Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani (JKK) ilikuwa jina la dola katika mashariki ya Ujerumani kati ya 1949 - 1990. Iliundwa 7 Oktoba 1949 katika eneo la ukanda wa utawala wa Kirusi kama nchi mshindi wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani
Ramani ya Ujerumani; sehemu ya kijani ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani
Ujerumani, kanda za utawala wa washindi wa Vita Kuu ya Pili mw. 1946

Dola hili lilijulikana pia kama "Ujerumani wa Mashariki". Sehemu ya wakazi wake hawakupendezwa na jina hili kwa sababu katika historia na utamaduni wa nchi maeneo makubwa yalihesabiwa zaidi kuwa "Ujerumani wa Kati" au "Ujerumani wa Kaskazini".

Mji mkuu ulikuwa Berlin lakini sehemu ya kiutawala iliyokuwa chini ya Urusi pekee.

Dola nyingine ya Kijerumani ilianzishwa katika maeneo ya kanda za utawala ya Marekani, Uingereza na Ufaransa kwa jina la Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani (SJU): Ujerumani ya Magharibi.

Wakazi wengi wa nchi hii hawakupendezwa na utaratibu wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi chini ya muundo wa ukomunisti.

Mwaka 1989 utawala wa chama cha kikomunisti uliporomoka. Serikali iliyochaguliwa katika uchaguzi huru ilianza majadiliano na serikali ya SJU kwa kusudi la kuunganisha pande zote mbili za Ujerumani. Mwishowe mikoa yote ya JKK iliamua kujiunga na SJU tarehe 3 Oktoba 1990.

Gari mashuhuri la Trabi ilikuwa moja kati ya modeli mbili za motokaa zilizotengenezwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani
  NODES