Kwa watu wengine wenye jina la Koreshi, Cyrus, Kyros tazama Koreshi

Kaburi la Koreshi Mkuu huko Pasargadae

Koreshi Mkuu (kwa Kiajemi کوروش بزرگ kurosh-e bozorg, kwa Kilatini Cyrus, ~ 590 KK au 576 KK — Agosti 530 KK), pia Koreshi II wa Uajemi alikuwa mwanzilishi wa nasaba ya Akhameni katika Uajemi ya Kale.

Aliunganisha kwanza maeneo ya nyanda za juu za Uajemi, akaendelea kutwaa mamlaka juu ya madola yote yaliyokuwepo katika Asia Magharibi, akatawala milki kubwa kuanzia pwani za Ugiriki katika Ulaya hadi mto Indus katika Uhindi na Yerusalemu upande wa kusini.

Vyanzo

hariri

Habari za Koreshi II zinapatikana katika maandishi ya Wagiriki wa Kale, hasa Herodoti, katika maandishi kwenye majengo yaliyoagizwa na Koreshi na wafuasi wake, katika bao za mwandiko wa kikabari kutoka Babeli na katika taarifa za vitabu vya Biblia kama Isaya, Kitabu cha Ezra, Mambo ya Nyakati II na Danieli.

Habari hizo zinaonyesha tofauti fulanifulani, lakini wataalamu wa historia bado wanapata picha ya maisha na mafanikio yake kwa kulinganisha taarifa mbalimbali.

Familia

hariri

Nasaba ya Akhameni ilianzishwa na Mwajemi Akhameni aliyekuwa mtawala wa eneo dogo la Uajemi kusini magharibi (ingawa wakati ule hakukuwa na "Uajemi" bado); sehemu kubwa ya nchi ilitawaliwa na Wamedi waliokuwa kabila la Uajemi ya magharibi.

Mwanawe Teispes alipanua eneo hilo hadi kushika Pars ambayo ni kiini cha Uajemi wenyewe.

Mwanawe Koreshi I akafuatwa na Kambisi I aliyekuwa baba wa Koreshi II anayejulikana kama Koreshi Mkuu.

Hadi hapo watawala hao walisimamia maeneo madogo wakipaswa kutii mabwana wao hasa Wamedi.

Koreshi Mkuu alimuasi bwana wake na kutwaa utawala wa milki ya Umedi akaendelea kutwaa nchi jirani.

Taarifa ya Herodoti juu ya kuzaliwa na maisha yake

hariri

Mwanahistoria Mgiriki Herodoti anasimulia ya kwamba wazazi wa Koreshi walikuwa Kambisi I na Mandane, binti wa mfalme Astyages wa Umedi. Baadaye mfalme Astyages alikuwa na ndoto iliyomwambia mjukuu wake atakuwa hatari kwake. Kwa hiyo alimtuma jenerali yake Harpagus kumwua mtoto wa binti yake na huyu mtoto alikuwa Koreshi. Lakini jenerali Harpagus hakutaka kumwaga damu ya kifalme akamtwaa mtoto na kumpa mchungaji mmoja wa kondoo aliyemzaa wakati huohuo mtoto aliyekufa mara moja. Mchungaji alimpokea Koreshi akamlea na Hapagus alimwonyesha mfalme maiti ya mtoto mchanga.

Koreshi alipofikia umri wa miaka 10 alitambuliwa kama mtoto wa kifalme. Astyages aliamua kumhurumia sasa, akamtuma kwa wazazi wake. Lakini jenerali Harpagus aliadhibiwa vikali kwa sababu alimwalika kwa chakula katika ikulu lake na kwa siri aliamuru kumwua mtoto wake Harpagus, kumpika, kumkatakata na kumweka mezani ili Harpagus ale. Hivyo jenerali alikuwa adui wa mfalme.

Mwaka 559 KK Koreshi alimfuata babake kama mtawala wa kieneo. Harpagus aliwasiliana naye na kumchochea hadi Koreshi aliasi dhidi ya mfalme Astyages mwaka 553 KK. Baada ya vita vya miaka 3 mfalme alishindwa 550 KK, Koreshi akawa mfalme wa Umedi na Uajemi.

