Posta ni mfumo wa kusafirisha barua na vifurushi kwa wapokeaji. Kuna makubaliano ya kimataifa ya Umoja wa Posta Duniani (Universal Postal Union) yanayounda kanuni za aina, ukubwa na uzito wa barua na vifurushi vinavyopokelewa.

Stempu ya posta ya Kenya, Uganda na Tanganyika mnamo mwaka 1954.

Posta ya Serikali na huduma za binafsi

hariri

Katika nchi nyingi huduma ya posta ni taasisi ya kiserikali; katika miaka ya nyuma shirika za binafsi ziliruhusiwa kushiriki lakini mara nyingi kwa masharti yaliyowekwa na serikali.

Katika mfumo wa posta kila huduma ina bei yake inayotangazwa kutegemeana na ukubwa au uzito wa barua au kifurushi, pia kutegemeana na kasi ya kufikisha ujumbe au mzigo.

Kama huduma ya posta inaendeshwa na serikali inakuja na ahadi ya kufikisha barua kila mahali katika nchi. Huduma za binafsi mara nyingi zinafikisha tu mahali ambako zina ofisi zao.

 
Sanduku la kuwekea barua nchini Ufaransa.

Huduma hadi nyumbani au sanduku la Posta

hariri

Katika nchi nyingi barua na vifurushi vinapelekwa hadi nyumba ya mpokeaji au anwani inayotajwa. Katika nchi nyingine barua zinapelekwa tu hadi ofisi ya posta na kuwekwa pale katika sanduku la posta yenye namba fulani.

Ofisi za posta huwa mara nyingi na sanduku la kutupia barua zilizotiwa stempu tayari ili watumiaji waweze kutuma barua kila wakati. Masanduku hayo hufunguliwa kwa utaratibu maalumu kwenye saa zilizotajwa na barua zinapelekwa njia. Masanduku ya aina hii yapo pia mahali pengine pa nchi nyingi.

Historia

hariri

Katika historia zilikuwa nchi chache tu zilizoweza kuunda huduma ya posta; pasipo huduma ya aina hii watu walihitaji kutafuta wasafiri walioweza kubeba barua au kama walikuwa matajiri kumtuma mtumishi wa kubeba barua yao. Milki kubwa kama Uajemi ya Kale, China ya kale na Roma ya Kale zilianzisha huduma za posta ambazo watumishi wa mtawala walikaa katika vituo vyenye umbali wa safari ya siku moja, kupokea barua na kuzipeleka kwa kupanda farasi hadi kituo kilichofuata. Wakati wa mvurugo au kudhoofika kwa serikali huduma hizo zilipotea tena.

Katika karne ya 19 mawasiliano kati ya nchi za Ulaya yaliongezeka kiasi cha kuonyesha haja ya kuboresha mawasiliano hayo. Tangu kipindi kile taratibu kama matumizi ya stempu kama ushahidi wa kuwa barua imeshalipiwa gharama zake na bahasha sanifu pamoja na maumbo ya anwani zilikubaliwa na kusambaa kote duniani.

Marejeo

hariri
  NODES