Bara la Antaktiki

bara
(Elekezwa kutoka Antaktiki)

Antaktiki ni bara lililopo kwenye ncha ya kusini ya dunia, kati ya bahari za Pasifiki, Atlantiki na Bahari Hindi.

Bara la Antaktiki
Antaktiki (kijani) katika ramani ya dunia.
Antaktiki kutoka angani.
Kituo cha kisayansi katika Antaktiki.

Jina "Antaktiki" linatokana na lugha ya Kigiriki likimaanisha "kinyume cha Aktiki", ambapo Aktiki ni eneo karibu na ncha ya kaskazini.

Bara hili lina eneo la kilomita za mraba milioni 14 na eneo hili limefunikwa karibu kabisa, yaani kwa asilimia 98% za eneo na theluji na barafu. Eneo lake ni kubwa kushinda Ulaya lakini hakuna mti hata mmoja. Bara hili linajulikana kama jangwa baridi.

Kwa sababu ya baridi kali katika bara hilo, ni bara pekee ambako binadamu hawaishi kwa namna ya kudumu, isipokuwa kuna watu 5,000, hasa wanasayansi, wanaokaa kwa muda katika vituo vyao.

Uvumbuzi

hariri

Bara la Antaktiki halikujulikana hadi karne ya 19, lakini wataalamu wa jiografia waliwahi kuhisi tangu zama za kale ya kwamba eneo kubwa la nchi kavu liko kwenye sehemu ya kusini ya dunia[1].

Kuanzia Aristoteli wataalamu waliamini ya kwamba dunia ilipaswa kuwa na uwiano fulani, hivyo kuwepo kwa bara kubwa ingekuwa lazima kulingana na mabara ya nusutufe ya kaskazini. Nchi hii isiyojulikana kwa muda mrefu ikaitwa kwa jina la Kilatini "terra australis" yaani "nchi ya kusini" na pia kuchorwa kwenye ramani za dunia zilizoanza kutengenezwa tangu safari za wavumbuzi Wareno waliozunguka dunia nzima kwa mara ya kwanza. Ila tu ramani hizi za kwanza zilikuwa kama njozi tu.

Kundi la kwanza la watu kufika kusini kwa kutosha na kuona kona ya barafu ya Antaktiki lilikuwa mwaka 1820 msafara wa kisayansi wa nahodha Fabian von Bellingshausen (Mjerumani Baltiki katika utumishi wa Tsar wa Urusi) akifuatwa mwaka uleule na nahodha Edward Bransfield wa Uingereza na tena Mmarekani Nathaniel Palmer.

Ila tu hakuna uhakika kama wavumbuzi hao walitambua tayari ya kwamba waliona bara jipya[2].

Pamoja na taarifa za mabaharia wengine waliopita kwenye pwani bado haikueleweka kama huko karibu na ncha ya kusini kulikuwa na visiwa mbalimbali au nchi kavu kubwa zaidi.

Ni misafara ya Wafaransa na Wamarekani mnamo mwaka 1840 iliyoweza kuthibitisha ya kwamba ncha ya kusini ilipatikana ndani ya bara jipya. Sasa shauku ya upelelezi ilififia kwa sababu haikueleweka kuna nini katika bara jipya.

Tangu mwaka 1890 Shirika la Kifalme la Jiografia (Royal Geographic Society) nchini Uingereza lilianza upya kusisitiza umuhimu wa utafiti wa Antaktiki iliyokuwa sehemu ya mwisho wa dunia isiyochunguliwa bado kabisa. Hapo misafara mbalimbali kutoka nchi tofauti ilifuatana na kupeleleza Antaktiki:

Katika miaka iliyofuata idadi ya misafara iliongezeka. Tangu mwaka 1929 eropleni zilitumika pia katika upelelezi. Ni hasa Mmarekani Richard Byrd aliyeongoza misafara kadhaa akitumia ndege akaweza kuweka msingi wa ramani kamili ya Antaktiki.

Jiografia

hariri
 
Ramani ya Antaktiki

Bara la Antaktiki lina takriban umbo la duara isiyo kamili ikizunguka ncha ya kusini. Pande zote inapakana na bahari: ni mahali ambako maji ya kusini ya Pasifiki, Atlantiki na Bahari Hindi yanakutana. Kwa namna nyingine inawezekana kusema inazungukwa na Bahari ya Kusini.

Eneo lake ni zaidi ya kilomita za mraba milioni 14, hivyo ni bara la tano duniani kwa ukubwa.

