Historia ya Afghanistan

Historia ya Afghanistan inahusu eneo ambalo leo linaunda Jamhuri ya Afghanistan ila limetekwa kwa kiasi kikubwa na Taliban.

Kabla ya karne ya 19 nchi yote au sehemu mbalimbali zilikuwa sehemu ya milki jirani hata kama sehemu za eneo la Afghanistan zilijitegemea chini ya watawala wadogo. Kwa vipindi virefu vya historia Afghanistan ilikuwa sehemu ya milki za Uajemi (Iran).

Afghanistan kama nchi ya pekee ilianza kutokea katika karne ya 18, watawala wa kieneo walipojiondoa katika himaya ya Uajemi.

Nchi ilifaulu kutunza uhuru wake kutokana na mashindano ya Uingereza na Urusi pamoja na nguvu na ukali wa wapiganaji kutoka makabila yake. Watawala wa kwanza waliofaulu kuunganisha sehemu nyingi za nchi chini ya mamlaka yao walitawala kama Emir, na tangu mwaka 1926 kwa cheo cha mfalme.

Mfalme Zahir Shah alipinduliwa mwaka 1973 na nchi ikawa Jamhuri. Mnamo 1978 wanajeshi Wakomunisti walipindua serikali na kutangaza serikali ya kisoshalisti iliyoanzisha mabadiliko mengi katika jamii kama ugawaji mpya wa mashamba, shule zilizounganisha wasichana na wavulana na kukamatwa kwa viongozi wa dini waliopinga maazimio ya serikali. Mabadiliko hayo yalileta upinzani kutoka wanamgambo waliopigana na jeshi la serikali.

Mnamo Disemba 1979 Umoja wa Kisovyeti iliamua kuingilia kati ikavamia nchi kwa shabaha ya kuokoa utawala wa Wakomunisti, lakini ukapaswa kujiondoa tena mwaka 1989.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilifuata kati ya vikundi vya wapinzani ambako nchi jirani ya Pakistan ilikuwa na athira kubwa kwa kutuma silaha na pesa. Nchi ilikuwa tena na kipindi kifupi cha serikali ya kitaifa, lakini vita vya wenyewe kwa wenyewe viliendelea katika sehemu za nchi.

Mateso ya vita hivyo yalihamasisha walimu na wanafunzi wa madrasa (shule za Kiislamu) kuchukua silaha dhidi ya migambo mbalimbali na kuwashinda wakijulikana kwa jina la Taliban (jina linamaanisha wanafunzi wa madrasa). Taliban walifaulu kuteka Kabul kwa msaada kutoka Saudia na Pakistan mwaka 1996. Walitangaza Emirati ya Kiislamu ya Afghanistan wakanzisha utawala uliotumia mafundisho makali ya sharia ya Kiislamu. Utawala wao ulikuwa maarufu kwa kuzuia wanawake wasishiriki katika maisha ya hadharani, kuwalazimisha kuvaa burka, kufunga shule za wasichana, kukataza kazi kwa wanawake nje ya nyumba zao tena matumizi ya adhabu kali kama kukata mkono wa mwizi na kumwua mzinzi kwa kumpiga mawe.

Serikali ya Taliban ilikwisha kwa sababu walimruhusu Osama bin Laden pamoja na kundi lake la Al-Qaida kuwa na kimbilio nchini. Baada ya Shambulio la 11 Septemba 2001 Marekani ililipa kisasi kwa kushambulia Afghanistan.

Hali ya vita iliendelea ndani ya Afghanistan katika vita vya Marekani na NATO 2001-2014. Tangu Disemba 2014 nchi za NATO zilitangaza ya kwamba wamemaliza kushiriki mapigano na kuondoa sehemu kubwa ya wanajeshi kutoka Afghanistan. Vikosi vya NATO vimebakizwa kwa shabaha ya kusaidia jeshi la kitaifa.

Mnamo mwaka 2020 Marekani ilipatana na Taliban kwamba Marekani ingeondoa askari wote kutoka Afghanistan katika mwaka 2021. Taliban waliahidi kutoshambulia wanajeshi wa Marekani lakini waliongeza mashambulio yao dhidi ya jeshi la serikali.

Baada ya kuondoka kwa wanajeshi wa NATO na idadi kubwa ya Wamarekani, Taliban walianza kuvamia maeneo mengi ilhali nguvu ya jeshi la kitaifa liliporomoka. Mnamo 15 Agosti 2021, rais wa Afghanistan aliondoka nchini na Taliban waliteka tena Kabul.

Baada ya kutwaa Kabul, wasemaji wa Taliban walitangaza kwamba wanataka kufuata siasa tofauti kiasi na ile ya zamani. Wasemaji walidai kwamba wataruhusu wanawake kufanya kazi na wasichana kusoma, kama wanakubali kuvaa hijabu. Walitangaza pia kwamba watasamehe wananchi wote waliowahi kupigana nao. Hata hivyo, Waafghanistan wengi walijaribu kukimbia nchi kwa njia mbalimbali.

Mwisho wa Agosti 2021, Taliban walidhibiti nchi yote isipokuwa jimbo la Panjir, ambapo wapinzani walijipanga chini ya makamu wa rais aliyejitangaza kuwa rais kufuatana na katiba ya jamhuri.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Afghanistan kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  NODES
os 8