Koreshi alioa mke kwa jina Kassandane aliyetoka katika kabila lake. Walizaa watoto wanne, kati yao Kambisi II aliyemfuata baba baadaye na binti Atossa aliyekuwa mama wa mjukuu wake Xerxes I. Kassandane alipokufa mapema Koreshi alionyesha huzuni kubwa sana. Kufuatana na taarifa kadhaa alioa baadaye mke kutoka kwa Wamedi.

 
Milki ya Umedi kabla ya kutwaliwa na Koreshi Mkuu

Mfalme wa Uajemi na Umedi

hariri

Wataalamu wa historia wanatofautiana kuhusu taarifa ya Herodoti katika vipengele mbalimbali. Lakini picha inakubaliwa kuwa anguko la mfalme Astyages wa Umedi lilisababishwa na uasi wa sehemu za jeshi lake -labda chini ya Harpagus- pamoja na uasi wa Waajemi walioongozwa na Koreshi.

Baada ya ushindi wake Koreshi alipokea pia cheo cha kifalme cha Umedi lakini rasmi alijiita "mfalme wa Waajemi". Kutokana na mamlaka yake mpya aliweza kudai pia kipaumbele kati ya viongozi wengine katika Uajemi.

Mjomba wake Arsames aliyekuwa mfalme wa mji wa Parsa chini ya Wamedi akawa gavana wa Parsa chini ya Koreshi.

Koreshi aliendelea kutumia Ekbatana, mji mkuu wa Wamedi, kama makao makuu wakati wa miezi ya joto. Kwa majira ya baridi alijenga mji mkuu mpya Pasargadi katika Pars.

Akitumia cheo cha "Mfalme wa Uajemi na Medi" akaendelea kudai utii kutoka wakubwa wote Wamedi.

Upanuzi hadi Lydia

hariri

Lydia ilikuwa milki katika magharibi ya Anatolia iliyokuwa maarufu wakati ule kutokana na utajiri wa mfalme wake Kroiso. Kroiso alikuwa alishiriki na Wamedi dada yake Aryenis alikuwa mke wa mfalme Astyages wa Umedi.

Tangu mwaka 550 KK Kroiso alikuwa na jirani mpya Uajemi. Kufuatana na taarifa ya Herodoti aliona milki ya Koreshi kama tishio.

Alitaka kulipiza kisasi kwa anguko la shemeji wake Astyages, akaona pia nafasi ya kupanua milki yake kwenye maeneo ya Uajemi. Kroiso aliuliza mizimu ya Delfi kuhusu mipango yake. Hapo alipata jibu maarufu "Ukivuka Halys, mto wa mpakani, utaharibu milki kubwa" - kumbe aliona baadaye ya kwamba milki iliyoharibiwa ilikuwa milki yake mwenyewe.

Kabla ya kuondoka vitani alipatana pia na majirani, hasa Sparta katika Ugiriki, Farao Amasis II wa Misri na mfalme Nabonidi wa Babeli. Pamoja na jeshi lake Kroiso alivuka mto Halys mwaka 542 KK akavamia eneo la Koreshi na kutwaa mji wa Pteria; wakazi wote waliuzwa kama watumwa. Sasa alisubiri jeshi la Koreshi.

Waajemi walikaribia mji wa Pteria na kulitokea mapigano makali yasiyokuwa na mshindi. Waajemi walirudi nyuma kidogo na Kroiso hakutegemea tena mapigano kabla ya majira ya baridi hivyo aliagiza wanajeshi warudi kwao kwa majira ya baridi na mwenyewe alielekea mji mkuu wake Sardes. Alipanga kuendelea na vita baada ya miezi ya baridi akatuma nyaraka kwa wafalme walioshirikiana naye wawe tayari baada ya miezi hiyo.

Lakini Koreshi alipeleka jeshi lake haraka hadi Sardes, mji mkuu wa Kroiso. Kroiso alituma vikosi vikubwa vya askari farasi dhidi ya Waajemi. Koreshi aliyekosa askari farasi bora alikuwa ameandaa kikosi cha askari ngamia. Hapa alifuata ushauri wa jenerali Harpagus aliyejua ya kwamba farasi hawapendi harufu ya ngamia, na kweli mashambulio ya askari farasi wa Lydia yalishindikana. Waajemi walizunguka mji mkuu wakaushambulia wiki 2 na mwishowe kuuteka 541 KK.

