Korintho (kwa Kigiriki: Κόρινθος, Kórinthos) ni mji wa Ugiriki wa Kusini. Uko kwenye shingo ya nchi ya Korintho inayounganisha rasi ya Peloponesi na sehemu kubwa ya Ugiriki bara.

Mahali pa Korintho nchini Ugiriki.

Siku hizi ni mji mdogo tu, wenye wakazi 36,555, lakini ina historia kubwa na ndefu.

Kimataifa Korintho inajulikana kutokana na mfereji wa Korintho unaokata shingo ya nchi kwa urefu wa kilomita sita na kufupisha safari kutoka bahari ya Adria kuingia Mediteranea ya mashariki kwa meli ndogo na za wastani.

Mfereji wa Korintho unavyokata shingo ya nchi.

Kihistoria jina la mji linajulikana zaidi kutoka Biblia ya Kikristo, na hasa barua za Mtume Paulo kwa Wakristo mjini zinazopatikana katika Agano Jipya kama Waraka wa kwanza kwa Wakorinto (1Kor) na Waraka wa pili kwa Wakorinto (2Kor).

Kitovu cha biashara zamani za Ugiriki wa Kale

hariri

Zamani za Ugiriki wa Kale Korintho ilikuwa bandari muhimu. Mji ulitajirika kutokana na biashara iliyopita kwenye shingo ya nchi. Biashara yote kwa majahazi kati ya Italia na Asia Ndogo ilipitia humo; bidhaa zilitolewa Korintho na kubebwa na wapagazi njia ya shingo ya nchi hadi kuendelea kwa jahazi nyingine upande wa mashariki.

Kwa uwezo wake wa kiuchumi na wa kisiasa ulishindana na Athene na Thebe.

Mji wa Kiroma

hariri

Mji uliharibiwa kabisa na Waroma mwaka 146 KK na kuundwa upya na Julius Caesar mwaka 44 KK kama koloni la Kiroma. Ulikua haraka na kuwa na mchanganyiko wa watu kutoka Italia, Ugiriki na Wayahudi.

Wakati Paulo wa Tarso alipofika mwaka 51/52 (taz. Mdo 18:1-18) alikutana na Akwila na mke wake Priska na kuunda pamoja nao ushirika wa Kikristo mjini huko.

Alirudi tena mwaka 58 akikaa miezi mitatu. Waraka kwa Waroma uliandikwa huko mwaka huo wakati akisubiri kuabiri kwenda Yerusalemu ili kuwasilisha michango kwa ajili ya Wakristo fukara.

  Makala hii kuhusu maeneo ya Ugiriki bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Korintho kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  NODES
os 1