshirika anaoshiriki ana jukumu la kuchukua uamuzi wa kujiuzulu. Wanachama wa U4C hawatashiriki katika kazi ikiwa wamehusika moja kwa moja na kazi hiyo kutokana na nyadhifa zao nyingine au shughuli nyinginezo. Uamuzi huu bado unaweza kupigiwa kura na wanachama wote wa U4C. Mwanachama yeyote wa U4C anaweza kuchagua kujiondoa kwenye kura ya kukataa, lakini bado akashiriki katika majadiliano ya kukataa kazi.

Kwa kawaida, mgongano wa kimaslahi kuhusu kazi ya U4C hujumuisha kuhusika kwa kibinafsi katika kiini cha mzozo au ushiriki mkubwa wa kibinafsi na mmoja wa wahusika wanaohusika katika kazi hiyo. Mwingiliano wa awali na wahusika kama mhariri wa kawaida, msimamizi au mwingiliano wa U4C kwa kawaida sio sababu za kukataa.

3.8.1. Mchakato na taratibu kuhusu kuomba kujiepusha na kazi fulani kwa mwanachama

Iwapo mtu anaamini kuwa mwanachama wa U4C anapaswa kujiepusha na kazi fulani ya U4C, mtu huyo atalazimika kutuma ombi lake kwa U4C akiomba mtu huyo ajiondoe na atambue kazi hiyo na kueleza sababu zake. Mwanachama wa U4C anaweza kutii ombi la kujiondoa au kura ya uanachama wa U4C itafanyika, bila kujumuisha mwanachama au wanachama walioathirika.

U4C inapaswa kujibu ombi kabla ya kuanza kupigia kura kazi husika. Maombi ya kujiepusha baada ya kazi husika kuingia katika hatua ya kupiga kura hayatakubaliwa, isipokuwa katika hali isiyo ya kawaida.

3.9. Mahusiano

U4C inaweza kutoa ushauri rasmi au usio rasmi na tafsiri ya UCoC. Inapowezekana, U4C inapaswa kujibu maombi kutoka kwa vyombo vingine vya juu vya kufanya maamuzi, Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Wikimedia Foundation, au Shirika la Wikimedia Foundation kwa ushauri au ufafanuzi. Vikundi vingine au watu binafsi wanaweza pia kuomba ushauri na tafsiri kutoka kwa U4C. Inapofaa, U4C inapaswa kuweka hadharani ushauri na tafsiri yao rasmi.

3.9.1. Uhusiano na miundo mingine ya kiutawala ya harakati

Kulingana na Miongozo ya Utekelezaji ya UCoC, kulingana na hali halisi, U4C inaweza kufanya kazi kama chombo cha juu cha kufanya maamuzi kuhusu UCoC na kama kikundi cha rika kwa vyombo vingine vya juu vya kufanya maamuzi. Jukumu la Kamati ni kutoa rasilimali kwa jamii kuhusu mbinu bora za UCoC na kuwa suluhu la mwisho katika hali ambapo kuna masuala ya kimfumo ya vikundi vya ndani ili kutekeleza UCoC wao wenyewe.

Kwa kesi zinazohusisha wafanyakazi Washirika, U4C inapaswa kushughulikia kesi hiyo kwa pamoja na Mshirikka na/au AffCom. U4C inaweza kuchukua hatua kuhusu wafanyakazi katika nafasi za harakati za Wikimedia na inaweza kupendekeza hatua nyingine kwa Washirika.

Miundo ya utawala ya vuguvugu inaweza pia kuelekeza kesi za utekelezaji wa UCoC au rufaa, hata zile ambazo kwa kawaida hazingekuwa katika upeo wa U4C, kwa U4C. U4C inaweza kuamua ikiwa itasikiliza au kutosikiliza kesi hizo au rufaa kulingana na taratibu zake za kawaida.

Maombi ya ushauri au tafsiri au marejeleo ya kesi yanapaswa kufanywa kwa ujumla kwenye Meta-wiki, isipokuwa iwapo haifai kwa sababu za kifaragha. Kwa hali zinazohusisha faragha, matumizi ya barua pepe maalum ya U4C yanatarajiwa.

4. Kazi

4.1. UCoC na Nyenzo za Mafunzo ya Utekelezaji

U4C itasimamia uundaji na udumishaji wa rasilimali za mafunzo, na pia kuratibu na Shirika la Wikimedia Foundation juu ya tafsiri ya nyenzo hizo za mafunzo.