Taarifa zinatofautiana kama mfalme Kroiso alikufa, aliuawa au kuhurumiwa wakati Waajemi walipoteka mji wake.

Hata hivyo milki ya Koreshi iliendelea sasa hadi pwani za Ugiriki pamoja na miji ya Wagiriki upande wa Anatolia ndani ya milki yake.

Uvamizi wa Babeli

hariri

Mfalme wa Babeli alikuwa alishirikiana na adui wa Koreshi na mfalme wa wafalme hakusita muda mrefu kumshambulia. Mwaka 540 KK alivamia eneo la Elamu mpakani kwa Babeli.

Koreshi alitumia nafasi ya kwamba sehemu za watu na viongozi wa Babeli hawakuridhika na utawala wa Nabonidi kwa sababu ya mabadiliko katika utaratibu wa ibada, akawasiliana nao na kuwaahidia hali nafuu baada ya kupinduliwa kwa mfalme wao. Nabonidi alitaka kuimarisha msimamo wa watu wake akaanza kukusanya sanamu za miungu muhimu kutoka miji ya milki yake zikapelekwa Babeli.

Mwaka 539 KK vita viliingia katika Mesopotamia yenyewe. Jeshi la Babeli lilishindwa kwenye mapigano ya Opis iliyopo kando ya mto Hedekeli takriban 160 km kaskazini kwa Babeli; vikosi vya Waajemi walifika siku mbili baadaye mjini Babeli wakaingia bila upinzani na kumkamata mfalme Nabonidi. Tarehe 23 Oktoba Koreshi aliingia Babeli kama mshindi akapokea cheo cha mfalme wa Babeli.

Mwaka uliofuata alimpa mwanawe Kambisi cheo cha mfalme wa Babeli na Koreshi mwenyewe alijiita "Mfalme wa wafalme".

Mara baada ya kushika utawala Koreshi alithibitisha ibada ya mungu Marduk kuwa mungu mkuu wa Babeli; majaribio ya Nabonidi ya kubadilisha ibada hii na kumweka mungu mwingine kwenye nafasi ya kwanza yalikuwa sababu muhimu ya watu wake kutoridhika naye.

Tarehe 21 Machi 538 KK Koreshi alifika mbele ya sanamu ya Marduk katika hekalu kuu akashika mikono ya sanamu na hivyo kupokelewa kama mfalme wa Babeli.

Aliendelea kuthebitisha viongozi wengi na wakuu wa idara mbalimbali waliowahi kuwepo chini ya mfalme wa kale.

 
Upanuzi wa Milki ya Uajemi wakati wa kifo cha Koreshi (njano juu ya mipaka ya kisasa)

,

Uenezaji upande wa mashariki

hariri

Baada ya ushindi juu ya Babeli Koreshi alitawala Asia Ndogo, Mesopotamia na Shamu hadi Palestina mpakani kwa Misri. Hapo aliangalia mipaka yake upande wa mashariki.

Uajemi inapakana mashariki na nchi za Asia ya Kati zilizokaliwa na makabila ya wahamiaji pamoja na wakazi wa oasisi penye miji au makabila makali ya milimani. Wengi wao walitumia lugha za karibu na Kiajemi. Wahamiaji hao walikuwa hatari kwa milki za nyanda za juu za Uajemi wakati ule na pia kwa milenia baadaye kwa sababu waliondoka mara kwa mara katika maisha magumu ya mapori yao kutafuta utajiri wa milki za nyanda za juu. Koreshi alijaribu kupanua mamlaka yake upande wao kwa kusudi la kuwanyamazisha na kusimamisha mashambulio na uporaji wao katika majimbo ya mpakani.

Mwaka 538 KK alivamia Baktria (Kaskazini mwa Afghanistan ya leo) na kuifanya jimbo la milki yake, akaendelea kuvamia pia Sogdia na Khorezmia. Kupitia Afghanistan ya leo alivuka pia njia ya Khyber hadi bonde la Indus.

Ilhali aliweza kuunganisha sehemu ya maeneo haya na milki yake alishindwa kutawala wahamisahi wa tambarare za kaskazini mashariki. Katika mapigano katika maeneo yale aliuawa vitani mwaka 530 KK. Kaburi lake linaonyeshwa huko Pasargadi.

