Brandenburg ni moja ya majimbo 16 ya kujitawala ya Ujerumani lenye wakazi milioni 2,6 kwenye eneo la 29 056 km². Mji mkuu ni Potsdam. Waziri mkuu ni Matthias Platzeck wa chama cha SPD anayesimamia serikali ya mseto.

Frankfurt, Brandenburg
Mahali pa Brandenburg katika Ujerumani
bendera ya Brandenburg

Jiografia

hariri

Brandenburg ni sehemu ya Ujerumani inayozunguka jimbo la mji mkuu wa Berlin; menginevyo imepakana na Poland upande wa mashriki na majimbo ya Kijerumani ya Mecklenburg-Pomerini (Mecklenburg-Vorpommern), Saksonia ya chini (Niedersachsen), Saksonia (Freistaat Sachsen) na Saksonia-Anhalt (Sachsen-Anhalt).

Uso wa nchi ulifinyangwa na barafuto kubwa za Enzi ya Barafu zilizoacha hasa mchanga kwa umbo la safu za vilima vidogo ambavyo kwa jumla havizidi kimo cha mita 100 juu ya UB. Kwa hiyo sehemu kubwa ya mashamba haina rutba nzuri lakini kuna pia maeneo kadhaa yenye rutba. Kilimo kinategemea umwagiliaji na kuna maeneo mapana ya misitu.

Mito mikubwa haipiti jimboni isipokuwa mto Havel lakini mito mikubwa ya Elbe na Oder ni mipaka ya Brandenburg.

Kuna mihji minne mikubwa kidogo ambayo ni mji mkuu Potsdam uliopo mpakani wa Berlin halafu miji ya viwanda Brandenburg an der Havel, Cottbus na Frankfurt (Oder) (ambayo ni tofauti na Frankfurt katika Hesse).

Historia

hariri

Eneo la jimbo lilikaliwa na makabila ya Waslavoni hadi mwaka 929 lilipovamiwa na Wajerumani. Baada ya kutekwa kabisa na makabaila Wajerumani Brandenburg ilikuwa dola la kujitegemea ndani ya Dola Takatifu la Kiroma tangu 1157.

Watawala wapya walichukua walowezi Wajerumani na Waholanzi waliojenga vijiji na miji na wakazi kwa jumla walikuwa mchanganyiko wa Waslavoni na Wajerumani. Hadi leo kuna vijiji kadhaa vya Wasorbia wanaotumia lugha ya Kislavoni hata wakiwa Wajerumani kisiasa.

Tangu 1415 nasaba ya Hohenzollern kutoka Ujerumani ya kusini ilipewa utemi wa Brandenburg. Nasaba hii iliendelea kutawala jimbo hadi 1918 na kuifanya dola kubwa kabisa katika Ujeruami na pia dola mihimu katika Ulaya.

Mwaka 1618 watawala walirithi eneo la Prussia lililowahi kuwa dola la Wamisalaba. Baada ya uharibifu wa vita ya miaka 30 utemi wa Brandenburg iliendelea kuwa sehemu ya Ujerumai iliyofaulu kujenga uchumi na jeshi lake na kupanusha eneo. Mwaka 1701 mtemi wa Brandenburg alijiwekea taji la kifalme akajiita mfalme wa Prussia.

Hivyo Brandenburg iliendelea kuwa jimbo kubwa ndani ya ufalme wa Prussia. Prussia ilipoingia 1871 katika Dola la Ujerumani Brandenburg ilibaki kama mkoa mkubwa wa Prussia.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia Prussia ilibomolewa 1945 na Brandenburg ilikuwa sehemu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani (JKK) iliyoshikamana upande wa Umoja wa Kisovyeti. Hapa eneo la Brandenburg iligawiwa mwaka 1952 wakati majimbo ya kale yaliondolewa katika JKK na ardhi yake iliingia chini ya mikoa mitatu.

Baada ya maungano wa Ujerumani mwaka 1990 majimbo ya awali yalirudishwa kwenye eneo la JKK pamoja na Brandenburg.

Tangu 1996 kuna mipango ya kuunganisha majimbo ya Brandenburg na Berlin lakini maungano haya yalisimamishwa mara ya kwanza katika kura ya wananchi isipokuwa mipango inaendelea.

Picha za Brandenburg

hariri

Tovuti za Nje

hariri
 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:


 
Majimbo ya Ujerumani
 
Baden-WürttembergBavaria (Bayern)BerlinBrandenburgBremenHamburgHesse (Hessen)Mecklenburg-Pomerini Magharibi (Mecklenburg-Vorpommern)Saksonia Chini (Niedersachsen)Rhine Kaskazini-Westfalia (Nordrhein-Westfalen)Rhine-Palatino (Rheinland-Pfalz)Saar (Saarland)Saksonia (Sachsen)Saksonia-Anhalt (Sachsen-Anhalt)Schleswig-HolsteinThuringia (Thüringen)
  NODES