Chungwa ni tunda la mchungwa. Jina la kisayansi ni Citrus aurantium L. var. sinensis L. au Citrus sinensis (L.) Osbeck kwenye familia ya Rutaceae. Tunda lifahamikalo kisayansi kama Citrus sinensis huitwa chungwa tamu ili kulitofautisha na Citrus aurantium, chungwa chungu. Chungwa ni mahulusi kati ya mbalungi-kubwa (Citrus maxima) na mchenza (Citrus reticulata).

Machungwa na maua yake
Chungwa bivu

Mti wake mdogo utoao maua hufikia urefu wa takribani mita kumi na unaota majani yake yasiyokauka muda wote.

Tunda lenyewe ni la rangi ya kijani likiwa bichi na likiwa limeiva rangi yake huitwa kama jina lake: rangi ya machungwa (hii ni sawa katika lugha za Ulaya na lugha nyingine, kama "orange" kwa Kiingereza). Pamoja na limau, danzi, balungi na ndimu ni mojawapo kati ya matunda chungwa, jamii ya matunda ya citrus. Matunda yote jamii ya jenasi ya citrus, huzaliana. Matunda ya jamii hiyo huonwa kama ya aina ya beri sababu ya kuwa na mbegu nyingi, kuwa laini na nyama nyingi huku yakikua kutoka kwenye ovari moja.

Siku hizi chungwa ndilo tunda linalovunwa zaidi kati ya matunda chungwa na ni kati ya matunda yanayovunwa sana duniani.

Uenezi

hariri

Asili yake ni katika Asia ya Kusini-Mashariki ambako lilioteshwa na wakulima.

Kuna aina mbili zinazotofautiana kwa ladha ama chungu au tamu.

Aina yenye ladha chungu iliwahi kusambaa duniani, hivyo jina la Kiswahili limetunza ladha hii hata kama matunda mengi yanayopandwa siku hizi ni aina tamu.

Chungwa tamu lilisambaa kote duniani baada ya Wareno kuchukua machipuko yake na kuyapanda kwanza Ureno baadaye hata Amerika na Afrika kuanzia karne ya 15.

Kiwango cha asidi

hariri

Kama ilivyo kwa jamii ya matunda ya Citrus, machungwa nayo huwa na hali ya asidi, yenye kiwango cha pH karibu na 2.5 -3, kulingana na umri, ukubwa na aina ya chungwa. Japo si kama ilivyo kwa limao, bado machungwa huwa na kiwango cha asidi cha kutosha, sawa kabisa na hata siki ya nyumbani.

Uzalishaji

hariri

Machungwa kwa kawaida hulimwa kwa ajili ya biashara na hulimwa maeneo mengi duniani. Wazalishaji wa machungwa wanaoongoza duniani ni Brazil, Marekani na Meksiko. Nchini Tanzania hulimwa katika mikoa mbalimbali ya ukanda wa joto, kwa mfano mkoa wa Tanga, wa Morogoro na wa Shinyanga.

Machungwa huathirika haraka sana na ukungu hivyo huhitaji matunzo mazuri pindi joto dogo sana linapotegemewa.

Nchi za mavuno — 2005
(tani milioni)
Brazil 17.8
Marekani 8.4
Mexiko 4.1
Uhindi 3.1
China 2.4
Hispania 2.3
Italia 2.2
Uajemi 1.9
Misri 1.8
Pakistan 1.6
Dunia yote 61.7
Chanzo:
FAO
[1]

Ulimaji

hariri

Michungwa huweza kukuzwa maeneo yenye joto na hata yale yenye baridi. Kama ilivyo kwa matunda mengine ya citrus, ili kupata mazao mazuri hakuna budi kukuza michungwa katika joto la 15.5 °C - 29 °C. Miti ya machungwa iliyooteshwa kutokana na mbegu zilizonunuliwa madukani inaweza kuwa tofauti kabisa na ile miti ya asili iliyozalisha mbegu hizo. Hii hutokana na mabadiliko ya kizazi yanayosababishwa na kuchanganywa mbegu kisayansi kwa muda mrefu. Ili kupata mmea wa mchungwa kama tunda ulilolinunua, huna budi kuitunza mbegu hiyo kwenye unyevunyevu, kisha tu baada ya kuzitua kwenye tunda na kuziotesha katika hali ya unyevu; na pindi mmea uchipuapo hapo ukapandwe kwenye udongo uliokusudiwa.

Sharubati na bidhaa nyingine

hariri

Machungwa yanakuzwa katika hali mbalimbali za joto duniani kote, na ladha yake hubadilika kuanzia hali ya utamu mpaka uchungu kabisa. Tunda kwa kawaida humenywa na kuliwa au huminywa na sharubati yake kunywewa. Limezungukwa na ganda lenye ladha chungu lakini huweza kukamuliwa na kuondolewa maji yake na kutumika kwa chakula cha mifugo. Pia hutumika kuongeza ladha ya vyakula vingine na hata maganda yake hufaa kwa kazi hiyo. Sehemu nyeupe ya ndani, kati ya nyama na ganda la nje, nayo huwa na vitamini sawa kabisa na nyama ya ndani.

Sharubati ya machungwa ndiyo bidhaa kuu kuliko zote za machungwa. Huweza kuzalishwa kwa matumizi ya nyumbani lakini hasa hufanywa kwa minajili ya biashara. Sharubati ya kugandishwa ya machungwa hutengenezwa kutokana na majimaji ya machungwa pia. Mafuta ya machungwa ni bidhaa ndogo inayotengenezwa kwa kukamua maganda ya machungwa. Hutumika kwa kuongeza ladha ya chakula na zaidi kwenye utengenezaji wa manukato.

Maua ya machungwa nayo hupendwa kwa harufu yake nzuri na hutumika mara nyingi nyakati za harusi na huhusishwa na bahati njema.

Majani ya michungwa yanaweza kutumika kutengenezea aina ya chai.

Marejeo

hariri
  1. "FAO Statistics". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2006-06-19. Iliwekwa mnamo 2008-10-07. {{cite web}}: Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help)

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Chungwa kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  NODES