Laurent Kabila
Laurent-Désiré Kabila (27 Novemba 1939 – 18 Januari 2001) alikuwa rais wa tatu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanzia Mei 1997 hadi kuuawa kwake tarehe 18 Januari 2001. Alifuatwa na mwanawe Joseph Kabila.
Laurent Kabila | |
Amezaliwa | 27 Novemba 1939 Baudouinville |
---|---|
Amekufa | 18 Januari 2001 |
Nchi | kongo |
Cheo | rahisi |
Kabila alifika ikulu kwa kumpindua Mobutu Sese Seko.
Asili ya Kiluba
haririAlizaliwa katika familia ya Waluba huko Baudouinville (sasa Moba) karibu na Albertville (Kalemie) kando ya Ziwa Tanganyika. Alisoma huko Ujerumani ya Mashariki na Paris akarudi Kongo baada ya uhuru wa nchi alipojiunga na umoja wa vijana wa chama cha Patrice Lumumba.
Mwanaharakati wa Lumumba
haririBaada ya kuuawa kwa Lumumba alijiunga na kundi la wafuasi wa marehemu akaingia katika upinzani wa kijeshi dhidi ya serikali ya Joseph Desiree Mobutu. Majaribio hayo yalikandamizwa na jeshi la serikali. Kabila alikuwa kati ya viongozi wachache walioendelea na upinzani.
Kiongozi wa vita ya msituni
haririAlikuwa na usaidizi wa siri wa rais Julius Nyerere wa Tanzania na kwa miezi michache katika 1965 Mkuba Che Guevara alijiunga na kundi la Kabila lakini kufuatana na kumbukumbu za Guevara hawakuelewana wala kufanikiwa.
Kuanzia mwaka 1967 aliungana na kundi dogo la Parti de la Revolution Populaire (PRP) akaongoza jeshi la Forces Armees Populaires (FAP) lililokuwa na makambi Tanzania na Zambia lakini aliweza pia kutawala eneo dogo katika milima ya Fizi ya mkoa wa Kivu hadi 1977 alipokufuzwa na jeshi la serikali ya Mobutu.
Baadaye aliishi Uganda na Tanzania asionekane tena Kongo. Hakushiriki katika uasi wa wananchi dhidi ya serikali ya Mobutu na jitihada ya kuongeza demokrasia nchini.
Kurudi kwa msaada wa Rwanda
haririAlirudi nchini mwaka 1996 wakati wa uvamizi wa Kongo ya Mashariki ya wanamgambo Wahutu kutoka Rwanda. Mabaki ya jeshi la Kihutu kutoka Rwanda walikuwa wamekimbilia Kongo mwaka 1994 baada ya mauaji ya kizazi ya Rwanda na sasa walishambulia Wabanyamulenge waliokuwa Watutsi wa Kongo. Serikali ya Rwanda ilitafuta njia ya kumaliza wanamgambo hao kwa sababu walikuwa tishio kwa utaratibu mpya wa Rwanda. Hapo walikuwa tayari kusaidia kujenga vikosi vya Wakongo wa kupambana na Wahutu katika Kongo.
Kabila aliunda maungano ya "Alliance des Forces Democratiques pour la Liberation du Congo-Zaire (AFDL)" akapokea silaha na washauri kutoka jeshi la Rwanda.
Katika muda mfupi Kabila aliweza kujipatia sifa kama kiongozi mwenye uwezo wa kushindana na jeshi la Mobutu aliyejua namna ya kufanya maazimio yake hata bila washauri wake Wanyarwanda aliowategemea bado.
Mshindi dhidi ya Mobutu
haririVikosi vya Kabila vilisogea mbele haraka dhidi ya jeshi la Mobutu lisilokuwa tayari tena kupigana na adui aliyejua kazi ya vita. Kabila alianza vita katika Oktoba 1996 huko Kivu akateka Bukavu mnamo Oktoba mwaka uleule, Kisangani katika Machi 1997 na Lubumbashi mwezi wa Aprili. Mwezi Mei jeshi lake likaingia Kinshasa na wakubwa wa Mobutu walikimbia Brazzaville. Tarehe 17 Mei Kabila alijitangaza kuwa rais mpya akabadilisha tena jina la nchi kuwa Kongo.
Kabila alikuwa na tatizo la kutokuwa na uhusiano na watu wa Kinshasa ambao wengi walimwona kama mgeni. Askari zake wengi waliwasiliana kwa Kiswahili na Kiingereza au lugha za Kongo mashariki, hawakujua Kifaransa wala lugha za Kongo magharibi. Baada ya kushika serikali Kabila alijaribu kupunguza umuhimu wa washauri wake Wanyarwanda.
Rais wa kuona upinzani
haririHii ilisababisha matatizo na uhusiano ulikuwa mbaya. Wananchi wa Kinshasa wengi hawakuona mabadiliko mengi katika maisha yao. Kabila hakuongeza haki za kidemokrasia wala kushirikiana na wanasiasa waliokuwa wapinzani wa Mobutu katika miaka ya kutafuta demokrasia nchini.
Upinzani dhidi ya Kabila ikakua katika sehemu za nchi. Hatimaye mwaka 2001 aliuawa na askari wa ulinzi wake kwa namna isiyoeleweka vizuri hadi leo. Hapo wakuu wa jeshi walimtangaza mwana wake Joseph kuwa mwandamizi wake.
Viungo vya Nje
hariri- Kumbukumbu ya Kabila katika gazeti la Independent ya London 18-01-2001 Ilihifadhiwa 24 Desemba 2007 kwenye Wayback Machine.