Gazeti (kupitia Kiingereza kutoka Kiitalia gazzetta) ni karatasi zilizochapishwa habari na kutolewa mara kwa mara ama kila siku au kila wiki; kuna pia magazeti yanayotolewa mara moja au mbili kwa mwezi tu.

Magazeti dukani

Aina za habari

Mara nyingi gazeti huwa na habari za siasa, uchumi, utamaduni, michezo pamoja na hali ya hewa na programu za TV na burudani mbalimbali kama vibonzo, hadithi an vitendawili.

Sehemu nyingine muhimu ni matangazo ya biashara ambako kampuni au watu hununua nafasi gazetini na kutangaza biashara, mikutano na mengineyo.

Uhuru wa habari

Pamoja na vyombo vingine vya habari kama TV, redio au blogu, magazeti yanastahili uhuru wa maoni. Lakini katika nchi nyingi serikali zinajaribu kuzuia habari zisizopendezwa nazo. Kwa sababu hii Tangazo kilimwengu la haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa linatetea uhuru wa magazeti.

Pia kwa nchi ya Tanzania na nyinginezo vyombo vya habari vinahitaji uhuru wa kusikilizwa kwa kuunda misingi iliyo kamili katika kutetea haki zao ndipo wataweza kusikilizwa zaidi.

Chombo cha habari ni muhimu sana kwa jamii zetu za Kiafrika kwa vyombo hivi pia ndipo elimu mbalimbali hutolewa kwao. Hata hivyo magazeti yamekuwa pia chanzo kikubwa sana cha vijana kuchafuana majina na kuzushiana taarifa zisizokuwa rasmi kwa jamii, hasa pale ambapo wanakoseana heshima na kudharauliana. Jambo hili ni baya sana kwa taifa na kwa jamii kwa ujumla, kwani kukosekana kwa maadili yaliyo muhimu kwa jamii ni chanzo kikubwa cha kuonekana kuwa magazeti hayana faida kwa kizazi cha baadaye, japo magazeti ni kitu muhimu sana kwa dunia ya leo, iwe ya mtandaoni au ya kuchapishwa kwenye karatasi.

Magazeti ya kuuzwa na magazeti ya bure

Magazeti huuzwa madukani au na wauzaji barabarani. Katika nchi nyingi kuna pia mashine zinazotoa gazeti baada ya kuingiza sarafu. Mengine huagizwa na wasomaji na kupelekwa kwao nyumbani, kwa mfano kwa njia ya posta.

Kuna pia magazeti yanayotolewa bure; gharama zao zinalipiwa na matangazo pekee.

Katika mazingira ya kisasa magazeti yanapatikana pia kwa njia ya mtandao yakionekana kwenye tarakilishi. Njia hii mara nyingi ni bure vilevile, ila kuna baadhi za magazeti yanayoweka sehemu ya makala tu mtandaoni kwa watu wote, lakini makala mengine yanaonekana kwa wasomaji waliowahi kulipa ada na kuwa na neno la siri linalowaruhusu kutazama kurasa zote.

Magazeti yenye nakala nyingi

Magazeti ya Japani huwa na wasomaji wengi kuna tatu za kila siku zinazotolewa kwa nakala kati ya milioni 5 hadi 14 kila siku. Gazeti kubwa la Ujerumani "Bild" hutoa nakala milioni 3.8 kwa siku, gazeti kubwa la Marekani "America Today" milioni mbili. Gazeti kubwa la Afrika ya Mashariki ni Daily Nation wa Kenya yenye nakala 200,000 kila siku. Upande wa Tanzania ni gazeti "Mwananchi"[1] .

Magazeti ya kitaifa, kimataifa au kimahali

Nchi nyingi huwa na magazeti kadhaa yanayouzwa kote taifani. Kuna machache yanayoandaliwa kwa solo la kimataifa hasa, kwa mfano International Herald Tribune.

Lakini kuna pia magazeti mengi yanayokusanya habari za eneo au mji fulani hasa. Mifano yake katika Afrika ya Mashariki ni Arusha Times au Coastweek ya Mombasa. Katika nchi kama Marekani au Ujerumani sehemu kubwa ya magazeti ni ya eneo au miji fulani hasa.

Matumizi baada ya kusomwa

Magazeti huwa tena na matumizi baada ya kusomwa hasa kwa kufunga vitu sokoni au kurudishwa kiwandani kwa kutengeneza karatasi mpya.

Tanbihi

  1. "Tanzania: Media and Publishing". Encyclopædia Britannica. Iliwekwa mnamo 12 Juni 2017.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)

Viungo vya nje

  • www.nationmedia.co.ke Nation Media Group, Nairobi Kenya


  NODES
INTERN 1