Musa (aliishi miaka 1250 hivi K.K.) alikuwa kiongozi wa Wanaisraeli walipoondoka nchini Misri kukimbilia nchi ya Kanaani (iliyoitwa "Israeli" na "Palestina" baadaye).

Sanamu ya Musa iliyochongwa na Michelangelo iko katika kanisa la Mt. Petro "in vinculis" mjini Roma (Italia).

Mungu ndiye aliyemteua kukomboa watu wake walioonewa awape nchi takatifu; katika mlima Sinai alimtokea na kumuambia: «Mimi ndimi niliye», akampa sheria ambayo iongoze maisha ya taifa teule.

Akiwa mzee sana, huyo mtumishi wa Mungu alifariki juu ya mlima Nebo kwenye nchi ya Moabu mkabala wa nchi ya ahadi[1].

Hasa Torati na vitabu vingine vya Biblia vinasimulia habari zake. Pia Qurani inamtaja katika aya 502 tofauti.

Tangu kale anaheshimiwa na Wayahudi, Wakristo na Waislamu kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa hasa tarehe 4 Septemba[2].

Utoto wa Musa

hariri
 
Musa akiokolewa katika maji ya mto Nile, alivyochorwa na Nicolas Poussin mwaka 1638.

Waisraeli waliishi Misri kama wageni tu zaidi ya miaka mia nne (Mdo 7:6-16) wakiongezeka kiasi cha kuwatisha wenyeji wao ambao walianza kuwafanya watumwa mwaka 1300 hivi K.K. Kwa mujibu wa Biblia, katika kuwakomboa utumwani, Mungu alijionyesha mtetezi wa haki za maskini. Pamoja na kushurutishwa kufanya kazi wasizozipenda, ilitolewa amri ya kuua watoto wao wote wa kiume, ingawa mpango huo haukutekelezwa sawasawa (Kut 1:7-22).

Mmoja kati ya watoto waliookolewa katika mpango wa kuua watoto wa kiume ni Musa wa kabila la Lawi (Kut 2:1-10; Eb 11:23; Mdo 7:17-22). Mama wa Musa alimficha mtoto halafu akamweka ndani ya kikapu mtoni. Hatimaye mtoto akaokotwa na binti Farao na kulelewa kama mtoto wa kifalme, lakini alijua asili yake.

Utu uzima

hariri

Alipomuua afisa wa Kimisri alipaswa kukimbilia jangwani kwa kabila la Wamidiani akaolea huko (Kut 2:11-22; Eb 11:24-27; Mdo 7:23-29): alipokuwa anachunga mifugo ya mkwewe kwenye mlima Sinai akaitwa na Mungu kutoka ndani ya kichaka kinachowaka moto bila kuteketea. Mungu alimchagua kurudi Misri na kuokoa watu wake katika utumwa wa Farao. Mungu akasisitiza aende mwenyewe, naye atatumia uwezo wake wa Kimungu kumlazimisha Farao. Kadiri Musa alivyoomba, Mungu alimfunulia jina lake takatifu YHWH ambalo linaeleweka kiasi tu, kama vile fumbo la Mungu mwenyewe (Kut 2:23-3:20; Mdo 7:30-35).

Mapigo ya Wamisri

hariri

Mungu alipomtuma Musa kwa Farao alijua tayari huyo atakataa kuwaruhusu Waisraeli waende zao, mpaka aone mapigo yake kwa Wamisri. Kwa kuwa ulihitajika muda kuleta ukombozi, iliwabidi Waisraeli wawe na imani na subira hadi ahadi za Mungu zitimie. Waisraeli walianza kunung’unika (Kut 5:1-6:1). Hata hivyo Mungu akaendelea na mpango wake.

Maajabu aliyoyatenda huwa yanatokea Misri lakini si yote kwa wakati mmoja wala si kwa kiasi kile alichosababisha Musa kwa fimbo yake (Kut 6:28-7:7). Tuna orodha mbalimbali za mapigo hayo, lakini kwa kawaida yanahesabiwa kumi: maji ya mto Naili kuwa mekundu kama damu, vyura kujaa nchi, chawa, nzi, tauni, majipu, mvua ya mawe, nzige, giza na hatimaye kifo cha wazaliwa wa kwanza wa kiume wa watu na wa wanyama. Adhabu hizo ziliwapata Wamisri, lakini si Waisraeli: hivyo ilikuwa wazi kuwa Mungu anabagua watu wake na watu waovu.

