Sanamu ya Kolossos kisiwani Rhodos

Sanamu ya Kolossos kwenye kisiwa cha Rhodos ilikuwa kati ya maajabu saba ya dunia ya kale.

Picha ioneshayo jinsi gani watu wa baadaye waliwaza Kolossos; hali halisi hakusimama juu ya mlango wa bandari lakini kando lake

Kolossos ilikuwa mnara wa taa mwenye umbo la sanamu ya mtu aliyesimama kwenye mlango wa bandari na kushika moto kama mwenge. Kazi ya sanamu ilikuwa kuelekeza meli bandarini wakati wa usiku. Sanamu ilimwonyesha mungu wa jua Helios.

Ilijengwa kwa muda wa miaka 12 ikakamilishwa mnamo 300 KK na kuwa na kimo cha zaidi ya mita 30. Ilikuwa sanamu kubwa kabisa ya dunia ya kale. Kumbukumbu zimehifadhiwa kuwa matumizi ya vifaa yalikuwa pamoja na tani 13 za bronzi na tani 8 za chuma zilizofunika nguzo za matofari na mawe zilizokuwa majenzi ya ndani.

Sanamu ilisimama miaka 60-70 tu ikaanguka wakati wa tetemeko la ardhi mnamo 226 KK. Ikakatika kwenye magoti. Mabaki yalikaa palepale kwa sababu watu wa Rhodos waliogopa hasira ya mungu Helios wakisimamisha kitu kilichoangushwa na miungu.

Kwa miaka karibu 900 watalii wa dunia ya kale walishangaa mabaki makubwa.

Mwaka 654 Rhodos ilivamiwa na Waarabu Waislamu na Muawiya (wakati ule bado gavana wa Shamu bado khalifa) aliuza metali kwa mfanyabiashara. Inasemekana ya kwamba ngamia 900 walihitajika kubeba mzigo.

  NODES
Done 1