Kunguni
Kunguni
Kunguni
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye mwili wa pingili na miguu ya kuunga wasio na ugwe wa mgongo kama wadudu, nge, buibui)
Nusufaila: Hexapoda (Arithropodi wenye miguu sita)
(bila tabaka): Dicondylia (Wadudu walio na mandibula zenye condyle mbili)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Nusungeli: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda ya juu: Paraneoptera
Oda: Hemiptera (Wadudu mabawa-nusu)
Haeckel, 1896
Nusuoda: Heteroptera (Kunguni-mgunda)
Familia ya juu: Cimicoidea (Wadudu kama kunguni)
Familia: Cimicidae (Kunguni)
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Nusufamilia 2, spishi 3:

Kunguni ni wadudu wadogo wa familia Cimicidae katika oda Hemiptera ya nusungeli Pterygota (wenye mabawa).

Mara nyingi huishi katika mazingira ya kificho na yenye mlundikano wa uchafu utokanao na taka mwili, hasa vitanda ambamo hufyonza damu ya watu au wanyama kama chakula chao, hasa usiku.

Spishi

Spishi muhimu sana ni kunguni wa Ulaya (Cimex lectularius). Inatokea duniani kote mahali ambapo watu wanaishi. Katika Afrika kuna spishi nyingine muhimu, kunguni wa Afrika (Cimex hemipterus). Spishi ya tatu, kunguni Magharibi (Leptocimex boueti), inatokea Afrika ya Magharibi na Amerika ya Kusini na hupendelea damu ya popo, lakini hufyonza damu ya watu pia mara nyingi. Spishi nyingine za Afrika hutokea kwa wanyama tu, hususan popo na ndege.

Biolojia

Kunguni hujilisha damu tu, lakini wanaweza kuishi mwaka mzima bila kula.

Wapevu ni wa rangi ya hudhurungi hadi kahawianyekundu, wana umbo la duaradufu bapa na hawana mabawa ya nyuma. Mabawa ya mbele hayafanyi kazi na yamepunguzwa kwa miundo kama pedi.

Wapevu hukua hadi urefu wa mm 4-7 na upana wa mm 1.5-3.

Wadudu hao wana hatua tano za maisha kama tunutu na hatua ya mwisho ya upevu. Huambua ngozi yao mwishoni mwa kila hatua, wakitupa kiunzi chao cha nje. Tunutu wakitoka mayai ni wangavu, wenye rangi isiyoiva na wanakuwa kahawia kadiri wanapoambua ngozi na kufikia upevu.

Kunguni wanaweza kudhaniwa kuwa wadudu wengine, kama vile chawa-vitabu, mende wadogo au mbawakawa-zulia, lakini wakipata joto na kufanya shughuli, mwendo wao ni ule wa sisimizi, na, kama kunguni-mgunda wengi, wakisetwa hutoa harufu bainifu inayononga.

Kwa sababu kunguni ni wafyonya damu shuruti, wana sehemu za kinywa ambazo zinakeketa ngozi na kuingiza mate yenye dutu dhidi ya mgando na viondoa maumivu. Kiwango cha hisia cha wanadamu kinatofautiana kutoka athari mbaya ya mzio hadi kutokuwepo kwa athari yoyote (karibu 20%). Kwa kawaida umo hutoa uvimbe bila doa jekundu, lakini wakati kunguni wengi hujilisha kwenye eneo dogo, madoa mekundu yanaweza kuonekana baada ya uvimbe kupungua. Kunguni hupendelea ngozi wazi, haswa uso, shingo na mikono ya mtu aliyelala.

Kunguni huvutiwa na vidusiwa wao kwa dioksidi ya kaboni hasa, kisha kwa joto, na pia kwa kemikali fulani. Kunguni wa Ulaya hujilisha kila siku tano hadi saba tu, ambayo inadokeza kuwa hatumii muda mrefu sana wa maisha yake kutafuta kidusiwa. Kunguni akiwa na njaa, huondoka makazi yake na kutafuta kidusiwa. Anarudi kwenye makazi yake baada ya kujilisha vizuri au ikiwa anakabiliwa na mwanga. Kunguni wa Ulaya hujumuika kwa hatua zote za maisha na hali za kukomaa. Kunguni wanachagua kujumuika labda kwa sababu ya umbuai, nguvu kinzi dhidi ya ukaushaji na fursa zaidi za kupata mwenzi. Feromoni zinazotumwa na hewa zina jukumu la jumuiya.

