Dini asilia za Kiafrika

Dini asilia za Kiafrika ni kati ya dini za jadi ambazo zinadumu hata leo, ingawa wafuasi wake wanapungua mwaka hadi mwaka kulingana na dini zilizotokea Mashariki ya Kati, hasa Ukristo na Uislamu, ambazo zinazidi kuenea Afrika, bara kubwa lenye jamii na tamaduni nyingi.

Vinyago vya Wakongo.

Leo hii Waafrika wengi wamejiunga na dini za Ukristo na Uislamu zinazomtangaza Mungu mmoja. Imani hizo zilikuwepo tangu miaka mingi katika sehemu kadhaa za Afrika lakini katika maeneo mengine Ukristo na Uislamu zilienea tu vizazi vichache vilivyopita zikiendelea hadi leo.

Dini za asili, Ukristo na Uislamu zinaathiriana katika Afrika. Hivyo kuna watu ambao wanafuata imani za jadi au walau sehemu za imani hizo. Kwa hiyo inafaa kupata picha ya imani katika jamii za Waafrika jinsi zilivyokuwa kabla ya kuguswa na Uislamu na Ukristo.

Dini za Kiafrika zinafuata imani maalumu, sawa kabisa na hizo za nje ambazo zimeleta mfumo mpya wa kuabudu. Badala ya kuabudia mapangoni au misituni kama Waafrika walio wengi walivyofanya kwa karne nyingi, zimehimiza kujenga makanisa na misikiti kwa ajili ya kumwabudu Mungu kadiri ya ufunuo wake mwenyewe.

Madhehebu mengi ya Kikristo yamekuwa yakimuabudu Mungu kwa kushirikiana na wafu wanaoheshimiwa kama watakatifu, wakati Waafrika tangu zamani waliwaenzi wazee wao waliokufa na kuwaita mizimu. Waafrika hao tangu zamani waliwaheshimu wafu kwenye makaburi yao, lakini baadhi ya Wakristo waliwaheshimu wafu kanisani kwa sala zao pamoja na kusujudu pengine masalia au picha za hao wafu.

Katika Amri Kumi za Biblia, Waafrika kwa jumla walikuwa nazo hata kabla ya kuja kwa Wazungu: walijua kwamba imewapasa kuwaheshimu wazazi wao, kutoua, kutoiba wala kufanya kinyume na maagizo ya wazee wao.

Kwa mtazamo wa Kikristo, Mungu mwenyewe ndiye aliyewaandaa hivyo Waafrika kupokea wokovu kwa njia ya Yesu Kristo, aliyekuja si kutangua bali kukamilisha yale yote yaliyo mema katika binadamu wote.

Pamoja na hayo yote, bado baadhi ya makabila yanaendelea na mila zao za kuheshimu wafu ingawa dini zenye asili ya Mashariki ya Kati zinakataza namna hiyo.

Mungu na miungu

Jamii hizo zilikuwa na dini zao ambamo tunaweza kuona imani katika nguvu za kiroho ambazo zinaitwa majina tofauti. Tunaweza kukuta imani ya Mungu Mkuu, pia ya miungu mbalimbali, pamoja na imani ya kuwepo kwa roho za wahenga, mizimu na pepo mbalimbali.

Tukijiuliza juu ya uhusiano kati ya mizimu, roho, miungu mbalimbali na Mungu Mkuu, ni lazima kwanza tujue imani za jadi hutofautiana kutoka jamii moja hadi jamii nyingine.

Mara ningi imani za Kiafrika humwona Mungu Mkuu mmoja kuwa wa juu na mwenye nguvu zaidi. Yuko kabla ya kila kitu kingine na asili yake haijulikani. Hivyo nguvu hutazamwa kwa ngazi tofauti; Mwenyezi Mungu yuko juu, chini yake kuna roho mbalimbali au hata miungu pamoja na nguvu za asili, na mwishoni binadamu wasio na nguvu nyingi.

Wakati mwingine hadithi za uumbaji za Kiafrika zinamwonyesha Mungu akiwa au akienda mbali na watu au hawasiliani nao tena moja kwa moja. Anaacha washughulikiwe na roho au miungu midogo aliyoumba pia. Mungu wa aina hiyo anaonekana mbali sana na mambo ya binadamu; kwa sababu hiyo, mara kwa mara miungu midogo huombwa badala yake ili kupata usaidizi. Katika jamii nyingine wanaamini kwamba mizimu inaweza kuleta mawasiliano baina ya Mungu na binadamu.

Vikundi vingine humwona Mungu Mkuu kuwa karibu sawa na miungu mingine, kama mwenyekiti wao au kama mfalme kati ya machifu. Wafon katika Afrika ya Magharibi humwaza Mungu mkuu kama mapacha mawili: Mavu, nguvu ya kike, na Lisa, nguvu ya kiume. Wakitazamwa kama nguvu moja huitwa Mavu pekee. Wameumba watoto ambao hutawala shughuli za dunia na viumbe vyake kama miungu.

Dhana za aina hiyo zimeleta majadiliano kati ya wataalamu kuhusu kuainisha dini za Kiafrika kuwa za Mungu mmoja (monotheistic) au za miungu mingi (polytheistic). Wengine huona uainishaji huo hauna maana kwa dini za Kiafrika.

Mtaalamu John Mbiti wa Kenya aliona kwamba kimsingi imani katika Mungu mmoja inapatikana kwa namna moja au nyingine katika dini zote za asili. Anaeleza nguvu nyingine za kiroho kama tabia au shughuli za Mungu yeye yule zinazotazamwa pekepeke.

  Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  NODES