Katika pigo la kumi Waisraeli waliopolewa kwa kuipaka milango yao damu ya mwanakondoo (Kut 11:1-10; Mdo 7:36-37; Eb 11:28). Hivyo Mungu aliwaandaa watu kupokea imani kwa Yesu Kristo, Mwanakondoo wa kweli na Mkombozi wa waliokuwa watumwa wa dhambi, shetani na kifo (Yoh 19:36; 1Kor 5:7; 1Pet 1:18-20). Hiyo ni wazi katika ibada iliyoagizwa ifanyike kila mwaka (Kut 12:1-14), yaani Waisraeli wale nyama ya mwanakondoo dume asiye na hila, pamoja na mkate usiotiwa chachu na mboga ya majani machungu. Yesu akaifanya ibada hiyo iwe ibada kuu ya agano jipya la milele, akiagiza tuifanye kwa ukumbusho wake, si tena kwa ukumbusho wa kutoka Misri (1Kor 11:23-26).

Safari ya kuendea nchi ya ahadi

hariri

Kut 12:29-42 inasimulia Waisraeli wote walivyokimbia Misri pamoja na mifugo yao waliposikia mayowe kutoka nyumba za majirani wao wote. Katika safari yao wakaongozwa na Mungu kwa sura ya wingu mchana na ya moto usiku (Kut 13:17-22; Yoh 8:12): hivyo Mungu alionyesha wazi kuwa hawaachi hata kidogo bali anawashughulikia kwa namna tofauti kadiri ya mahitaji.

Kut 14:5-31 inasimulia jinsi Wamisri, kisha kuwalilia wafu wao, walivyoanza kuwatafuta Waisraeli kwa farasi na magari wakawakuta karibu na bahari ya Shamu. Lakini Waisraeli walivuka bahari kama kwamba ni nchi kavu, kwa kuwa maji yamegawanyika. Kumbe Wamisri wakazama kwa kuwa maji yamerudi mahali pake (Eb 11:29). Asubuhi Waisraeli wakaona maiti za Wamisri wote zikielea wakamshangilia Mungu aliyewaokoa (Kut 15:1-21 inatuletea wimbo ambao maneno yake ni kati ya yale ya kale zaidi katika Biblia). Hivyo Mungu aliwaokoa tena watu wake katika maji, na huu pia ni mfano wa ubatizo ambao unaadhimishwa hasa usiku wa Pasaka. Hata katika hatari ya kukandamizwa Mungu alidai Waisraeli watulie kwa imani ya kuwa ushindi ni wake tu. Tena walitakiwa wasiyasahau kamwe mang’amuzi hayo, kwa kuwa ndiyo msingi wa imani ya dini yao. Sisi vilevile tunatakiwa kukumbuka daima ubatizo wetu ambapo Mungu ametuokoa. Baada ya ushindi wa Pasaka safari ikaendelea mpaka kufikia nchi aliyoahidi Mungu, ila Waisraeli wakaja kusahau uweza wake na kumlalamikia kipumbavu hata kumchosha. 1Kor 10:1-11 inatuonya tusifanye vile. Kama kawaida malalamiko ya kwanza yalihusu kula na kunywa (Kut 15:22-17:7). Mungu aliwakubalia kwa kuwateremshia kwale halafu mana: hasa chakula hicho kiliwashangaza Waisraeli wakazidi kukikumbuka hata wakamdai Yesu awapatie tena kama kweli ndiye Musa mpya. Yesu akawajibu kuwa mwenyewe ndiye chakula cha uzima kutoka mbinguni kinachotulisha safarini hapa (Yoh 6:22-59). Vilevile kuhusu maji, Mungu aliyatokeza katika mwamba huko Masa au Meriba, lakini alichukizwa sana na matendo yao (Eb 3:15-19).

Shida nyingine ya kawaida kwa makabila ya wahamaji ni kupigana vita. Waisraeli walilazimika kufanya hivyo na Waamaleki, wakapata ushindi si kwa nguvu zao, ila kutokana na sala ya Musa, mwombezi wao (Kut 17:8-16). Sisi taifa la Mungu tunatakiwa tutegemee sala kuliko uhodari wetu, na daima tuwe na watu wenye kumuinulia Mungu mikono yao kama Musa jangwani.

Agano la mlima Sinai

hariri
 
Mchoro wa William Blake (1780 hivi) unaomuonyesha "Musa akipokea Sheria", Yale Center for British Art.

Walipofikia mlima huo wa kutisha, Mungu alimuita Musa aupande ili aseme naye, huku wengine wakibaki chini. Hapo akampa Musa masharti ya agano lake na Waisraeli (Kut 19). Akiwa Muumba na hasa Mkombozi wao alidai waishi kitakatifu kwa kushika amri kumi, ambazo tatu zinahusu heshima kwake na saba uhusiano na watu wengine (Kut 20:2-17). Ndiyo mawe mawili ambayo Musa alipewa halafu Yesu akayakamilisha katika amri kuu ya upendo kwa Mungu na kwa jirani (Mk 12:28-34). Amri hizo zinaweza kujulikana na kukubaliwa na mtu yeyote mwenye mapenzi mema, lakini Mungu alipenda kutusaidia tujue kwa urahisi na hakika zaidi tufanye nini ili kumpendeza, tuwe watu wake naye awe Mungu wetu kwelikweli. Agano hilo upande wa Mungu ni imara kwa kuwa yeye ni mwaminifu kabisa, shida iko upande wetu tulio geugeu, tukiahidi tusitekeleze. Ndiyo sababu likahitajika agano lingine lililofungishwa na Yesu Kristo (2Tim 2:11-13).

