Vita Kuu ya Pili ya Dunia

(Elekezwa kutoka Vita Kuu ya Dunia ya Pili)

Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilikuwa vita iliyodumu kuanzia mwaka 1939 hadi 1945 kati ya Ujerumani, Italia, Japani na mataifa yaliyoshikamana nazo (Romania, Hungaria na Bulgaria) dhidi ya nchi nyingi za dunia (ziliitwa mataifa ya ushirikiano) kati yake hasa Uingereza, Uchina, Urusi na Marekani.

Vita Kuu ya Pili ya Dunia

Vita Kuu ya Dunia

hariri

Jina limetokana na vita ya miaka 1914-1918 iliyoona mapambano kati ya Ujerumani na wenzake dhidi ya nchi nyingi. Vita ya 1914/1918 iliitwa "Vita Kuu ya Dunia" kwa sababu mapigano yalienea pande nyingi za dunia, tofauti na vita zilizotangulia.

Kwa namna fulani vita iliyoanza 1939 ilikuwa marudio ya vita iliyotangulia. Hivyo imekuwa kawaida kuzitaja vita hizi kama Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia.

Mwanzo wa vita

hariri

Vita hii ilianza huko Ulaya tarehe 1 Septemba 1939 kwa mashambulizi ya Wajerumani dhidi ya Poland. Wengine huhesabu mashambulizi ya Japani dhidi ya Uchina tarehe 7 Julai 1937 kuwa mwanzo wa vita. Mwisho wake ulikuwa huko Ulaya tarehe 9 Mei 1945 halafu huko Asia tarehe 2 Septemba 1945.

Vita katika Ulaya

hariri

Wakati Ujerumani iliposhambulia Poland, nchi hiyo ilikuwa na mikataba ya kulindana na Uingereza na Ufaransa. Hivyo ilibidi Uingereza na Ufaransa zitangaze hali ya vita dhidi ya Ujerumani. Serikali za Australia, New Zealand, Nepal, Afrika Kusini na Kanada zilishikamana na Uingereza kwa kutangaza vita dhidi ya Ujerumani. Umoja wa Kisovyeti ilikuwa na mkataba wa siri na Ujerumani ikaweza kuchukua nafasi ya kuteka sehemu kubwa za Poland ya Mashariki.

Baada ya uvamizi wa Poland hali kwenye mpaka na Ufaransa ilibaki kimya ingawa vita ilikuwa imeshatangazwa. Uingereza ilipeleka sehemu kubwa ya jeshi lake huko Ufaransa kwa kusudi la kutetea nchi hiyo kama Ujerumani itashambulia.

Mwezi Aprili 1940 Waingereza walianza kupeleka wanajeshi Norway wakiwa na shabaha ya kuzuia kupelekwa kwa madini ya chuma kutoka Sweden kwenda Ujerumani kupitia bandari za Norway. Wajerumani walichukua nafasi hiyo kuteka Denmark na Norway na kufukuza Waingereza.

Mnamo Mei 1940 Wajerumani walishambulia Ufaransa. Walitumia mbinu ya kupitia Uholanzi, Ubelgiji na Luxemburg zilizowahi kutangaza kwamba hawako upande wowote katika vita. Mapigano hayo yalikwisha haraka: Wajerumani walishinda na kupiga kikosi cha Waingereza pamoja na jeshi la Ufaransa. Lakini Waingereza walifaulu kuokoa wanajeshi wao kutoka Dunkirk kwa meli walipozingirwa na Wajerumani kwa sababu Hitler aliwaamuru kusubiri. Baadaye walisitasita kushambulia Uingereza yenyewe. Mipango yao ilihitaji mbinu za kuvuka bahari. Wakajaribu kuvuruga nguvu ya kijeshi ya Waingereza kwa mashambulizi ya ndege lakini pia hapo Hitler hakuendelea mashambulio dhidi ya wanahewa wa Uingereza na hatimaye kukosa uwezo wa kutosha. Katika shambulizi dhidi ya Ufaransa Waitalia walishiriki upande wa Wajerumani.

Mwisho wa mwaka 1940 Waitalia walianza kushambulia Ugiriki na jeshi la Waingereza huko Misri na Malta. Lakini mahali pote walirudishwa nyuma, hadi dikteta Mjerumani Adolf Hitler alipoamua kuwasaidia Waitalia na kupeleka wanajeshi Wajerumani kwenda Afrika ya Kaskazini pamoja na Ugiriki mwaka 1941. Hii ilisababisha pia Wajerumani kuteka Yugoslavia wakiwa njiani kwenda Ugiriki.