Umbali kutoka pwani hadi pwani uko baina ya kilomita 4,500 na 5,600.[3] Pwani ina urefu wa kilomita 17,968.

Sehemu za Antaktiki

hariri

Safu ya Milima ya kuvukia Antaktiki (kwa Kiingereza Transantarctic Mountains) inagawa bara katika sehemu mbili za Antaktiki Magharibi na Antaktiki Mashariki. Mpaka huu unalingana takriban na longitudo ya 180.

  • Antaktiki Magharibi ni upande mdogo zaidi. Ndani yake inagawiwa kwa rasi kadhaa kwa hiyo ina athira ya tabianchi kutoka bahari. Hata kama sehemu kubwa inafunikwa na barafu halijoto haishuki chini mno jinsi ilivyo upande wa mashariki. Rasi kubwa ni Rasi ya Antaktiki (ing. Antarctic Peninsula)
  • Antaktiki Mashariki inafanana zaidi na nusutufe, hakuna rasi au hori kubwa. Kwa hiyo tabianchi ni zaidi ya kibara. Uso unafunikwa na ganda la barafu lenye unene wa kilomita 1.6 au zaidi. Halijoto ya duni inayojulikana ilipimika mwaka 1983 kuwa sentigredi 89,4 chini ya sifuri.

Visiwa

hariri
 
Kisiwa cha Berkner jinsi inavyoonekana chini ya ngao ya barafu kwenye picha ya satelaiti

Visiwa kadhaa vinahesabiwa kuwa sehemu za Antaktiki. Baadhi ya visiwa hivyo viko ndani ya maji ya bahari. Vingine vinafunikwa na barafu ya kudumu na hivyo haionekani mara moja ya kwamba kuna kisiwa, maana sehemu nyingi ngao nene ya barafu ya kudumu inaingia baharini nje ya pwani.

Visiwa hivi ni pamoja na

  • Kisiwa cha Alexander ambacho ni kisiwa kikubwa cha Antaktiki; kina upana wa kilomita 200, urefu wa kilomita 378 na eneo la km² 49,070. Kinatengwa na bara kwa mfereji wa bahari mwenye upana wa kilomita 24-60, lakini yote inafunikwa kwa barafu ya kudumu ila tu sehemu ya pwani inaiongia katika maji ya bahari.
  • Kisiwa cha Berkner ambacho ni kisiwa kikubwa cha pili chenye urefu wa 320 km, upana wa 135 km na eneo la km² 43,873. Kinafunikwa kabisa na ngao ya barafu, hakionekani hata kutoka baharini.
  • Visiwa vya Joinville, Roosevelt, Ross na kadhalika.

Milima

hariri
 
Ncha za Milima ya kuvukia Antaktiki zinaonekana juu ya ngao ya barafu ya kudumu

Milima mingi ni sehemu ya Safu ya Milima ya kuvukia Antaktiki (au: milima transaktiki) ambayo ni safu ndefu yenye urefu wa kilomita 3,500 na kufikia kimo cha mita 4500 na zaidi. Ncha za milima yake mirefu zinaonekana juu ya uso wa ngao ya barafu inayofunika bara lote. Mlima mrefu katika safu hii ni Mlima Kirkpatrick wenye urefu wa mita 4528 juu ya UB.

Pale ambako Rasi ya Antaktiki inaanza kuna safu ya milima ya Ellsworth na huko uko mlima mrefu kabisa wa bara: ni Mlima Vinson wenye mita 4,892 juu ya UB.

Kuna pia volkeno kadhaa, nyingine zimelala, nyingine ziko hai. Volkeno hai ndefu inayotema moto barani ni Mlima Erebus wenye kimo cha mita 3,794: iko kwenye kisiwa cha Ross.

Ngao ya barafu ya kudumu

hariri
 
Ramani inaonyesha unene na uenezi wa ngao ya barafu ya Antaktiki:
- Rangi za buluu zinaonyesha unene wa ngao ya barafu kwa kutumia hatua za mita 1,000;
- buluu-nyeupe ni ngao ya barafu inapofunika maji ya bahari
- mistari minene: miinuko inayogawa mwendo wa barafu
- mistari membamba: mielekeo ya mwendo wa barafu
- nyekundu: sehemu zisizofunikwa na barafu

Tabia ya pekee ya Antaktiki ni ngao ya barafu inayofunika karibu uso wote wa nchi yake pamoja na sehemu za bahari ya karibu. Ngao ya barafu hii ni mkusanyiko mkubwa wa barafu duniani. Unene wake (yaani kimo juu ya ardhi) unafikia hadi mita 4,500.