Ndama ya dhahabu

hariri

Kut 32 inasimulia uasi wa Waisraeli ulivyofikia kilele chake walipojitengenezea mungu wa dhahabu mwenye sura ya fahali (Biblia kwa dharau inasema “ndama” na “mla nyasi”). Hata Haruni alikubali kufuata matakwa yao huku mdogo wake akichelewa mlimani (Mdo 7:38-42). Israeli kuabudu ndama ilikuwa chukizo mbele za Mungu, kwa kuwa Mungu hana mbadala wa yeye kufanyiwa ibada. Musa akambembeleza Mungu asiwaangamize watu wake, hivyo akawa mfano bora wa mwombezi, kwa kuwa hakujali ahadi ya Mungu ya kumfanya chanzo cha taifa lingine kubwa. Kazi hiyo ni hasa ya Bwana Yesu ambaye aliwatetea watu wake kwa kumwaga damu yake, na anazidi kuwaombea kwa Baba yake (Eb 7:25-27).

Mungu kujifunua tena kwa Musa

hariri

Kut 33:18-34:9 inasimulia jinsi Mungu alivyokubali kiasi ombi la Musa la kumuonyesha utukufu wake; badala ya kumuonyesha uso wake (Yoh 1:18) alijifunua kwake kwa kulitangaza na kulifafanua jina lake: YHWH ni mwingi wa rehema na uaminifu, anawaonea wivu watu wake, yaani hawezi kukubali waabudu miungu mingine kwa hasara yao. Ndiyo sababu alipoagana nao kwa kuandika tena amri zake kumi katika mawe, pamoja na kuahidi kuwafukuza wenyeji wa nchi takatifu ili kuwapatia nafasi Waisraeli, aliwaagiza wasichanganyikane nao wasije wakavutwa katika Upagani. Hasa alikataza ndoa za mseto ili kulinda usafi wa imani. Kwa namna ya pekee Kristo analipenda na kulionea wivu Kanisa lake analolitaka bikira safi katika imani na maadili (2Kor 11:2; Ef 5:25-27): hivyo tunaposhirikiana na watu wengine tuwe macho tusifuate mawazo, maneno na matendo yao, bali tushuhudie imani na upendo kwa maisha yetu tofauti na ya kwao (Yoh 17:15-17).

Mwendelezo wa habari katika Kitabu cha Hesabu

hariri

Kitabu cha nne cha Biblia kinaitwa hivyo kwa sababu kinaleta hesabu mbalimbali, hasa ya idadi ya Waisraeli: wanaume wa kuweza kwenda vitani walikuwa 603,500 (mbali na Walawi waliohesabiwa peke yao: wanaume 22,000 wakiwa pamoja na watoto wa kiume); ukiongeza wanawake na watoto mpaka umri wa miaka ishirini, basi jumla yao iliweza kufikia watu milioni tatu, ingawa si lazima kuamini idadi hiyo ni sahihi (pengine namba hizo hazilingani katika makala kwa kuwa ilikuwa rahisi kukosea wakati wa kunakili).

Uzito wa kazi ya kuwaongoza watu wengi hivyo wanaonung’unika kila mara ulimchosha Musa hata akamuomba Mungu tena ampunguzie mzigo au amuue kabisa (Hes 11:1-30). Musa alieleza shida yake kama rafiki kwa mwenzake, kwa unyofu uleule wa watu wengine wa Mungu katika Biblia. Mungu akamkubalia akawashirikisha watu sabini roho yake kwa ajili ya uongozi katika ngazi mbalimbali. Huo pia ni mfano wa Agano Jipya, ambapo askofu hawezi kuchunga waamini peke yake, bali anahitaji msaada wa viongozi wa daraja za chini, yaani mapadri na mashemasi (Mdo 6:1-6). Katika nafasi hiyo Musa alimueleza Yoshua kwamba hawaonei kijicho kwa kupewa karama, tena angependa kama Waisraeli wote wangekuwa manabii. Hamu hiyo ikatimia siku ya Pentekoste: katika Kanisa wote wanapewa Roho Mtakatifu na kuwa manabii, hata wanawake na watoto (Mdo 2:16-18).

