Tumbaku (pia tumbako) ni majani (minoga) makavu ya mtumbaku ambayo yanatumiwa na binadamu kwa kuvutwa kama sigara, kutafunwa mdomoni au kunuswa. Tumbaku ndani yake huwa na kemikali ya nikotini ambayo mwili unaizoea haraka sana na kufanya iwe vigumu kwa wavuta tumbaku kuachana na desturi hiyo.

Majani ya tumbaku yaliyokatwa tayari kwa kanda nyembamba sana, tayari kwa kutengeneza sigara.

Asili ya tumbaku

hariri

Asili ya tumbaku ni Amerika ambako wenyeji Waindio waliitumia kama dawa ya kidini, pia burudani. Tangu zamani za Kristoforo Kolumbus, Wahispania walipeleka mtumbaku hadi Ulaya ambako uliangaliwa mwanzoni kama mmea wa kiganga. Matumizi hasa kwa njia ya kuvuta na kutafuna yalienea haraka katika Ulaya na kwa njia ya mabaharia Wareno katika pande zote za dunia.

 
Shamba la tumbaku nchini Kuba.

Kazi ya nikotini ndani ya tumbaku

hariri

Tumbaku inavutia hasa kwa sababu nikotini ambayo ni dawa ndani yake inaathiri ubongo na neva ya binadamu na kupunguza uchovu na kusaidia mtu kusikia utulivu na raha. Tofauti na dawa nyingine kama pombe, bangi au afyuni yanayoathiri pia ubongo na neva, tumbaku haisababishi hali ya ulevi. Lakini inasababisha haraka zoea la mwili unaoshikwa na hamu ya kupata nikotini tena na tena. Hapo ni vigumu kwa watu walioanza kutumia tumbaku mara kwa mara kuachana na matumizi yake.

Hatari za kiafya

hariri

Matumizi ya tumbaku yamegunduliwa kuwa kati ya sababu kuu za magonjwa mengi kwa binadamu pamoja na kansa, magonjwa ya moyo na mapafu, na mengine. Magonjwa hayo hayasababishwi na nikotini lakini na desturi ya kuvuta tumbaku. Moshi wa majani ya tumbaku huwa na maelfu ya kemikali ndani yake: ni hasa kemikali hizo zinazoingizwa ndani ya mwili wakati wa kuvuta ambazo ngozi ndani ya mwili, mishipa, moyo na mapavu. Kwa hiyo nikotini inamlazimisha mvutaji kuvuta tena na tena na hivyo kuingiza mwilini kemikali nyingi zenye hasara.

Matumizi ya tumbaku nje ya kuvuta (kutafuna, kunusa) yamegundunduliwa kupunguza hatari hizo za kiafya lakini yanaleta matatizo yaleyale ya kutegemea nikotini na kutoachana nayo.

 
Nchi zilizolima zaidi ya tani 100,000 za tumbaku mwaka 2000.

Kilimo

hariri

Kilimo cha tumbaku ni tawi muhimu la uchumi kwa nchi mbalimbali. Kila mwaka mavuno duniani ni takriban tani milioni 6.7. Wazalishaji wakuu ni China (39.6%), Uhindi (8.3%), Brazil (7.0%) na Marekani (4.6%). [1] Tanzania ni kati ya nchi kumi za kwanza zinazolima tumbaku, huku inavuna asilimia 1.6 ya tumbaku yote ya dunia.[2]

Katika nchi zilizoendelea kilimo cha tumbaku kimepungua na kiasi cha China kimeongezeka.

 
Majani ya tumbaku wakati wa kukauka.

Baada ya mavuno

hariri

Mavuno hutokea siku 70 hadi 130 baada ya kulima shamba. Majani huvunia wakati yanapoanza kuonyesha rangi ya manjano maana yameiva. Mavuno yanakwenda kwa uangalifu kwa sababu mashimo katika majani yanapunguza ubora na bei. Baada ya mavuno majani yanafungwa pamoja kwa kamba na kukaushwa. Kuna mbinu za kuzikausha polepole kivulini au juu ya moto au penye hewa ya moto haraka katika muda wa siku chache tu.

Majani yaliyokauka hufungwa pamoja kwa mchakato wa kuchachua. Huu unabadilisha ladha ya tumbaku kwa njia inayotakiwa. Baadaye tumbaku hutiwa sosi zenye sukari au vitu vingine vya kutia ladha halafu hukatwa na kufungwa kulingana na matumizi kama tumbaku ya kuvuta katika sigara za kawaida, sigara kubwa, pipo, ya kutafunia au ya kunusa.

Marejeo

hariri
  1. US Census Bureau-Foreign Trade Statistics, (Washington DC; 2005)
  2. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2016-03-07. Iliwekwa mnamo 2014-06-02. {{cite web}}: Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help)

Viungo vya Nje

hariri
  NODES
Association 1
INTERN 1