Vita ya kidunia

hariri

Mwaka wa 1941 uliona vita kubadilika kutoka vita ya Kiulaya kuwa vita ya kidunia.

Wajerumani walishambulia Urusi wakifika hadi kando ya mji mkuu Moscow, lakini walishindwa kuiteka. Walikamata eneo lote la kusini mwa Urusi hadi milima ya Kaukazi na hadi mto Volga.

Wajapani walishambulia Marekani pamoja na makoloni ya Waingereza na Waholanzi huko Asia. Hitler alitangaza pia vita dhidi ya Marekani akitaka kuwasaidia Wajapani ingawa Japan haikushambulia Urusi.

Katika miaka iliyofuata nguvu ya Ujerumani na Japani ilipungua. Hasa uwezo wa kiuchumi wa Marekani ulizalisha mitambo na silaha kwa mkasi usiopatikana kwa Wajerumani na Wajapan. Ukali wa utetezi wa Warusi ulichosha nguvu za Wajerumani.

Kuanzia mwaka 1943 mataifa ya ushirikiano yalianza kusogea mbele pande zote. Warusi walisukuma Wajerumani polepole warudi nyuma. Waamerika na Waingereza walipeleka wanajeshi Italia ya Kusini. Italia ilifanya mapinduzi: dikteta Mwitalia Mussolini aliondolewa madarakani na serikali mpya ilijiunga na mataifa ya ushirikiano.

Mwaka 1944 askari wa mataifa ya ushirikiano waliingia Ufaransa wakielekea Ujerumani. Wakati huohuo Warusi walisogea mbele zaidi wakikaribia mipaka ya Ujerumani. Huko Asia Japan ilipoteza sehemu kubwa sana ya meli zake za kivita na Jeshi la Marekani lilikaribia visiwa vya Japani tayari.

Mwisho wa vita

hariri

Mwaka 1945 iliona mwisho wa vita. Mataifa mengi yaliyokuwa mbali, kama Argentina, Peru au Mongolia, yalitangaza pia hali ya vita dhidi ya Ujerumani na Japani. Pia nchi zilizowahi kushikamana na Wajerumani waligeukia mataifa ya ushirikiano. Ujerumani yenyewe ilivamiwa kutoka Magharibi na Mashariki. Warusi walifika mji mkuu wa Berlin na Adolf Hitler alijiua tarehe 30 Aprili 1945; wanajeshi wake walitia sahihi mkataba wa kusalimu amri tarehe 8-9 Mei 1945.

 
Wingu la kinyuklia juu ya Nagasaki tarehe 9 Agosti 1945

Huko Asia Japani iliendelea kupigana na Waamerika walioweza kufikisha ndege zao zilizobeba mabomu hadi Japani yenyewe. Mnamo Agosti 1945 Waamerika walitumia silaha mbili za kinyuklia walizokuwa nazo wakati ule na kuua watu wengi sana huko Hiroshima tarehe 6 Agosti na Nagasaki tarehe 9 Agosti 1945. Siku zilezile Warusi walianza kuwashambulia wanajeshi Wajapani huko Uchina. Haya yote yalisababisha serikali ya Japani kukubali wameshindwa wakatia sahihi mkataba wa kusalimu amri tarehe 2 Septemba 1945.

Waliokufa vitani

hariri

Kwa jumla takriban watu milioni 60 walikufa kutokana na vita hivi. Makadirio hutaja wanajeshi milioni 25 na raia milioni 35. Taifa lililopoteza watu wengi ni Urusi walipokufa kati ya milioni 20-28, idadi kubwa wakiwa raia.

Takriban watu milioni 10 waliuawa na Wajerumani au walikufa kutokana na kutendewa vibaya nje ya mapigano, kama vile milioni 6 za Wayahudi, wengine Wapoland, Warusi, Wasinti, walemavu n.k.

Umoja wa Mataifa

hariri

Tokeo mojawapo la vita kuu ya pili ni kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa. Uliundwa mwaka 1945 kama chombo cha kuzuia vita zijazo. Kutokana na historia hiyo mataifa yenye nafasi za kudumu na kura ya veto katika Baraza la Usalama ndiyo mataifa washindi wa vita kuu ya pili: Marekani, Uchina, Ufaransa, Ufalme wa Muungano na Urusi. Kutokana na kura ya veto hawawezi kuondolewa bila kukubali wenyewe hata kama siku hizi Ufaransa na Ufalme wa Muungano si tena nchi muhimu sana duniani.

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Vita Kuu ya Pili ya Dunia kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  NODES