Chingis Khan (pia: Genghis Khan; takriban 116218 Agosti 1227) alikuwa kiongozi wa Wamongolia aliyeunda Milki ya Wamongolia iliyoendelea kutawala eneo kubwa kuanzia China pamoja na Asia ya Kati hadi Urusi na Mashariki ya Kati.

Chingis Khan (picha ya karne ya 14 BK)
Dola la Chingis-Khan wakati wa kifo chake 1227 BK; mipaka ya nchi za kisasa

Kuunganisha makabila ya Wamongolia

hariri

Alizaliwa kwa jina la Temujin kama mtoto wa chifu wa kabila la Kimongolia. Wakati ule Wamongolia walikuwa wafugaji wahamaji walioishi kaskazini mwa nchi ya Mongolia ya leo. Walikuwa na makabila mengi yaliyoendelea kupigana kwa vita. Temujin alishiriki katika vita vingi akaendelea kuunganisha makabila mbalimbali. Tangu mwaka 1201 alikuwa na nguvu ya kutosha akashambulia mataifa ya jirani kama Watartari waliowahi kumwua baba yake akawashinda. Mwaka 1206 Temujin aliitisha mkutano wa viongozi wote wa Wamongolia waliomkubalia kama kiongozi mkuu na kumpa cheo cha "Chingis Khan" yaani mtawala mkubwa.

Sheria za kimaandishi

hariri

Maazimio ya mkutano yalianzisha dola jipya ambamo Temujin alikuwa mtawala pekee mwenye madaraka ya kutunga sheria. Alitawala kwa msaada wa halmashauri iliyokuwa na mama yake, kaka yake na wana wake. Temujin alimwagiza mwana wake aliyejua mwandishi kuandika sheria zote za kale zilizohifadhiwa kwa kumbukumbu tu katika kitabu pamoja na amri na sheria mpya alizoendelea kutangaza. Nakala za kitabu hicho zilitumwa katika pande zote za milki yake. Sheria hizo zilimaliza utawala wa machifu waliowahi kuamua mambo kufuatana na hiari zao.

Jeshi la kudumu

hariri

Temujin aliendelea kuanzisha jeshi kwa kutangaza sheria kuwa kila Mmongolia alipaswa kuwa mwanajeshi. Aliweza kuzawadia askari wake kwa mali zilizotekwa vitani. Yeye mwenyewe aliteua viongozi waliosimamia vikosi vya wanajeshi 1,000. Hapo hakuteua tena ndugu zake bali aliwachagua viongozi hao kulingana na uwezo na uaminifu.

Mwenyewe alikuwa na kikosi cha ulinzi wake wa wanajeshi wateule 10,000.

Utawala

hariri

Kazi kubwa ya Temujin ilikuwa kujenga umoja na nidhamu. Wamogolia walizoea kuungana kwa vita lakini kuacha maungano na kufarakana kufuatana na hiari za machifu. Kwa kuunda jeshi la pamoja Temujin alikuwa na chombo cha kuunganisha makabila kwa njia ya kudumu kwa sababu machifu wa kale hawakuwa na nafasi tena katika muundo huo wakapungukiwa umuhimu.

Baada ya kutwaa milki za majirani alipata pia maafisa Wachina hasa waliokuwa na maarifa ya utawala, hivyo aliweza kuanzisha utaratibu wa kodi na huduma.

Mwenyewe hakujua kuandika wala kusoma lakini alielewa umuhimu wa maandiko akaamuru kutungwa kwa mwandiko maalumu kwa ajili ya lugha ya Kimongolia.

Baada ya kuimarisha utawala wake kati ya China na Bahari ya Kaspi alijenga mji mkuu mpya wa Karakorum uliokuwa mji wa kwanza wa kudumu wa Mongolia. Kwa kazi kama utawala, biashara na ufundi alichukua watu kutoka sehemu mbalimbali za milki yake; alitambua ya kwamba Wamongolia wenyewe walizoea ufugaji na vita tu kwa hiyo alitegemea wafanyabiashara Waislamu Waturuki na Waajemi, maafisa wa utawala na mafundi Wachina na wataalamu Wakristo.

Upanuzi

hariri

Baada ya kuunganisha makabila ya wafugaji Temujin aliongoza jeshi lake dhidi ya milki ya China katika kusini. Kuanzia mwaka 1211 alivuka ukuta mkubwa wa China kwa jeshi la askari 100,000. Mwaka 1215 alitwaa Beijing na kuanzia 1219 hata milki ya Korea ilianza kumlipia hongo.

Mwaka 1218 kulitokea matatizo na majirani wa Khorezmu upande wa magharibi; msafara wa Kimongolia uliwahi kushambuliwa na mabalozi waliotumwa huku kupeleleza hali waliuawa. Kwa hiyo Temujin aliitisha mkutano wa viongozi wa milki yake wakaamua kushambulia Khorezmu. Mkutano uleule ulimkubali pia mwana wa tatu Ugedai kama mrithi wa Temujin atakayemfuata kama Khan mkuu.

Miaka 1219/1220 Wamongolia walimshinda mfalme wa Khorezmu wakaangamiza miji ya ufalme huu na kuua watu wengi. Vikosi vya jeshi hilo viliendelea upande wa magharibi na kuangamiza nchi za Warusi na sehemu za Kaukazi.

 
Eneo la Karakorum leo alipojenga Chingis Khan mji mkuu wake

Kifo na urithi

hariri

Mwaka 1227 Chingis Khan alikufa akiwa mzee; wengine husema ya kwamba sababu ya kifo ilikuwa anguko kutoka juu ya farasi; wengine husema ya kwamba binti wa mfalme aliyeuawa na Temujin alilipiza kisasi kwa kumchoma kwa kisu.

Kaburi lake lilifichwa na walinzi wake kufuatana na desturi ya Wamongolia haijajulikana hadi leo. Inasemekana ya kwamba wapandafarasi 1,000 walikanyaga sehemu ya kaburi kwa miguu ya farasi zao halafu waliuawa wenyewe baada ya kuleta taarifa ya kwamba walitimiza kazi ya kumzika Chingis Khan.

Wafuasi wake waliendela kupanua milki. China yote pamoja na Urusi zilikuwa majimbo ya milki ya Wamongolia nayo ilikuwa milki kubwa katika historia ya dunia.

Kwa watu wengi Chingis Khan ni sawa na ushindi katili na wa kinyama. Lakhi za watu waliuawa na wanajeshi wake. Aliposhinda taifa la Watartari aliamuru watu wote wenye urefu juu ya futi nne wauawe yaani watu wazima wote. Wamongolia siku hizi wanamwona kama Baba wa Taifa lao. Alitumia miaka mingi kuunganisha na kueneza makabila ya watu wahamaji wa Mongolia.

Baadhi ya wanahistoria wanasema kwamba alikuwa na kichwa kizuri cha kijeshi kuliko karibu watu wote wengine katika historia ya dunia.

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Chingis Khan kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  NODES
Done 1