Ngao ya barafu inajumlisha

  • asilimia 90 ya barafu yote duniani
  • asilimia 70 ya maji matamu yote duniani

Ni asilimia 2-3 za eneo lote la bara zisizofunikwa na barafu, yaani km² 280,000 tu.

Ngao hiyo ilianza kutokea miaka milioni kadhaa iliyopita. Uzito wake ni mkubwa na inaaminiwa ya kwamba bara lote lilishuka chini kiasi na kama siku moja ngao ya barafu itapotea litapanda tena juu mita kadhaa.

Barafu hii inashika maji mengi kiasi kwamba kama barafu yote itayeyuka siku moja uwiano wa bahari duniani kote itapanda juu takriban mita 61.

Mito, maziwa na barafuto

hariri
 
Ziwa la Lake Vostok - uso wa ziwa unaonekana kama eno tambarare; wakati wa joto kuna maji
 
Barafuto kubwa (mto wa barafu) barani Antaktiki

Tabia ya pekee ya Antaktiki ni pia uhaba wa mito. Mito yote inayotokea ni ya maji ya barafu ya kuyeyuka wakati wa "majira ya joto" katika miezi ya Februari na Machi. Katika sehemu nyingine ya mwaka mito yote inaonekana kama kanda la barafu. Mto mkubwa ni Onyx unaofikia urefu wa kilomita 30 ukiishia katika Ziwa Vanda.

Mito haina samaki, lakini katika ile mikubwa zaidi kuna mikrobi na algae.

Kuna maziwa kadhaa chini ya ngao ya barafu. Hata kama jotoridi yake ni chini ya sentigredi 0 baadhi yanaweza kuwa na maji ya kiowevu kwa sababu shinikizo kubwa ya ngao ya barafu linashusha halijoto ya kugandisha maji, hasa kama maji ni ya chumvi.

Barafu ya ngao haikai kimyakimya lakini yote ina mwendo ikifuata mtelemko wa uso wa nchi. Katika sehemu kadhaa barafu ina mwendo wa haraka zaidi na sehemu hizi zinaitwa "mito ya barafu" na ni aina ya barafuto. Mito ya barafu hii iko yenye urefu hadi kilomita mia kadhaa, upana wa 50 km na unene wa kilomita 2. Mwendo unafikia hadi mita 1.000 kwa mwaka. Pale inafikia kwenye ufuko wa bahari inajenga ulimi wa barafu inayosukumwa katika maji.

Hali ya kisiasa

hariri
 
Madai ya mataifa katika Antaktiki

Antaktiki si nchi wala dola na hakuna wenyeji au wananchi. Lakini madola mbalimbali yalitangaza madai ya kutawala sehemu za eneo lake. Madai haya hayalingani na mara kadhaa kuna mataifa mbalimbali yanayodai sehemu ileile.

Mataifa yanayodai kutawala sehemu za Antaktiki ni pamoja na Argentina, Australia, Chile, Ufaransa, New Zealand, Norwei na Ufalme wa Maungano.

Tangu mwaka 1961 kuna Mkataba wa Kimataifa kuhusu Antaktiki unaosimamisha madai yote ya utawala bila kuyafuta. Mataifa yote yana haki ya kuwa na vituo vya kisayansi. Mapatano ya kando yaliweka masharti makali kwa shughuli za kiuchumi na hadi sasa imewezekana kuzuia migodi na uchimbaji wa madini.

Mengineyo

hariri

Mtoto wa kwanza kuzaliwa barani huko alizaliwa mwaka 1984. Kwa sasa kuna shule kadhaa na kanisa moja la Waorthodoksi Warusi.

Marejeo

hariri
  1. [Aristoteli (mwaka 350 [KK]) katika fungu la tano la kitabu chake juu ya metrolojia] Archived 27 Juni 2015 at the Wayback Machine.: "kuna kanda mbili zinazoweza kukaliwa na watu duniani: moja kwa upande wa juu, au karibu na ncha yetu ya kaskazini, nyingine karibu na ncha nyingine, au ncha ya kusini"
  2. "Terence Armstrong, Bellingshausen and the discovery of Antarctica, Polar Record / Volume 15 / Issue 99 / September 1971, pp 887-889". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2016-08-20. Iliwekwa mnamo 2016-03-08.
  3. Ilhali ncha ya kusini iko takriban katikati ya bara, kila upande kutoka huko uko kaskazini.

Viungo vya nje

hariri
  NODES
mac 4
os 11
text 1
web 1