Mweneo

Uingiaji wa kunguni mahali papya husababishwa na ukosefu wa usafi mara chache tu. Kwa kawaida uhamisho hadi maeneo mapya huwa katika vitu vya binafsi vya wanadamu ambapo wanajilisha. Makazi yanaweza kuingiliwa na kunguni kwa njia tofauti, kama vile:

  • Wadudu na mayai yaliyoletwa kutoka kwa makazi mengine yaliyokuwa nayo kwenye mwili wa mgeni au mavazi au mizigo yake;
  • Vitu vilivyo na kunguni (kama vile samani, haswa vitanda na kochi, mavazi au shanta) vinavyoletwa katika nyumba au jengo la biashara;
  • Ujirani wa makazi yaliyo na kunguni, ikiwa njia rahisi za kupitia zinapatikana, k.m. mifereji au dari bandia;
  • Wanyama-mwitu (kama vile popo au ndege) walio na kunguni au spishi ndugu kama kunguni-popo.

Ingawa kunguni watajilisha juu ya wanyama vipenzi nafasi ikitukia, hawaishi au kusafiri kwenye ngozi ya vidusiwa wao na wanyama vipenzi hawafikiriwi kuwa sababu ya kuenezwa kwao.

Ishara na dalili

Ngozi

Athari za binafsi za maumo hutofautiana na kwenda kutoka kutokuonekana kwa athari (20-70%) hadi madoa madogo na hata vivimbe pamoja na mwasho mkali unaoweza kudumu siku kadhaa. Maumo yapo katika safu mara nyingi. Doa la kati litoalo damu linaweza kuwapo kwa sababu ya kufeleti kwa dutu dhidi ya mgando katika mate ya mdudu.

Dalili labda hazionekani mpaka siku kadhaa baada ya maumo kutukia. Athari zinakuwa kali zaidi baada ya maumo mengi kwa sababu inawezekana kama protini katika mate ya kunguni huhisisha ngozi. Athari ya ngozi hutukia kwa kawaida katika eneo la umo ambalo mara nyingi sana ni mikono, mabega na miguu kwa sababu imefiduliwa usiku kwa kawaida. Maumo mengi yanaweza kusababisha ugonjwa wa mabaka ngozini.

Elimunafsia

Uwepo wa mashambulio tele na ya kudumu yanaweza kusababisha wasiwasi, dhiki na kukosa usingizi. Inawezekana mtu aanze kufikiri kwamba vidusia wapo ingawa kwa kweli hawapo, kwa sababu anafikiria sana kunguni kila wakati.

Nyingine

Dalili nyingine kadhaa zinaweza kutukia kwa sababu ya maumo ya kunguni au kusikia harufu yao. Anafilaksisi iliyosababiswa na uingizaji wa protini za mate ya kunguni imeripotiwa kwa nadra. Kwa sababu kila umo linachukua kima kidigi cha damu, uwepo wa kudumu wa kunguni wengi unaweza kusababisha anemia.

Ambukizo la ngozi na bakteria linaweza kutukia kwa sababu kujikuna kunaweza kufungua ngozi na hii inaweza kusababisha kusumu damu kote ikiwa kuna maumo mengi sana.

Kusikia harufu ya kunguni kunaweza kuchokonoa shambulio la pumu kwa sababu ya vizio katika hewa, ingawa ithibati ya mwungano huu ni ndogo.

Hakuna ithibati ya kwamba kunguni wanaeneza magonjwa ya kuambukiza, ingawa wanaonekana kuweza kubeba pathojeni na uwezekano umechunguzwa. Umo lenyewe linaweza kuleta uchungu ambao unasababisha usingizi mbaya na utendaji mbaya katika kazi.

Mithili ya wanadamu, wanyama kipenzi pia wanaweza kuumwa na kunguni. Ishara zilizoachwa na maumo ni sawa na kisa ya watu na dalili zinafanana (kuwasha ngozi, kujikuna n.k.).

Utambuzi

Utambuzi dhahiri wa athari za kiafya zinazosababishwa na kunguni unahitaji kutafuta na kuona wadudu katika mazingira ya kulala kwani dalili siyo maalum ya kutosha. Kwa kawaida kunguni hufanya safu ya maumo yanayoitwa kimazungumzo "kiamshakinywa, chakula cha mchana na chakula cha jioni". Pia kwa nadra hujilisha kwenye kwapa au nyuma ya magoti ambayo inaweza kusaidia kuwatofautisha na wadudu wengine wanaouma.

Dalili hizi zinaweza kuchanganywa na hali za afya zifuatazo: upele (unaosababiswa na matitiri ya watu na ya ndege), athari za mzio, maumo ya mbu na buibui, tetekuwanga na maambukizo ya ngozi yanayosababishwa na bakteria.