Kinyume chake Hes 12 inasimulia kijicho kilivyowafanya dada na kaka wa Musa wamseme wakijidai nao pia ni manabii. Lakini Mungu akawaeleza kuna namna mbalimbali za unabii, na Musa ni wa pekee. Kisha akatoa adhabu ambayo ikaondolewa kwa maombezi ya Musa tu: ndiyo sababu anasifiwa kwa upole wake. Kijicho kitasumbua daima taifa la Mungu, hata katika Agano Jipya (1Kor 12:1-31; 14:37-38).

Waisraeli walipofikia mipakani mwa nchi takatifu walituma wapelelezi ili waivamie, nao waliporudi walisimulia uzuri wake, lakini pia walitisha kwa kuzidisha habari za wananchi na miji yao (Hes 13). Hapo Waisraeli wakaanza kunung’unika usiku kucha (Hes 14) wakapanga kuwaua kwa mawe Kalebu na Yoshua waliotaka kuivamia nchi bila ya hofu kwa jina la Bwana. Lakini Mungu akaonyesha utukufu wake na kutisha ataleta tauni ili kuwaangamiza wote kwa ukaidi wao. Kwa maombezi ya Musa, akakubali kuwahurumia lakini akaamua warudi jangwani na kuzungukazunguka huko mpaka wafe wote; ila watoto wao pamoja na Kalebu na Yoshua ndio watakaoingia nchi takatifu kuimiliki. Maana ya kiroho ni kwamba hatutakiwi kuzitia shaka ahadi za Mungu; hata zikionekana ngumu kupatikana, ni lazima tuwe na moyo mkuu na imani hata tukabili vipingamizi vyovyote.

Kinyume chake, Waisraeli walipoamua kuivamia nchi kwa kusikitikia adhabu waliyopewa wakashindwa kabisa, maana ni lazima tumtii Mungu kwa wakati wake. Pia kughairi kutokana na matatizo kunaweza kukatusukuma tutende namna ambayo haimpendezi tena; ni lazima tuchukue majukumu ya matendo yetu na kukubali adhabu au matatizo tuliyojitakia:majuto hayo yanafaa kwa kuonyesha utiifu kwa Mungu (Zab 119:71).

Manung’uniko ya Waisraeli katika safari yao jangwani yakawaletea adhabu nyingine, mojawapo ile ya kugongwa na nyoka wengi wenye sumu kali. Lakini walipoomba msamaha, Mungu akamuagiza Musa atengeneze nyoka wa shaba na kumuinua juu ya mti ili mtu aliyeumwa akimtazama tu apate kupona (Hes 21:4-9). Ufafanuzi wa tukio hilo ulitolewa na Yesu mwenyewe: ndiye aliyeinuliwa juu ya mti wa msalaba ili watakaomtazama kwa imani wapate kuishi (Yoh 3:14-15).

Musa katika kitabu cha Kumbukumbu la Sheria

hariri

Kitabu hicho cha mwisho cha Torati kiliandikwa kama miaka 600 baada ya Musa, ingawa kina namna ya hotuba tano alizoweza kuwatolea Waisraeli kabla hajafa. Kinasisitiza sana uaminifu kwa sheria za Agano la Kale na pia tuzo na adhabu zitakazotolewa kufuatana na matendo ya Waisraeli.

Katika maneno yake yote ya kukumbukwa ni hasa yale ya 6:4-9 ambayo Mwisraeli yeyote anayakariri kila siku katika sala na kuyashika neno kwa neno.

Maneno mengine muhimu sana yapo 26:5-10: ni kama kanuni ya imani ambayo Mwisraeli alikuwa anaiungama mbele ya Mungu wakati wa kumtolea malimbuko ya ardhi. Hivyo alikuwa akikiri amepewa yote na Bwana, halafu akaweza kuyafurahia mavuno.

Baada ya hotuba hizo, Kumb 31:1-8 inasimulia jinsi Musa alivyomuachia Yoshua uongozi wa Waisraeli wote kwa kumwekea mikono (Hes 27:12-23). Musa alifikia mpakani mwa nchi takatifu asikubaliwe kuiingia kama adhabu ya makosa yake, ila alionyeshwa yote kutoka mlimani (Kumb 32:48-52) halafu akafariki (Kumb 34) na kuzikwa ng'ambo ya mto Yordani. Kazi aliyopangiwa iliishia huko, mwingine akampokea na kuendeleza ukombozi wa Kimungu. Binadamu wote ni vyombo tu vinavyotumika kwa muda fulani, halafu vinaweza kuachwa. Kumbe Mungu ndiye mtendaji mwenyewe ambaye hasinzii wala halali, bali anazidi kuwashughulikia watu wake. Kwa imani hiyo tuwe daima tayari kuwaachia wengine nafasi yetu.

Anakumbukwa kama kiongozi na mwanzilishi wa dini ya Uyahudi.

Sala yake (Kut 33:18)

hariri

"Nakusihi unionyeshe utukufu wako".

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Marejeo

hariri
  NODES
mac 2
os 34