Witu ni mji mdogo, kata na tarafa katika kaunti ya Lamu, eneo bunge la Lamu Magharibi, mashariki mwa Kenya[1].

Bendera ya Sultani Fumobakari wa Witu mnamo mwaka 1890.

Mji huu upo kilomita 5 (maili 3) magharibi mwa msitu wa Witu, barabarani kutoka Malindi kwenda Lamu, takriban katikati ya mto Tana na Lamu.

Katika karne ya 19 ilikuwa mji mkuu wa Usultani wa Witu. Kwa muda mfupi, kati ya mwaka 1885 hadi 1890, usultani wa Witu ulikuwa nchi lindwa chini ya Ujerumani na sehemu ndogo katika delta ya mto Tana ilikuwa koloni la moja kwa moja.

Ramani ya kihistoria (mnamo 1890) ya pwani ya kaskazini ya Afrika ya Mashariki pamoja na Witu.

Idadi ya watu

hariri

Mnamo Septemba mwaka 2013, idadi ya wakazi wa mji huo imekadiriwa kuwa 5,380.

Historia

hariri

Kulikuwa mahali pa makazi ya Waswahili wa kale katika pwani ya kaskazini ya Kenya kwenye Bahari ya Hindi.

Historia ya Witu ilianza mwaka 1858 BK. Sultani wa Pate Ahmad ibn Fumo Bakari, aliyezaliwa katika familia ya watawala wa Nabahani, alijenga makao mapya barani kwa sababu alitaka kujiokoa na Usultani wa Zanzibar uliotafuta utawala juu ya funguvisiwa la Lamu wakati ule.

Mashambulio ya Wazanzibari yaliendelea na kumsababisha sultani kuomba msaada wa ulinzi wa Ujerumani mara ya kwanza mwaka 1867. Mwaka 1885 Sultani alifunga mkataba na ndugu Wajerumani Clemens na Gustav Denhardt akaweka nchi yake chini ya ulinzi wa Dola la Ujerumani kuanzia tarehe 27 Mei 1885. Kama shukrani kwa ndugu Denhardt aliwapa eneo la maili za mraba 25 akawafanya kuwa mawaziri wake.

Sultani wa Zanzibar hakufurahia habari hizi wala balozi wa Uingereza Zanzibar mjini. Lakini mipango yao dhidi ya Witu ilishindikana kwa sababu serikali ya Ujerumani ilituma manowari SMS Gneisenau Afrika ya Mashariki na wanajeshi 30 Wajerumani walipiga kambi Witu. Mwaka 1888 Ujerumani ilifungua ofisi ya posta Lamu mjini kwa ajili ya mawasiliano kati ya Witu na Ujerumani kwa sababu meli zilipita mara kwa mara Lamu ilhali Witu haikuwa na bandari kamili.

Serikali ya Ujerumani haikuonyesha nia ya kuimarisha utawala wake kwenye pwani ya Kenya; iliona Witu kama bidhaa kwa ajili ya biashara na Waingereza. Katika mkataba wa Helgoland-Zanzibar Witu iliachiliwa Uingereza na ulinzi wa Ujerumani ulikwisha tarehe 1 Julai 1890.

Wenyeji wa Witu hawakupendezwa na mabadiliko hayo kwa sababu waliogopa ya kwamba watafikishwa chini ya Zanzibar, angalau waliwajua Waaingereza kuwa karibu sana na Sultani wa Zanzibar. Walihisi kuwa Wajerumani waliwasaliti. Katika Septemba 1890 ilitokea ugomvi mkali. Mfanyabiashara Mjerumani Andreas Küntzel alitegemea kuanzisha biashara katika eneo la Sultani lakini alikataliwa kwa sababu ya hasira iliyosababishwa na mkataba wa Julai 1890. Wenzake Küntzel walijaribu kulazimisha maafisa wa Sultani kwa kuonyesha silaha lakini walikamatwa, na silaha zao kuchukuliwa. Küntzel alijaribu kuwaweka huru akamtukana sultani mbele ya watu wake. Wenyeji wenye hasira waliwaua Wajerumani wale na kushambulia Wazungu wengine. Jumla Wajerumani 9 waliuawa, wengine wakakimbia.

Waingereza walituma jeshi chini ya Admirali Sir E. Freemantle wakavamia Witu katika Septemba 1890. Tarehe 28 Oktoba 1890 mji mkuu wa Witu ulichomwa moto na Waingereza. Lakini mapigano yaliendelea. Kuna makadirio ya kwamba wenyeji 500 waliuawa, mji Witu ikaharibika na Sultani alitupwa jela alikokufa. Mapigano yaliendelea hadi mwaka 1894. Witu ikawa koloni la Uingereza. Katika mkataba wa Helgoland-Zanzibar Uingereza iliahidi ya kwamba itaheshimu mipaka ya eneo la Witu. Awali Waingereza walimteua sultani mpya Omar-bin-Hamed aliyetoka katika ukoo wa Nabahani vilevile.

Lakini baadaye hawakuheshimu tena usultani wa Witu jinsi walivyowahi kuahidi katika mkataba wa 1890 wakaitendea kama sehemu ya mkoa wa Tana tu.

Baada ya kifo cha Sultani mwaka 1923 usultani ulikwisha kabisa.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Viungo vya nje

hariri
  NODES