Dhambi (kutoka Kiar. ذنب dhanaba kukosa, kutenda dhambi au jinai[1]) ni kosa la kiumbehai mwenye hiari dhidi ya uadilifu unaompasa.

Inaweza kufanyika kwa mawazo, maneno, matendo na kwa kutotimiza wajibu.

Maadili yanamuelekeza binadamu katika kutambua dhambi ni zipi pamoja na madhara yake.

Kwa kawaida dini zinahusianisha kosa hilo na Mungu aliye asili ya uadilifu, kwa kuwa ndiye aliyeumba viumbe vyote na kuvielekeza maishani.

Akiwapa baadhi ya viumbehai akili na utashi, papo hapo Mungu amewapa wajibu wa kufuata maelekezo yaliyomo katika utaratibu wa nafsi yao na wa ulimwengu wote.

Katika dini zinazofundisha kwamba Mwenyezi Mungu alitoa ufunuo wake hata kwa njia ipitayo maumbile, ni dhambi kwenda kinyume cha ufunuo huo, kwa mfano unavyopatikana katika vitabu vitakatifu vya dini husika, kama vile Biblia kwa Wayahudi na Wakristo na Kurani kwa Waislamu.

Kutokana na uenezi wa dhambi kuanzia dhambi ya asili, linajitokeza suala la wokovu, ambalo linaweza kutazamwa zaidi kama neema, lakini kwa kawaida linadai toba ya mkosefu.

Kanisa Katoliki na hata baadhi ya madhehebu mengine ya Ukristo linaamini linaweza kuondolea dhambi yoyote katika ubatizo na kitubio kwa kutumia mamlaka ambayo Yesu mfufuka aliwashirikisha Mitume wake alipowavuvia akisema: “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23). “Mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu” (1Kor 6:11).

Aina za dhambi

hariri

Dhambi za ujinga, udhaifu na uovu

hariri

Kwa ufupi, kadiri ya Kanisa Katoliki, dhambi ya ujinga ni ile inayotokana na ujinga wa kujitakia na wenye kosa. Dhambi ya udhaifu ni ile inayotokana na maono yenye nguvu ambayo yanapunguza hiari na kuvuta utashi uyakubali. Dhambi ya uovu ni ile inayotendwa kwa makusudi mazima, na mara nyingi bila maono wala ujinga. Hata hivyo si dhambi ya uovu tu inaweza kuwa ya mauti: dhana hiyo inatokana na upotovu wa dhamiri na kuchangia kuuzidisha.

Dhambi za ujinga

hariri

Ujinga usioshindikana si dhambi; ila ujinga wa hiari kuhusu mambo ambayo tunaweza au tunapaswa kuyajua ni dhambi kadiri ya ukubwa wa wajibu tusioutimiza. Kwa kuwa tulifanya uzembe, ujinga huo hauwezi kututetea, ila unapunguza kosa letu; kumbe unatutetea tusipoweza kuachana nao kwa kuwajibika. Haukubaliki kuhusu mambo makuu ya sheria ya kimaumbile, k.mf. “ni lazima kutenda mema na kukwepa maovu”; “usimtende mwenzako usiyopenda kutendwa naye”; “usiue”; “usiibe”; “umuabudu Mungu mmoja tu”. Hii ni kwa sababu walau katika utaratibu wa ulimwengu mtu anahisi kwa urahisi uwepo wa Mungu, mratibu wake; na kisha kuhisi hivyo anatakiwa kujitahidi ajue zaidi na kuomba mwanga wa juu. Ni vilevile kwa mtu aliyehisi kuwa Kanisa Katoliki ndilo la kweli: asipojitahidi kusoma na kuomba mwanga wa Mungu anatenda dhambi dhidi ya imani, kwa kuwa hataki kushika njia za lazima kuifikia.

Mara nyingi wenye moyo wa ibada hawafanyi bidii za kutosha ili kukwepa dhambi za ujinga, wakizitenda kwa kutozingatia – kadiri wanavyoweza na wanavyopaswa – majukumu yao au haki na sifa za watu wanaohusiana nao. Tunapaswa kuchukua jukumu la mema yote tusiyoyatenda ingawa yanatupasa, na ambayo tungeyatenda kama tungekuwa na juhudi kwa utukufu wa Mungu na kwa wokovu wa watu.

Dhambi za udhaifu

hariri

Roho ni dhaifu inaposhindwa na nguvu za maono yanayofanya akili iyaone kuwa yanafaa, na utashi uyakubali kinyume cha sheria ya Mungu. Tutofautishe maono yanayotangulia kibali cha utashi, na maono yanayokifuata. Yanayotangulia yanapunguza kosa kwa kupunguza hiari katika kupima na kuchagua la kutenda, hasa kwa watu wepesi kuguswa. Kinyume chake maono yanayofuata ni dalili ya kuwa dhambi ni ya hiari, kwa kuwa utashi wenyewe unachochea maono, k.mf. mtu akitaka kukasirika ili kuonyesha hana nia njema na mwingine.