Katika utawala alifuatwa na mwanawe Kambisi II.

 
Silinda ya Koreishi, tangazo lake baada ya kutwaa Babeli

Siasa ya kidini

hariri

Baada ya kueneza milki yake Koreshi alitawala watu wenye lugha na dini mbalimbali. Wakati wa kutwaa Babeli aliona ya kwamba mfalme adui wake Nabonidi alijitengenezea upinzani kati ya watu wake kutokana na kupuuza ibada ya Marduk, mungu wa Babeli.

Hivyo kushughulikia dini mbalimbali za watu chini yake kulikuwa sehemu muhimu ya siasa yake.

Katika amri ya Koreshi jinsi ilivyoripotiwa katika Kitabu cha Ezra Mungu wa Israeli anaitwa "Bwana, Mungu wa mbingu" aliyempa mfalme huyu falme zote za dunia. Kwa Wayahudi hii ilikuwa kama tamko la imani kwa Mungu wao, hivyo walimsifu Koreshi sana.

Kwa lugha ya kufanana Koreshi alitoa pia sifa za Marduk mbele ya watu wa Babeli: katika tangazo lake baada ya kutwaa Babeli aliandika ya kwamba Marduk alimteua kuwa mfalme juu ya yote na kumbariki kila siku. [1]

Katika tangazo hili Koreshi alijivunia pia kuwa alirudisha sanamu zote za miungu kutoka ufalme wa Babeli zilizokusanywa na Nabonidi katika mji wa Babeli kwenda miji yao ya asili.

Siasa hii katika mambo ya kidini hutazamiwa kama azimio lenye hekima kwa kuonyesha stahamala kwa dini na tamaduni mbalimbali.

Koreshi na Wayahudi

hariri

Alipovamia Babeli Koreshi alikuta pia jumuiya ya Wayahudi waliopelekwa huko baada ya Yerusalemu kutekwa na mfalme Nebukadreza II wa Babeli mwaka 587 KK. Josephus anatoa taarifa ya kwamba katika miaka yake ya kwanza alifahamiana pia na viongozi Wayahudi. Hatuna taarifa kamili lakini katika mwaka wa tatu baada ya kuteka Babeli Koreshi alitoa amri inayoripotiwa katika kitabu cha Ezra:

"Katika mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi, mfalme Koreshi alitoa amri, 'Kwa habari ya nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, nyumba hiyo na ijengwe, mahali watoapo dhabihu, na misingi yake ipigwe na kufanywa imara sana; kuinuka kwake kuwe mikono sitini, na upana wake mikono sitini; ziwepo safu tatu za mawe makubwa, na safu moja ya miti mipya; gharama zake zitolewe katika nyumba ya mfalme. Na vyombo vya dhahabu na fedha, vya nyumba ya Mungu, ambavyo mfalme Nebukadreza alivitoa katika nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu, akavileta mpaka Babeli, na virudishwe, vikaingizwe tena katika hekalu lililoko Yerusalemu, kila kimoja mahali pake, na wewe uvitie katika nyumba ya Mungu'."

Kutokana na amri hii sehemu ya Wayahudi walirudi Yerusalemu ambako mababu wao walifukuzwa zaidi ya miaka 40 iliyopita wakajenga upya hekalu lakini wengine walibaki na kuwa chanzo cha jumuiya muhimu ya Wayahudi wa Mesopotamia na Uajemi.

Kutokana na siasa hii Wayahudi walimheshimu na kumsifu Koreshi kushinda watawala wengine nje ya taifa lao. Koreshi ni mfalme wa mataifa wa pekee anayeitwa na Biblia "Masiya" [2]

Marejeo

hariri
  1. "(Marduk) took under his hand Cyrus, king of the city of Anshan, and called him by his name, proclaiming him aloud for the kingship over all of everything…. Marduk, the great lord, bestowed on me as my destiny the great magnanimity of one who loves Babylon, and I every day sought him out in awe. … Marduk, the great lord, rejoiced at [my good] deeds, and he pronounced a sweet blessing over me, Cyrus, the king who fears him" tafsiri kutoka The Cyrus Cylinder - The Bristish Museum homepage
  2. "Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi wake" Isaya 45,1
  NODES
HOME 1
iOS 1
mac 1
os 11