Schutztruppe
Schutztruppe (tamka shuts-tru-pe; Kijerumani kwa "Jeshi la Ulinzi") ilikuwa jina la jeshi la kikoloni la Ujerumani hadi Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Ilifanywa na askari Waafrika chini ya amri wa maafisa Wajerumani. Ilianzishwa katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (hasa Tanganyika ya baadaye) ikaendelea kupanuliwa pia katika makoloni ya Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani (Namibia ya leo) na Kamerun.
Katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani jeshi hilo lilikuwa na vikosi 14 vyenye askari 2,500 kwa jumla. Chini ya mkuu Paul von Lettow-Vorbeck Schutztruppe ilipiga Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ikaweza kuendelea hadi mwisho wa vita na kusalimu amri siku chache baada ya mwisho wa vita.
Chanzo
haririChanzo cha jeshi hili kilikuwa kikosi kilichoajiriwa na Hermann von Wissmann mwaka 1889 kwa niaba ya Dola la Ujerumani kwa kusudi la kukomesha vita ya Abushiri kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki. Hapa wakazi wa pwani ya Tanzania ya leo walipinga majaribio ya Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki ya kushika utawala juu ya pwani. Wissmann aliajiri maafisa 21 na maafande 40 kutoka Ujerumani akaelekea Afrika. Njiani alipita Misri akawaajiri askari Wasudan 600 kutoka jeshi la Misri (walioachishwa kazi wakati ule kutokana na kupungukiwa kwa jeshi la Misri baada ya vita ya Mahdi). Wakati huohuo alimtuma afisa moja, luteni Hans von Ramsay, kwenda Hori ya Inhambane, Msumbiji alipoajiri askari 150 Wazulu kama nyongeza[1]. Jeshi hili lilijulikana kama "Wissmanntruppe" (kikosi cha Wissmann). Kwa kutumia silaha za kisasa kama bombomu walifaulu kushinda upinzani dhidi ya utawala wa Kijerumani.
Mwaka 1891 kikosi hiki kiliajiriwa na serikali yenyewe na kwa sheria maalumu kuwa sehemu ya jeshi la Ujerumani, ikipangwa mwanzoni iwe chini ya usimamizi wa jeshi la majini na kuitwa "Schutztruppe für Ostafrika" yaani jeshi la ulinzi kwa Afrika ya Mashariki.
Katika miaka iliyofuata vikosi vilivyoitwa "Schutztruppe" viliundwa pia katika koloni za Afrika ya Kusini-Magharibi ya Kijerumani (Namibia) na Kamerun. Mwaka 1896 vikosi hivyo katika koloni viliunganishwa kama mkono wa pekee wa jeshi la Ujerumani chini ya amri kuu ya Kaisari mwenyewe; Schutztruppe ndani ya kila koloni ilikuwa chini ya mamlaka ya gavana wa koloni.
Askari wa vikosi katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani na Kamerun walikuwa Waafrika walioajiriwa, wakitekeleza shughuli chini ya maafisa na maafande Wajerumani; kulikuwa pia na maafisa na maafande wachache Waafrika wenye cheo cha "efendi"[2]. Katika Afrika ya Kusini-Magharibi hapakuwa na askari Waafrika, hata askari wa kawaida walikuwa Wajerumani.
Schutztruppe kabla ya Vita Kuu
haririMnamo mwaka 1913 jeshi la Schutztruppe lilikuwa na maafisa 69 Wajerumani, maafisa waganga Wajerumani 42, wafanyakazi Wajerumani wa ofisini 12, maafande wa kijeshi Wajerumani 60, maafande wa kiganga 66 na askari Waafrika 2,472.
Hao waligawiwa katika vikosi 14 pamoja na ofisi kuu ya utawala Dar es Salaam na kituo cha kufunza askari wapya.
Kila kikosi kilikuwa na askari 160-200, waliopangwa kwa platuni 3 za askari 50-60. Kila platuni ilikuwa na vikundi 2 vya bombomu. Kila kikosi kilikuwa pia na kundi la wapagaji takriban 250.
Vikosi hivi vilipangwa mahali pafuatapo:
- Kikosi cha 1.: Arusha
- Kikosi cha 2.: Iringa na Ubena
- Kikosi cha 3.: Lindi
- Kikosi cha 4.: Kilimatinde na Singida
- Kikosi cha 5.: Masoko (Neu-Langenburg / Tukuyu)
- Kikosi cha 7.: Bukoba, Usuwi (Biharamulo) na Kifumbiro
- Kikosi cha 8.: Tabora
- Kikosi cha 9.: Bujumbura (Burundi)
- Kikosi cha 10.: Dar es Salaam
- Kikosi cha 11.: Kisenji na Ruhengeri (Rwanda)
- Kikosi cha 12.: Mahenge
- Kikosi cha 13.: Kondoa-Irangi
- Kikosi cha 14.: Mwanza na Ikoma
Tazama pia
haririMarejeo
hariri- ↑ Florian Hoffmann: Okkupation und Militärverwaltung in Kamerun,uk 159, Göttingen 2007, ISBN 9783867274739
- ↑ Cheo cha "efendi" kilipokelewa kutoka jeshi la Kituruki katika Misri ambako askari wengi wa kwanza waliajiriwa na Wissmann. Cheo hiki kikaingia katika lugha ya Kiswahili kwa umbo la "afande"
Kujisomea
hariri- Kopf, Werner. The German colonial force 1889/1918, Dörfler Publishing House
- Morlang, Thomas. Askari und Fitafita. Farbige Söldner in den deutsche Kolonien. Berlin 2008
- Reith, Wolfgang. The Command Authorities of the Imperial Colonial Force in the Homeland. German Soldier Yearbook 2000 and 2001 (2 parts). Munich: Signal Publishing House.
- Farwell, Byron. The Great War in Africa, 1914–1918. New York: W. W. Norton & Company. 1989. ISBN 0-393-30564-3
- Haupt, Werner. Deutschlands Schutzgebiete in Übersee 1884–1918 [Germany’s Overseas Protectorates 1884-1918]. Friedberg: Podzun-Pallas Verlag. 1984. ISBN 3-7909-0204-7
- Hoyt, Edwin P. Guerilla. Colonel von Lettow-Vorbeck and Germany's East African Empire. New York: MacMillan Publishing Co., Inc. 1981; and London: Collier MacMillan Publishers. 1981. ISBN 0-02-555210-4.
- Miller, Charles. Battle for the Bundu: The First World War in German East Africa. London: Macdonald & Jane's, 1974; and New York: MacMillan Publishing Co., Inc. 1974. ISBN 0-02-584930-1.
Viungo vya Nje
hariri- Makala "Schutztruppen" katika Kamusi ya Koloni za Kijerumani (1920) (jer.) Archived 17 Mei 2017 at the Wayback Machine.
- German Colonial Uniforms
- A German language naval and military history site
German language sites: