Biashara ya watumwa

(Elekezwa kutoka Biashara ya utumwa)

Biashara ya watumwa ni biashara inayohusu watumwa yaani watu wasio huru wakitazamwa kuwa mali ya binadamu wengine.

Soko la watumwa katika Roma ya Kale (picha ya karne ya 19).
Kusafirisha watumwa katika Afrika ya karne ya 19 (kutoka kitabu cha Livingstone.
Soko la watumwa kwenye bandari ya Rio de Janeiro, Brazil mnamo mwaka 1830
Watumwa kwenye soko la Zanzibar, karne XIX.

Historia

Katika historia ilitokea mara nyingi.

Uchumi wa Roma ya Kale ulitegemea watumwa waliokamatwa na kusafirishwa kutoka pande zote za mazingira ya Bahari Mediteranea.

Milki za makhalifa wa Uislamu ziliendelea kutegemea watumwa. Waosmani walichukua watoto wa Kikristo, hasa kutoka nchi za Balkani, na kuwapeleka kama watumwa katika sehemu za kusini za milki yao kama Misri walipofanya kazi kama wanajeshi.

Biashara ya Waarabu kuhusu watumwa ilidumu miaka 1,300, na kupeleka mamilioni ya Waafrika, hasa wanawake, upande wa Asia.

Mahitaji ya uchumi wa kimataifa tangu karne ya 15 yalisababisha kuongezeka kwa biashara ya watumwa hasa kutoka Afrika; mamilioni walikamatwa na watawala wa milki kwenye pwani za Afrika au Waarabu na kuuzwa kwa wafanyabiashara Wazungu waliowapeleka Amerika walipohitajika kwa kazi kwenye mashamba makubwa ya miwa na pamba.

Wareno na Wahispania waliunda utawala wao kule Amerika Kusini hasa katika karne ya 16. Walitafuta madini ya nchi hizo wakaanzisha mashamba makubwa. Lakini wakaona ugumu wa kutumia Wahindi wekundu kama wafanyakazi.

Watu hao waliishi miaka elfu kadhaa bila mawasiliano na watu wengine. Magonjwa yaliyokuwa kawaida Ulaya, Afrika na Asia (kwa sababu watu wa kule waliwahi kuambukizana tangu karne nyingi) yaliua wenyeji wengi wakiishi pamoja na Wazungu. Tena walowezi Wazungu walikuwa wakatili mno. Wahindi wekundu waliofanywa watumwa wakafa kwa mamilioni.

Hapo wazo jipya lilijitokeza: kuchukua watumwa kutoka Afrika ili wafanye kazi Amerika! Waliopendekeza wazo hili walisema Waafrika wana nguvu na afya kuliko wenyeji wa Amerika. Ndivyo ilivyotokea. Msingi wa maendeleo ya Ulaya uliwekwa kwa malighafi za Amerika zilizochimbwa na kulimwa na watumwa Waafrika.

Kwa karne tatu biashara ya watumwa ilikua na kuongezeka kwenye pwani za Afrika. Katika karne ya 16 Wareno walikuwa mstari wa mbele katika biashara hii ya aibu, halafu Waingereza wakashika nafasi ya kwanza kabisa wakauza watumwa popote.

Makanisa makubwa yalinyamaza au kufumba macho mbele ya maovu hayo. Wakristo wa madhehebu madogo ya Kiprotestanti katika Uingereza (kama "Makweka" au "Marafiki" na Wamethodisti, baadaye pia sehemu ya wafuasi wa makanisa makubwa) ndio walioanza kupinga utumwa hasa tangu mwisho wa karne ya 18. Walifaulu kupata hukumu ya mahakama iliyosema si halali kuwa na watumwa nchini Uingereza. Lakini bado utumwa uliendelea katika makoloni.

Wakristo walimtumia Mbunge Wilberforce pamoja na wahubiri kanisani kukaza kampeni kote nchini. Mwaka 1807 walifaulu kupata sheria bungeni iliyopiga marufuku biashara ya watumwa kwa Waingereza na katika makoloni ya Uingereza (lakini watumwa waliokuwepo walibaki hivihivi).

Waliendelea kudai matumizi ya meli za kijeshi za Uingereza dhidi ya biashara ya mataifa mengine kama vile Wafaransa, Wareno na Waarabu. Baada ya mapambano marefu walipata sheria iliyoweka huru watumwa wote katika makoloni yote ya Uingereza. Lakini bado nchi nyingine ziliendelea na utumwa wa ndani.

Mkutano wa Vienna (1814-1815) ulikuwa mapatano ya kwanza ya kimataifa yaliyolenga kukataza biashara ya watumwa kutoka Afrika.

Mskoti David Livingstone (1813-1873) ndiye aliyetumia nguvu zake zote kupeleleza habari za biashara ya utumwa na kuzipeleka Uingereza. Alikuwa mmisionari na daktari aliyezunguka nchi zote za Kusini mwa Afrika hadi Ujiji (leo katika Mkoa wa Kigoma) kwenye ziwa Tanganyika. Akafa mwaka 1873, moyo wake ukazikwa Chitambo (Zambia). Alifaulu kuamsha watu wengi dhidi ya biashara ya watumwa.

Hata hivyo biashara hiyo haramu iliendelea kwa miaka kadhaa hasa upande wa bahari Hindi ambako wanafayabiashara Waislamu kama Tippu Tip waliendelea kukamata watumwa na kuwapeleka pwani na Zanzibar kulikokuwa na soko la watumwa kubwa kuliko yote.

Afrika Mashariki biashara ya watumwa iliendelea hata baada ya Waingereza kumlazimisha Sultani wa Zanzibar kufunga soko la watumwa mjini mwaka 1874.

Biashara ilikomeshwa tu baada ya kuundwa kwa utawala wa kikoloni. Lakini watu walishikwa kama watumwa mpaka mwanzo wa karne ya 20, serikali za kikoloni zilipofanya taratibu za kuwaweka huru.

Kule Marekani suala hilo lilisababisha farakano la majimbo ya kusini na vita vya wenyewe kwa wenyewe (1861-1865). Majimbo ya kaskazini yalishinda na kuwaweka huru watumwa. Kule Brazil utumwa uliendelea karibu mpaka mwisho wa karne ya 19.

Katika kampeni hizo Wakristo ndio waliosukuma serikali zao na kuonyesha aibu kubwa juu ya mataifa ya Kikristo ya Ulaya kushiriki biashara ya watumwa katika karne zilizopita, karibu sawa na walivyofanya Waarabu Waislamu.

Ukoloni ulimaliza kwa kiasi kikubwa biashara hiyo Afrika pia, ingawa Mauritania ilifanya utumwa kuwa kosa la jinai mwaka 2007 tu.

Tangu karne ya 20 utumwa na pia biashara ya watumwa zimepigwa marufuku katika mapatano ya kimataifa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Lakini miaka ya hivi karibuni imeona biashara mpya inayotumia nafasi za usairi wa kisasa; hata kama duniani hakuna utumwa kisheria tena, ni hasa wanawake na mabinti wanaouzwa kwa kazi haramu ya ukahaba kati ya nchi na nchi (53%).

Watumwa wamekadiriwa na ofisi za UM kuwa milioni 21 na kuzalisha $ 32,000,000,000 kwa mwaka.

Tazama pia

Marejeo

  NODES
eth 1