Moduli tatu za msingi za mafunzo zitashughulikia kama ilivyoagizwa katika miongozo ya utekelezaji itajumuisha:

  • Mwelekeo
  • Utambulisho na kuripoti
  • Kesi tata na rufaa

Moduli hizi zitapatikana kwa umma, kwenye majukwaa kama vile Learn.wiki, na lazima zitafsiriwe kwa ushirikiano na Shirika la Wikimedia Foundation katika lugha nyingi iwezekanavyo. Orodha au idadi ya lugha itaamuliwa na U4C.

Kando na kutoa moduli za mafunzo, U4C inaweza kuchunguza na kusaidia njia nyingine za mafunzo, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa jumuiya kama vile Shirika la Wikimedia Foundation na washirika wake pekee.

U4C inaweza pia kushirikisha mbinu bora za ukiukaji wa UCoC na masuala yanayohusiana na kutoa uhakikisho wa ubora na uidhinishaji wa nyenzo za mafunzo za UCoC zilizoundwa na wadau wengine wa harakati baada ya ombi.

Kama vile UCoC yenyewe inavyofafanua viwango vya chini, na kualika na kuhimiza jumuiya kujenga juu ya viwango hivyo vya chini vya tabia, wadau wa harakati wanakaribishwa kujenga na kuboresha nyenzo za msingi za mafunzo.

4.2. Mamlaka, shauri, uamuzi, rufaa

4.2.1. Mamlaka

U4C ina mamlaka ndani ya nafasi zote zinazohusiana na Wikimedia mtandaoni na nje ya mtandao ndani ya upeo wa mamlaka yake kama ilivyofafanuliwa na Miongozo ya Utekelezaji. U4C haitachukua kesi ambazo hazihusishi ukiukaji wa UCoC, au utekelezaji wake. U4C inaweza kukasimu mamlaka yake ya mwisho ya kufanya maamuzi isipokuwa katika matukio ya hitilafu za kimfumo.

U4C haina mamlaka, isipokuwa kama ilivyobainishwa katika sehemu za uhusiano hapo juu, juu ya: (i) hatua rasmi za Shirika la Wikimedia Foundation au wafanyakazi wake; (ii) Masuala shirikishi ya Wikimedia ya uhusiano wa ajira yanayosimamiwa na sheria na kanuni za mamlaka ya kampuni husika.

Isipokuwa katika matukio ya hitilafu za kimfumo, U4C haitakuwa na mamlaka wakati chombo cha maamuzi cha ngazi ya juu kilichotiwa saini na NDA kipo (Kamati za Usuluhishi, Kamati ya Ushirikiano, Baraza la Kimataifa, Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Maadili ya Kiufundi, wasimamizi), kuthibitisha. ufanisi wa kujitawala. U4C inapaswa pia kuheshimu kanuni ya harakati ya ugatuaji, ikielewa kuwa UCoC inapaswa kutekelezwa katika kiwango cha ndani kinachofaa zaidi iwezekanavyo.

U4C ina mamlaka juu ya masuala yote yanayosikilizwa nayo, ikiwa ni pamoja na taratibu zinazohusiana za utekelezaji, na inaweza, kwa uamuzi wake pekee, kurejea mchakato wowote wakati wowote isipokuwa suala hilo likabidhiwe kwa Shirika la Wikimedia Foundation katika nafasi yake kama mtoa huduma wa jukwaa kutokana na masuala ya kisheria.

4.2.1.1. Kushindwa kwa utaratibu

Masuala yanayohusiana na kushindwa kwa utaratibu yanaweza kuibuliwa na mtu yeyote na U4C inaweza kuchagua kufungua uchunguzi kwa angalau usaidizi mwingi. Iwapo Shirika au chombo cha kufanya maamuzi cha ngazi ya juu kitaomba uchunguzi kuhusu kutofaulu kwa utaratibu, U4C itafungua uchunguzi. Kutokubaliana kwa nia njema juu ya jinsi ya kutafsiri UCoC haitoshi kubainisha kuwa shirika la kufanya maamuzi la ngazi ya juu limeshindwa kimfumo kutekeleza kanuni.

