Kiazeri (pia: Kiazerbaijani, Kituruki cha Azerbaijani, kwa lugha ya wenyewe: Azərbaycanca, Azərbaycan dili, آذربایجان تورکجه‌سی) ni moja ya lugha za Kiturki ambayo ni karibu na Kituruki chenyewe. Wengine hutofautisha lugha mbili za Kiazeri, yaani Kiazeri-Kaskazini nchini Azerbaijani inayoandikwa kwa alfabeti ya Kilatini, na Kiazeri-Kusini nchini Uajemi inayoandikwa kwa alfabeti ya Kiarabu (angalia hapo chini).

Maeneo yenye wasemaji wa Kiazeri.

Maeneo lugha inapotumiwa

Lugha inatumiwa katika jamhuri ya Azerbaijan na katika sehemu za magharibi-kaskazini za Uajemi, pamoja na sehemu za Georgia, Uturuki na Urusi. Idadi ya wasemaji ni takriban milioni 30.

Historia ya lugha ya Kiazeri

Chanzo cha lugha kiko katika lahaja za Kituruki cha magharibi zilizotumiwa na wahamiaji Waturuki waliofika Asia ya Magharibi tangu karne ya 10. Waturuki Waosmani walioteka Konstantinopoli waliendeleza lugha yao kama Kitiruki cha Kiosmani kilichokuwa baadaye msingi wa Kituruki cha leo.

Lugha ya makabila ya Anatolia mashariki na Uajemi magharibi imeendelea kuwa asili ya Kiazeri. Wasemaji wa Kiazeri walitawala Uajemi tangu mwaka 1500 kwa nasaba ya Wasafawi. Hii ni sababu ya kwamba Kiazeri kilipokea maneno mengi kutoka lugha ya Kiajemi na Kiarabu.

Tangu mwaka 1800 Urusi uliteka eneo la Kaukazi na hivyo wasemaji wa Kiazeri waliishi sasa kwa sehemu katika Dola la Urusi na kwa sehemu katika milki ya Uajemi. Kiazeri-Kaskazini kilipokea maneno mmengi kutoka Kirusi.

Baada ya Mapinduzi ya Urusi ya 1917 Azerbaijan ya Kirusi iliendelea kama Jamhuri ya Kisovyeti ya Kijamii ya Kiazeri ambako Kiazeri kilifanywa lugha ya taifa na kukuzwa kama lugha ya kisasa. Hapo maandishi ulibadilishwa kwa kutumia alfabeti ya Kisirili.

Baada ya uhuru wa Azerbaijan mwaka 1991 serikali ilibadilisha mwandiko kuwa herufi za Kilatini kama vile huko Uturuki.

Lakini Kiazeri kinaendelea kuandikwa kwa herufi za Kiarabu nchini Uajemi.

Mifano ya maandishi ya Kiazeri kwa alfabeti tofauti

Yafuatayo ni kifungu cha kwanza katika Azimio la ulimwengu juu ya haki za binadamu kwa lugha ya Kiazeri lakini kwa maandishi tofauti "Watu wote wamezaliwa huru, hadhi na haki zao ni sawa. Wote wamejaliwa akili na dhamiri, hivyo yapasa watendeane kindugu."

Alfabeti ya Kisirili kwa Kiazeri (hadi 1991)

Бүтүн йнсанлар ләјагәт вә һүгуларына ҝөрә азад вә бәрабәр доғулурлар. Онлрын шүурлары вә виҹданлары вар вә бир-бирләринә мүнасибәтдә гардашлыг рунһунда давранмалыдырлар.

Alfabeti ya Kilatini/Kituruki kwa Kiazeri (tangu 1992)

Bütün insanlar ləyaqət və hüquqlarına göre azad və bərabər doğulurlar. Onların şüurları və vicdanları var və bir-birlərinə münasibətdə qardaşlıq ruhunda davranmalıdırlar.

Alfabeti ya Kiarabu jinsi ilivyo kawaida katika Iran

‏بوتون انسانلار حيثيت و حقلر باخميندان دنك (برابر) و اركين (آزاد) دوغولارلار. اوس (عقل) و اويات (وجدان) ييهﺳﻴﺪيرلر و بير بيرلرينه قارشى قارداشليق روحو ايله داورانماليدرلار‎.

(kwa herufi za Kilatini): Bütün insanlar heysiyyət və haqlar baxımından dənk (bərabər) və ərkin (azad) doğularlar. Us (əql) və uyat (vicdan) yiyəsidirlər və bir birlərinə qarşı qardaşlıq ruhu ilə davranmalıdırlar.

Matini ileile kwa Kituruki kwa ulinganifu

Bütün insanlar hür, haysiyet, ve haklar bakımından eşit doğarlar. Akıl ve vicdana sahiptirler ve birbirlerine karşı kardeşlik zihniyeti ile hareket etmelidirler.

Viungo vya nje

  Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kiazeri kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  NODES