Idd el Hajj (pia: Idi el haji, eid el hajj) ni sikukuu ya Uislamu wakati wa mwezi wa Dhul Hijjah ambao ni mwezi wa Hajj. Sherehe hii inatunza kumbukumbu ya sadaka ya Ibrahimu.

Malaika Jibril ashika mkono wa Ibrahimu kabla hajamchinja mwanawe
(uchoraji wa Kiosmani karne ya 16/17)

Majina ya sikukuu

Kati ya Waislamu duniani sikukuu hii hujulikana kwa majina mbalimbali ambayo hutafsiriwa pia kwa lugha mbalimbali kama vile:

  • Idd-al-Adhha (kwa Kiarabu: عيد الأضح) yaani sikukuu ya sadaka
  • Idd-al-Qorban (kwa Kiarabu: عید قربان) sikukuu ya sadaka (kwa kutumia neno tofauti ya "sadaka" katika Qurani); kwa Kituruki: Kurban Bayramı; kwa Kikurdi "Cejna Kûrbanê";
  • Idd-al-Kabir (kwa Kiarabu: عيد الكبير) au "sikukuu kubwa"; "Bari Eid" huko Uhindi na Pakistan; jina hili hutumiwa kwa sababu kati ya sikukuu mbili zinazoamriwa katika Qurani hii ni sikukuu kubwa zaidi.

Sadaka ya Ibrahimu

Idd husheherekewa kama kumbukumbu ya sadaka ya Ibrahimu (Abrahamu) ambaye kufuatana na taarifa za Biblia na za Qurani alikuwa tayari kumchinja mwanawe kama sadaka kwa Mungu. Lakini Mungu alimzuia asimchinje akampatia kondoo badala yake. Habari zake kati Qurani ziko sura al-Hajj aya 37, katika Biblia Mwanzo 22.

 
Nyama ya sadaka ya Idd-al-Hajj hugawiwa kwa maskini nchini Pakistan

Katika mapokeo ya Biblia huyu mwana alikuwa Isaka. Qurani haitaji jina lake lakini Waislamu walio wengi huamini aliyemaanishwa ni Ismaeli, mwana wa Ibrahimu na Hagar.

Ibada zake

Sherehe huanza na sala ya idd katika msikiti. Mara nyingi hufuatwa na baraza au mkutano wa Waislamu. Katika nchi nyingi huwa na kawaida ya kutembelea pia makaburi ya marehemu.

Kila Mwislamu mwenye uwezo hupaswa kumchinja mnyama wa sadaka siku hiyo, mara nyingi kondoo, lakini kuna pia sadaka za mbuzi, ng'ombe au ngamia kufuatana na uwezo na kawaida ya nchi.

Sehemu ya nyama ya sadaka hizo hugawiwa kwa maskini wasio na uwezo. Nyingine hutumiwa kwa karamu ya familia.

Tarehe za Idd

Idd husheherekewa kati ya tarehe 10 hadi 13 ya mwezi wa Dhul Hijjah wa kalenda ya Kiislamu. Tarehe hali halisi hutegemea kuonekana kwa hilali au mwezi mwandamo. Hapa hutokea tofauti za kila mwaka kati ya Waislamu. Kimsingi mapokeo ya Kiislamu hudai mwezi kuonekana kwa macho.

Tofauti za makadirio kati ya Waislamu

Sehemu za Waislamu hukubali ya kwamba inawezekana kukadiria tarehe hii kisayansi, lakini huko Saudia husisitizwa kuona kwa macho. Maadamu Saudia ni mahali pa miji mitakatifu ya Maka na [Madina]], Waislamu wengine hupenda kufuata kawaida ya kule.

Zamani hapakuwa na tatizo sana kwa sababu kila nchi ilikuwa na azimio lake. Mitambo ya kisasa huonyesha siku hizi kama Waislamu wameshaanza kusheherekea nchi moja lakini nchi nyingine bado. Katika nchi mbalimbali, hasa kule ambako Waislamu walihamia juzi tu kama Ulaya, kuna tarehe tofauti kandokando kama wengine hufuata matangazo ya Uturuki yanayokadiriwa kisayansi na wengine matangazo ya Saudia yanayofuata kuonekana kwa macho. Matangazo ya Saudia yamepingwa mara nyingi kwa sababu tarehe zilitangazwa ambapo hapakuwa na uwezekano kuona hilali kisayansi.

Kubadilika kwa tarehe katika kalenda ya jua

Katika kalenda ya Gregori, ambayo ni kalenda ya kawaida, tarehe za Kiislamu hubadilika kila mara kwa sababu mwaka wa Kiislamu hufuata kalenda ya mwezi lakini kalenda ya kawaida hufuata jua. Kalenda ya Kiislamu ina takriban siku 11 pungufu kuliko kalenda ya jua. Kila mwaka tarehe ya Idd huweza kutokea kwa siku mbili tofauti za kalenda ya Gregori kwa sababu kawaida ya Uislamu hufuata kuonekana kwa mwezi kunakopatikana tofauti duniani.

Orodha inyaofuata yaonyesha tarehe rasmi za Idd-al-Hajj kwa nchi ya Saudia jinsi ilivyotangazwa hadi 2007 na halmashauri kuu ya Majlis al-Qadā’ al-A‘lā . Tarehe za miaka 2008 na kuendelea ni tarehe zinazokadiriwa kulingana na kalenda ya Kiislamu jinsi ilivyo kawaida katika nchi kama Uturuki. Tofauti zitaendelea kutokea kulingana na maelezo hapo juu kuhusu tofauti ya makadirio na kuonekana kwa hilali

Viungo vya nje

  NODES
Done 1