Atlantiki ni bahari kubwa inayotenganisha Amerika upande wa magharibi na Afrika na Ulaya upande wa mashariki. Eneo lake ni kilometa za mraba 106,200,000 au sehemu ya tano ya uso wa dunia pamoja na bahari za pembeni kama bahari ya Baltiki na Mediteranea. Hivyo ni bahari kubwa ya pili duniani baada ya Pasifiki. Bila bahari hizi za pembeni eneo lake ni kilometa za mraba 82,400,000.

Bahari ya Atlantiki na bahari zake za kando

Beseni yake ina umbo kama "S". Kina ya wastani ni mita 3,332; kina kikubwa katika mfereji wa Puerto Rico kinafikia mita 8,605. Upana wa bahari ni kati ya km 2,648 kati ya Brazil na Liberia hadi km 4,830 kati ya Marekani na Afrika ya Kaskazini.

Kuna ghuba nyingi pamoja na bahari za pembeni. Atlantiki inabadilishana maji yake na Pasifiki na Bahari Hindi hasa kusini ya mabara ya Afrika na Amerika ya Kusini.

Jiografia ya Atlantiki

Atlantiki inafunika sehemu za mabamba ya gandunia ya Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Karibi, Afrika na Ulaya-Asia. Yanapokutana katika ya beseni uko mgongo kati wa Atlantiki ambao ni safu ya milima chini ya bahari. Mahali pachache inafikia hadi uwiano wa bahari na kuonekana kama visiwa.

Visiwa na funguvisiwa za Atlantiki

Visiwa vikubwa ni (vyenye alama ya * ni sehemu ya safu ya mgongo kati wa Atlantiki):

Greenland, *Iceland, Britania (Uingereza), Ueire (Ireland), Kuba, Newfoundland

Funguvisiwa muhimu ni: visiwa vya Faroe, visiwa vya *Azori, visiwa vya Madeira, visiwa vya Kanari, visiwa vya Cabo Verde, visiwa vya Karibi (pamoja na Kuba), visiwa vya Britania (pamoja na Uingereza na Ueire - Ireland, visiwa vya *Bermudas na vingine.


Mikondo ya bahari

Mikondo ya Atlantiki inatawala hali ya hewa katika nchi zinazoongozana bahari. Kati ya mikondo hizi ni mkondo wa ghuba la Mexiko kutoka eneo la visiwa vya Karibi ukivuka Atlantiki na kubeba maji ya moto (ambayo bado ni vuguvugu kiasi wakati wa baridi) hadi pwani la Ulaya. Mkondo huu umesababisha ya kwamba sehemu kubwa ya Ulaya ina hali ya hewa ya wastani bila joto au baridi kali mno na mvua nyingi hivyo kuhakikisha rutuba ya bara. Bandari za Ulaya hubaki bila barafu hadi kaskazini kabisa.

Vilevile mkondo baridi wa Benguela kutoka Antaktika hubeba maji baridi kwa pwani za Afrika ya Kusini-Magharibi na kusababisha kutokea kwa jangwa la Namib.

Kwa ujumla mikondo katika Atlantiki ya kaskazini hufuata mwendo wa saa, mikondo ya Atlantiki ya kusini huzunguka kinyume cha mwendo wa saa.

 
Jiografia ya Atlantiki, ramani inaonyesha kimo na kina chini ya maji

Bahari za pembeni

Mahali Jina Eneo
kati ya Skandinavia na Greenland Bahari ya Kaskazini ya Ulaya 1.380.000 km²
kati ya Ujerumani, Denmark, Norway na Uingereza Bahari ya Kaskazini 575.000 km²
kati ya Skandinavia na Ulaya bara Bahari ya Baltiki 413.000 km²
kati ya Ulaya na Afrika Mediteranea 2.596.000 km²
kati ya Uturuki na Urusi Bahari Nyeusi 424.000 km²
kati ya Marekani, Amerika ya Kusini, Amerika ya Kati na Visiwa vya Karibi (Kuba, Haiti) Bahari ya Karibi na Ghuba ya Mexiko 4.354.000 km²
ndani ya Kanada Ghuba ya Hudson 1.230.000 km²
kati ya Labrador (Kanada) na Greenland Bahari ya Labrador, Hori la Baffin km²
  NODES