Kwa mujibu wa miongozo ya utekelezaji iliyoidhinishwa na jumuiya, U4C inaweza kuchukua hatua zote inazoona zinafaa na sawia kushughulikia hitilafu za kimfumo (k.m. kunasa mradi) ili kutekeleza UCoC ipasavyo. U4C inaweza kutegemea ripoti za Shirika la Wikimedia Foundation na vikundi vingine vya harakati au inaweza kuomba ripoti yake ya nje inapofanya uamuzi wake. Vikwazo vya kushindwa kimfumo kutekeleza UCoC ni pamoja na anuwai kamili ya hatua, hadi na kujumuisha kufungwa kwa wiki. Ripoti inapaswa kuchapishwa kwa kuzingatia jumuiya ya kimataifa baada ya uamuzi.

4.2.2. Mashauri

4.2.2.1. Kuomba mapitio ya uamuzi

Maombi ya ukaguzi wa uamuzi lazima yawasilishwe kwa njia iliyoteuliwa na U4C. U4C inaweza kukubali au kukataa jambo lolote kwa hiari yake; itazingatia, lakini haitafungwa na maoni ya wahusika kwa ombi na watumiaji wengine wenye ujuzi.

4.2.2.2. Fomu za shauri
  • Mashauri ya Kawaida: Kwa chaguo-msingi, vikao ninatakiwa kuwa ni vya hadharani na hufuata taratibu zilizochapishwa kwenye kurasa husika za U4C. Uendeshaji unaweza kuwa wa faragha ikiwa U4C itazingatia kwamba kesi ya umma inaweza kusababisha madhara yasiyolingana - kwa kawaida ambapo faragha, unyanyasaji, au masuala ya kisheria yanahusika - kwa washiriki wanaoendelea, watu wengine, au inaweza kuathiri vibaya sheria, kiufundi ya Shirika la Wikimedia Foundation, na wajibu wa mtoa huduma wa jukwaa unaohusiana na umma. Wahusika wataarifiwa kuhusu kusikilizwa kwa faragha na kupewa fursa nzuri ya kujibu kile kinachosemwa kuwahusu kabla ya uamuzi kufanywa.
  • Hatua iliyoharakishwa: Pale ambapo ukweli wa jambo haupingikiwi kwa kiasi kikubwa, U4C inaweza kutatua mgogoro huo kwa kura bila utaratibu wa kawaida.

4.2.2.3. Ushiriki

Mwanachama ambaye muda wake unaisha wakati kesi inasubiri anaweza kusalia katika kesi hiyo hadi kukamilika kwake. Wanachama wapya walioteuliwa wanaweza kuanza kazi katika jambo lolote lililo mbele ya U4C mara moja kuanzia tarehe ya uteuzi wao.

Taarifa zinaweza kuongezwa kwa kurasa za kesi na mtumiaji yeyote aliye na habari na anayevutiwa. U4C inaweza kuweka sheria zaidi inapohitajika kwa uwasilishaji wa taarifa. Watumiaji wanaweza kujibu taarifa kuwahusu wao na U4C itafanya juhudi za nia njema kuwasiliana na mtumiaji yeyote ambaye ni mhusika wa kesi; kushindwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha maamuzi kufanywa bila ushiriki wao. Wahariri wote wanatakiwa kuchukua hatua kulingana na UCoC kwenye kurasa za kesi za U4C, na wanaweza kukabiliwa na vikwazo ikiwa hawatafanya hivyo.

4.2.2.4. Kukubalika kwa ushahidi

Katika kesi zote, ushahidi unaokubalika ni pamoja na:

  1. Mabadiliko yote na maingizo ya kumbukumbu, ikijumuisha mabadiliko yaliyofutwa au yaliyofichwa na maingizo ya kumbukumbu kutoka kwa miradi ya mtandaoni, majukwaa na huduma ndani ya mawanda ya U4C;
  2. Ushuhuda na ushahidi kutoka kwenye matukio ya nje ya mtandao kama inavyoonekana inafaa na U4C.