Ugunduzi

Kunguni wanaweza kuweko peke yao, lakini huwa hukusanyika ikiwa wamelowea. Ingawa ni vidusia madhubuti, hutumia sehemu ndogo tu ya maisha yao wakishikamana kimwili na vidusiwa. Mara kunguni akimaliza kujilisha, huhamia mahali karibu na kidusiwa anayejua, kwa kawaida katika au karibu na vitanda au kochi kwenye vikundi vya wapevu, wachanga na mayai, ambapo bingwa wa wadudu huita maeneo ya bandari au bandari tu ambapo mdudu hurudi baada ya kujilisha akifuata nyayo za kemikali. Maeneo haya yanaweza kutofautiana sana katika muundo, pamoja na mizigo, ndani ya magari, katika samani, katikati mparaganyo kando ya vitanda, hata ndani ya soketi za umeme na katika tarakilishi za karibu. Kunguni zinaweza kukaa pia karibu na wanyama ambao wameweka kiota ndani ya makazi, kama vile popo, ndege au panya. Pia wanaweza kuishi juu ya paka na mbwa kipenzi, ingawa binadamu ndiye kidusiwa anayependelewa na kunguni wa Ulaya.

Ikiwa idadi katika nyumba ni kubwa, harufu tamu na chungu inaweza kusikiwa ambayo inafanana na harufu ya rasiberi zinozooza. Mbwa wagundua kunguni hufunzwa ili kuonyesha mahali kamili pa uwepo wao, ambayo ina kiwango cha ugunduzi kati ya 11% na 83%.

Uzuiaji

Ili kuzuia kuleta kunguni nyumbani, wasafiri wanashauriwa kuchukua tahadhari baada ya kutembelea mahali palipoathiriwa: kwa ujumla hii ni pamoja na kuangalia viatu wakati wa kuondoka mahali hapo, kubadilisha nguo nje ya nyumba kabla ya kuingia na kuweka nguo zilizotumiwa katika kikausha nguo nje ya nyumba. Wakati wa kutembelea nyumba mpya ya kulala, inashauriwa kukagua kitanda kabla ya kuleta masanduku katika eneo la kulala na kuweka sanduku juu ya jukwaa ili kupunguza uwezekano wa kuingia ndani kwa kunguni. Inapaswa kutundika nguo au kuziacha katika sanduku na kamwe kuziacha kwenye sakafu. Mwanzilishi wa kampuni iliyojitolea kuangamiza kunguni alikuta kwamba 5% ya vyumba vya hoteli vilikuwa vimeathiriwa. Alishauri watu wasikae chini kwenye usafiri wa umma, wakague viti vya ofisi, viti vya ndege na magodoro ya hoteli, na waangalie vizuri vitanda vya nyumbani na kuvipigia kivuta vumbi mara moja kwa mwezi.

Udhibiti

Tiba inahitaji kuzuia mtu asiumwe tena na tena na labda kutumia antihistimini na kortikosteroidi kidalili (ama mahali penyewe ama kupitia mfumo wa damu). Lakini hakuna ithibati kwamba dawa zinaleta matokeo mazuri zaidi na kwa kawaida dalili zinaisha bila matibabu katika wiki 1-2.

Kuzuia maumo kunaweza kuwa ngumu, kwa sababu kunahitaji ukomeshaji wa kunguni katika nyumba au ofisi. Hii ni ngumu mno kwa vitendo na kwa kawaida inahitaji mchanganyiko wa njia za viuawadudu na njia bila viuawadudu.

Vile vilivyoonwa kufaa zamani vinajumuisha piretroidi (dawa zifananazo na pareto), dichlorvos na malathion, lakini nguvu ya kukinza dawa imezidi sana sasa na matumizi yao yana athari mbaya kwa afya. Siku hizi hakuna kiuawadudu kinachofaa.

Njia za umakanika, kama vile kutumia kivuta vumbi na kuwekea magodoro joto au kuyafunika kabisa, zinafaa mara nyingi. Muda wa saa moja kwa nyuzijoto ya 45ºC au zaidi ama muda wa saa mbili kwa chini ya -17ºC unaua kunguni. Kikausha nguo cha nyumbani au stima ya kibiashara zinaweza kutumiwa.

Kuwanyima kunguni chakula hakufanyi kazi kwa sababu wataendelea kuishi muda wa siku 100 hadi 300 kulingana na nyuzijoto.

  NODES
Idea 1
idea 1