Dhambi ya udhaifu ni ile ambayo utashi unashindwa na nguvu ya maono yaliyotangulia, na kwa hiyo uzito wake umepungua; lakini si kwamba haiwezi kamwe kuwa ya mauti. Hakika ni ya mauti ikihusu jambo kubwa, pamoja na mtu kujua na kutaka, k.mf. akiua kwa hasira. Hasa mwanzoni anaweza kujizuia na kujiombea msaada wa Mungu: asipofanya hivyo, maono yanakuwa ya hiari. Dhambi ya udhaifu, hata ikiwa ya mauti, inaweza kusamehewa kwa urahisi kuliko nyingine.

Wenye moyo wa ibada nao wanatakiwa kujihadhari wasije wakapatwa na makosa makubwa kutokana na kijicho kisichozuiliwa, k.mf. kuhukumu bila msingi kwamba wengine wana dhambi kubwa, au kusema na kutenda kwa namna inayosababisha mafarakano makubwa, kinyume cha haki na upendo.

Dhambi za uovu

hariri

Anayetenda dhambi kwa uovu, akijua na kutaka, ni kwamba anakusudia jambo lililo baya kwa roho (k.mf. kupotewa na urafiki wa Mungu) ili kupata jema la kidunia. Si kwamba kila dhambi ya uovu ni ya kumkufuru Roho Mtakatifu: hiyo ni kati ya dhambi za uovu zilizo kubwa zaidi, na inafanyika mtu anapodharau yale yanayoweza kumuokoa au anaposikitikia kwa makusudi neema na maendeleo ya Kiroho ya jirani kutokana na kijicho.

Ni wazi kuwa dhambi ya uovu ni kubwa kuliko zile za ujinga na za udhaifu: ndiyo sababu sheria za binadamu zinaadhibu vikali mauaji yaliyopangwa kuliko yale yanayotokana na maono. Uzito mkubwa wa dhambi za uovu unatokana na kwamba utashi unahusika nazo kuliko unavyohusika na dhambi nyingine, bila kutetewa kiasi na ujinga wala maono yenye nguvu; mara nyingi zinasababishwa na kilema kinachotokana na marudio ya makosa.

Katika suala hilo tunaweza kudanganyika kwa namna mbili tofauti. Baadhi wanadhani dhambi ya uovu tu inaweza kuwa ya mauti, wasione uzito wa dhambi kadhaa za ujinga wa kujitakia, na za udhaifu zenye jambo kubwa, ujuzi wa kutosha na nia kamili. Kumbe wengine hawaoni uzito wa dhambi kadhaa za uovu zilizotendwa bila ono lolote, kama kwa utulivu wa nafsi: wale ambao kwa namna hiyo wanapinga dini ya kweli na kuzuia watu wanyofu wasijue ukweli wa Mungu, wanaweza kutenda dhambi kubwa kuliko ya mtu ambaye anamkufuru Mungu au kuua kwa hasira. Tunapaswa kuzingatia hasa akili na utashi, vilivyo sehemu zetu za juu. Kosa ni zito kadiri lilivyo la hiari, linavyotendwa kwa kujua na linavyotokana na kujipendea ambako pengine hatima yake ni kumdharau Mungu. Kinyume chake, tendo adilifu linastahili kadiri lilivyo la hiari na linavyotokana na upendo mkubwa kwa Mungu na kwa jirani. Kwa msingi huo, mtu anayesali kwa kushikamana na faraja za kihisi anastahili kidogo kuliko yule anayedumu kusali pasipo faraja yoyote, katika ukavu wa mfululizo; lakini huyo akitoka hali hiyo, stahili zake hazipungui ikiwa sala yake inatokana na upendo uleule ambao sasa una mwangwi katika hisi zake. Basi, ikiwa tendo baya la makusudi mazima (k.mf. agano na shetani) lina matokeo ya kutisha, tendo jema ambalo linatendwa kwa makusudi mazima na kurudiwa mara nyingi (k.mf. kujitoa kwa Mungu) lina matokeo mema makubwa, kwa sababu Roho Mtakatifu anaweza kututakasa kuliko shetani anavyoweza kutupoteza. Tena yumo ndani mwetu kuliko tulivyo sisi wenyewe, naye anaweza kutuelekeza kwa nguvu na upole tutende yaliyo ya hiari na stahili, ya ndani na ya juu zaidi.

Tanbihi

hariri
  1. Linganisha kamusi ya Krapf (1882), "thambi".

Marejeo

hariri

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
 
Simple English Wiktionary
Wikamusi ya Kiswahili ina maelezo na tafsiri ya maana ya neno:
 
Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
  NODES
Idea 1
idea 1