Ushahidi unakubalika katika lugha zote zinazoungwa mkono na majukwaa na huduma za Wikimedia Foundation. Iwapo U4C inahitaji nyenzo za ziada za uchakataji wa rasilimali zilizopokewa, inaweza kuratibu na Shirika la Wikimedia Foundation kama kamati nyingine za jumuiya za kujitawala zinazoshirikiana na mtoa huduma wa jukwaa zinavyofanya. Ushahidi unaotokana na mawasiliano ya faragha (ikiwa ni pamoja na, lakini sio tu, tovuti nyingine, mabaraza, vyumba vya mazungumzo, kumbukumbu za IRC, mawasiliano ya barua pepe) unakubalika tu kwa idhini ya awali ya U4C.

Ushahidi unaweza kuwasilishwa kwa faragha, lakini U4C kwa kawaida hutarajia ushahidi kuchapishwa hadharani katika shughuli zote za umma isipokuwa kama kuna sababu za msingi za kutofanya hivyo, au imebainika kuwa kesi hiyo itakuwa ya faragha. U4C itaamua ikiwa itakubali kila uwasilishaji wa ushahidi wa kibinafsi kwa uhalali wake na, ikiwa itakubaliwa, ushahidi huo utazingatiwa kwenye kikao cha faragha.

4.2.2.5. Maagizo ya muda mfupi

Wakati wowote kati ya ombi la kesi kufanywa na kufungwa kwa kesi, U4C inaweza kutoa maagizo ya muda mfupi, kuzuia mienendo ya wahusika, au watumiaji kwa ujumla, kwa muda wa kesi.

4.2.3. Uamuzi

4.2.3.1. Muundo wa maamuzi

Maamuzi yameandikwa kwa Kiingereza kilicho wazi, kifupi cha kawaida na lugha ya msingi inayohusiana na kesi inayohusika; kwa kawaida ikijumuisha: (i) muhtasari wa kanuni kuu, (ii) matokeo ya ukweli, (iii) kuweka suluhu na maamuzi, na (iv) kubainisha mipango yoyote ya utekelezaji. Ambapo maana ya kifungu chochote haijulikani kwa mwanachama yeyote wa U4C, wahusika, au wahariri wengine wanaovutiwa, inaweza kufafanuliwa endapo kutakuwa na ombi.

4.2.4. Rufaa

4.2.4.1. Kukubalika kwa rufaa

Rufaa za watumiaji waliozuiwa, waliopigwa marufuku, au wa kufanana na hao waliowekewa vikwazo maranyingi hufikiwa kwa barua pepe.

4.2.4.2. Rufaa ya maamuzi

Upande wowote katika kesi unaweza kuomba U4C kufikiria upya au kurekebisha uamuzi, ambao U4C inaweza kukubali au kukataa kwa hiari yake. U4C inaweza kuhitaji kiwango cha chini cha muda ambao lazima upite tangu kupitishwa kwa uamuzi huo, au tangu ombi lolote la awali la kuangaliwa upya, kabla ya kuipitia.

4.3. UCoC na Miongozo ya Utekelezaji- Mapitio na Mabadiliko

4.3.1. Ufuatiliaji wa UCoC

U4C itafuatilia kwa karibu tafiti za Mtazamo wa usalama wa Shirika, mienendo yake yenyewe ya upakiaji, na maoni kutoka kwa michakato ya kujitawala kwa jumuiya ili kutambua changamoto za kujitawala kwa ufanisi kwa jumuiya ili kutekeleza UCoC. Wasiwasi uliotambuliwa utarekodiwa hadharani kwenye ubao wa matangazo wa U4C, kushughulikiwa kama inavyostahili, au kuwasilishwa wakati wa ukaguzi wa kila mwaka wa UCoC & EG.

Kabla ya ukaguzi wa kila mwaka, U4C itakamilisha yafuatayo:

  • Kuwasiliana na watendaji katika jumuiya yetu ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na:
    • Wasimamizi
    • Wanachama wa ArbCom
    • Wakaguzi
    • Waangalizi
    • Wakabidhi
    • Jumuiya
  • Kutoa ripoti za uchunguzi wowote unaohitaji U4C kuchunguza UCoC au changamoto zinazohusiana na EG katika jumuiya. U4C ina wajibu wa kujadili ripoti hizi ili zijumuishwe katika pendekezo lao.
  • Kufungua ukurasa wa maoni kwenye Meta-wiki unaopatikana kwa kila mtu. Una sehemu ya mwanajamii yeyote kuripoti masuala kuhusu jinsi U4C, EG na UCoC hufanya kazi kama inavyotekelezwa. Ukurasa wa maoni umeunganishwa kwenye mawasiliano ya U4C kuhusu ukaguzi wa kila mwaka. U4C itaangalia maoni na maswali yaliyowekwa kwenye ukurasa huo, lakini hailazimiki kufuatilia kwa kina.
  • Ukurasa wa maoni wa Meta-wiki uliotajwa hapo juu una sehemu ya pili maalum inayowaruhusu wanajamii kushiriki mawazo ya kuboresha na kurekebisha. Hii inasaidia kukusanya mawazo kutoka kwa watu binafsi na inalenga kuwa wazi kwa sauti zote katika jamii. U4C inahitajika kusoma na kuamua ikiwa wanataka kupitisha mawazo haya wakati wa kuandaa pendekezo wakati wa mchakato wa kila mwaka.
  • U4C inapaswa kutafuta kikamilifu na kutambua mienendo yoyote mipya au isiyo ya kawaida ya tabia zisizokubalika zinazotokea katika harakati. Wanaweza kuchunguza mienendo, maoni ya jumuiya, na kuzingatia utafiti wa kitaaluma.

4.3.2. Mabadiliko ya Mkataba, Miongozo ya Utekelezaji au UCoC

Mabadiliko kwenye Mkataba, Miongozo ya Utekelezaji au UCoC yanahitaji idhini ya jumuiya. U4C itapanga kwa hiari yake mapitio ya kila mwaka ya UCoC, Miongozo ya Utekelezaji na Mkataba. Inajumuisha angalau:

  • Awamu ya tathmini ya maoni
    • Mwaliko wa kimataifa wa kutoa maoni
    • Tathmini ya maoni na hisia zilizokusanywa za jumuiya kutoka kwa vituo vyote
    • Maarifa kutoka kwa hali halisi ya utafiti kuhusu harakati zetu na mtandao kwa ujumla
  • Awamu ya kuandaa rasimu
    • Kujumuisha watendaji waliotathminiwa na maoni ya jumuiya, madokezo ya ndani kutoka kwenye ubao wa matangazo na ujuzi kutoka kwa hali halisi ya utafiti kuhusu harakati zetu na mtandao kwa ujumla.
    • Wakati wa awamu ya uandishi wa rasimu kuna angalau mazungumzo ya wamu tatu ya wazi ya jumuiya, kwa ajili ya ufikiaji kwa saa za eneo.
    • Rasimu iliyobadilishwa huchapishwa mara kwa mara wakati wa awamu ya kuandaa, kulingana na mtiririko wa kazi wa U4C ama baada ya kila kipindi au kila wiki.
    • Rasimu ya mwisho inakaguliwa na Idara ya Sheria ya Shirika la Wikimedia Foundation kwenye wiki.
  • Awamu ya kupiga kura
    • Kura zitapigwa na wanajumuiya walio na idhini ya > 60% au > 66%.
    • Tafsiri ya rasimu ya mwisho inayotangulia upigaji kura na kuendesha na kutangaza kura kulingana na maelezo ya U4C inahakikishwa na Shirika la Wikimedia Foundation.
    • Kura lazima iruhusu wapiga kura kupiga kura tofauti katika sehemu kuu za kibinafsi.

5. Faharasa

Kikundi cha Usambazaji cha Kikanda: Kikundi cha Usambazaji cha Kikanda ni kikundi cha wawakilishi waliochaguliwa na Jumuiya wa U4C wanaotoka katika kila kanda 8 zilizobainishwa na Wikimedia (Ulaya ya Kati na Mashariki (CEE); Amerika ya Kusini na Karibea; Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini; Amerika Kaskazini (Marekani na Kanada); Asia ya Kusini; Mashariki; Asia ya Kusini-Mashariki na Pasifiki (ESEAP); Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara; Ulaya Magharibi).

Jumuiya kwa Kundi Kubwa: Jumuiya kwa Kundi kubwa ni kundi la wawakilishi waliochaguliwa wa Jumuiya ya U4C wanaoshiriki katika mradi wowote wa Wikimedia. Hata hivyo si zaidi ya wanachama wawili wanaweza kuchaguliwa kutoka mradi mmoja wa wiki ya nyumbani, huku pia idadi hii ikiwa ni pamoja na wanachama waliochaguliwa Katika chama cha Kikanda cha usambazaji.


  NODES
Done 1
eth 1