African National Congress, kwa kifupi "ANC", ni chama cha kisiasa kinachotawala nchini Afrika Kusini. Mwenyekiti wake tangu Desemba 2017 ni Cyril Ramaphosa aliyemshinda mtangulizi wake Jacob Zuma ambaye alikuwa rais wa Afrika Kusini hadi 2018.

Nembo la ANC

Kuanzishwa kwa ANC

hariri

ANC ilianzishwa mjini Bloemfontein tar. 8 Januari 1912 kwa jina la "South African Native National Congress". Jina la "Congress" lilichaguliwa kufuatana na mfano wa chama cha Kinhindi cha "Indian National Congress" ilikuwa chama cha kwanza katika koloni za Uingereza kilichodai mabadiliko ya ukoloni kwa njia ya kisiasa. Madai ya ANC yalikuwa hasa haki kwa ajili ya wakazi asilia katika nchi mpya ya Umoja wa Afrika Kusini. Mwaka 1924 jina likabadilishwa kuwa "African National Congress".

Chama kilidai haki sawa kwa wakazi wote bila kujali rangi yao. Mwendo huu uliunganisha Waafrika kutoka pande mbalimbali kama vile wasomi, machifu, viongozi wa kanisa na wengine. Wanawake walikubaliwa tangu 1931 na 1943 wakapewa haki zote za uanachama.

Umoja wa Vijana

hariri

Umoja wa Vijana wa ANC (ANC Youth League) ulianzishwa 1944 na Nelson Mandela, Walter Sisulu na Oliver Tambo ukaongeza ukali katika mwendo wa kupinga ubaguzi wa rangi bila kutumia mabavu au silaha. 1947 ANC iliamua kushikama kwa karibu na vyama vya Natal Indian Congress na Transvaal Indian Congress.

Kipindi cha Apartheid (ubaguzi wa rangi wa kisheria)

hariri

Ushindi wa National Party katika uchaguzi wa raia weupe pekee mwaka 1948 ulileta mwanzo wa siasa ya Apartheid iliyolenga kuwaondoa Waafrika kabisa katika siasa ya Afrika Kusini hata katika eneo lake isipokuwa kwa wafanyakazi waliotakiwa kukaa kwa muda tu na uhamisho wa Waafrika wote katika mikoa ya Bantustan.

Kadiri jinsi ukandamizaji dhidi ya Waafrika ulivyoongezeka ANC ikaongeza ukali wa upinzani hadi kuunda kwa siri idara ya kijeshi kilichoitwa "Umkhonto We Sizwe" ("mkuki wa taifa") iliyoanzishwa na Nelson Mandela. Azimio la kuchukua hatua hii ilichukuliwa baada ya mauaji ya Sharpeville tar. 21 Machi 1960.

ANC marufuku

hariri

8 Aprili 1960 ANC ikapigwa marufuku. Wanaharakati wengi walikamatwa wengine wakakimbia nje ya Afrika Kusini. Viongozi kama Walter Sisulu na Nelson Mandela wakafungwa jela. ANC iliendelea kufanya kazi kwa siri lakini viongozi wote huru walikaa nje ya nchi. Oliver Tambo aliongoza chama kutoka makao makuu huko Zambia. Kwa jumla ANC ilifaulu kiasi katika kempeni yake ya kutangaza maovu ya ubaguzi wa rangi kimataifa na kuandaa maazimio ya Umoja wa Mataifa dhidi yake. Majaribio ya kupinga serikali kijeshi hayakufaulu sana na ANC haikupita kwenye ngazi ya uchafuzi, kutega mabomu na kuua watu wachache ndani ya nchi walioonekana wakisaidia siasa ya serikali.

Harakati ya wanafunzi Waafrika wa Afrika Kusini walioanza kupigana na polisi tangu 1976 imekua bila kuathiriwa sana na ANC. Upinzani huu uliendelea pamoja na migomo ya wafanyakazi kwenye migodi.

Mwisho wa Apartheid

hariri

Hadi mwisho wa miaka ya 1980 serikali ya Makaburu iliona ugumu kuendelea na siasa ya Apartheid jinsi ilivyokuwa. Gharama za ukandamizaji wa upinzani zilikua na pamoja na mwisho wa "vita baridi" siasa ya nchi zilizowahi kusaidia serikali ya Apartheid ikaanza kubadilika kwa kudai kuongeza haki za Waafrika.

Katika hali hiyo viongozi Makaburu walianza majadiliano kwa siri na Nelson Mandela na pia na viongozi wa ANC nje.

Tar. 2 Februari 1990 Rais F.W. de Klerk alitangaza ya kuwa ANC si marufuku tena. Baada ya tangazo hili Nelson Mandela alikubali kuondoka gerezani. Sheria za Apartheid zikafutwa.

Katika uchaguzi huru wa kwanza wa Afrika Kusini ANC ikapata asilimia 62 ya kura. Mandela akawa rais pamaoja na makamu wawili De Klerk na Thabo Mbeki.

ANC imeendelea kushinda kura za kitaifa katika Afrika Kusini. Vyama vya upinzani vimepata kura nyingi katika majimbo vya Western Cape na Kwa-Zulu Natal.

Mwaka 2005 chama cha New National Party (iliyoendeleza kazi ya National Party ya awali) ikajiunga na ANC.

  NODES