Unajimu

imani ya dini na unajimu

Unajimu (wakati mwingine pia: astrolojia kutoka Kiingereza: "astrology") ni mafundisho yasiyo ya kisayansi juu ya uhusiano kati ya nyota na maisha hapa duniani. Wafuasi wa unajimu hufundisha ya kwamba nyota zinaathiri maisha ya watu na matukio duniani kama amani, vita au maafa. Hapa huangalia hasa makundinyota yaliyopo kwenye mzingo wa zodiaki ambazo ziliitwa "Buruji za Falaki" katika utamaduni wa Waswahili. Siku hizi wanajimu huziita zaidi "alama za nyota".

Mwindaji Orion: watu waliwaza ya kwamba nyota kadhaa zinazoonekana kwa pamoja angani ni picha ya mungu fulani au nguvu muhimu katika ulimwengu, hata kama nyota hizi hali halisi hazina uhusiano kati yao.

Kuna aina nyingi za unajimu:

  • wengine wanataka kugundua mwendo wa dunia na utabiri wa mambo yajayo kutokana na nyota
  • wengine wanaamini ya kwamba tabia za mwanadamu zinatokana na hali ya nyota wakati wa kuzaliwa kwake
  • wengine wanaona nyota kama alama za miungu au nguvu za mbinguni.

Tofauti ya unajimu na astronomia

Unajimu na astronomia zilianza pamoja kama kazi ileile ya kutazama na kuelewa nyota zikaendelea pamoja kwa karne nyingi. Tangu mwanzo wa sayansi ya kisasa takriban miaka 500 iliyopita wataalamu walitambua tabia za nyota kuwa magimba ya angani yenye sifa za kifizikia si pepo, roho au miungu wanaoweza kutawala dunia au wanadamu. Kwa hiyo njia za unajimu (astrolojia) na astronomia zimeachana tangu karne kadhaa. Lakini miaka 400 iliyopita wanasayansi muhimu kama Tycho Brahe, Johannes Kepler, Giordano Bruno au Galileo Galilei walitengeneza horoskopi, ingawa waliweka misingi ya astronomia ya kisasa.

 
Uchoraji wa Meksiko ya Kale unaonyesha zodiaki ya makundinyota ya unajimu wa Waazteki

Siku hizi wanajimu hawaangalii tena nyota wakitumia mapokeo ya elimu yao kujadili hatma ya binadamu. Hapo hawafuati mbinu zinazokubaliwa katika sayansi. Kinyume chake wanaastronomia wanaangalia nyota kwa njia ya kuzitazama, kupima mwanga wao na kujadili tabia za nyota, si ya binadamu, kwa kutumia matokeo ya sayansi nyingine kama vile fizikia, kemia au biolojia.

Asili ya unajimu

 
Alama kwa makundinyota 12 ya Zodiaki katika mapokeo ya Ulaya; zinadaiwa kuwa muhimu na kutawala tabia za watu kwenye horoskopi.
 
Zodiaki ya Kiarabu

Tangu mwanzo wa historia wanadamu katika sehemu mbalimbali za dunia walitazama nyota.

Nyota zinaonekana wakati wa usiku kwa kufuatana na mwendo wa dunia yetu kuzunguka jua. Kwa namna hiyo kuonekana kwa nyota kunalingana na majira ya mwaka. Kwa hiyo katika dunia kabla ya kupatikana kwa kalenda watazamaji wa nyota waliweza kutabiri mabadiliko ya hali ya hewa, kuja kwa majira ya mvua, baridi, joto na kadhalika. Kati ya nyota zilizotazamwa hivyo ni, kwa mfano, Kilimia na Zuhura.

Kwa mfano kuonekana kwa nyota fulani (hii inategemea mahali duniani) inaweza kuwa alama ya kwamba mvua ni karibu, au majira ya baridi yanaanza. Sababu yake ni ya kwamba nyota huonekana kwa vipindi fulani wa mwaka tu; kwa nyakati nyingine ziko angani kwenye mchana ambako nuru ya jua inaficha nyota zote hazionekani tena. masaa ya usiku kuna vipindi ambako nyota fulani zinaonekana vizuri angani juu kabisa na kwa njia hiyo zinaweza kutambuliwa kama ishara za majira.

Leo hii watalaamu wengi huamini ya kwamba hapo ndipo msingi muhimu wa imani ya kwamba nyota zinaathiri maisha duniani. Watu wa kale walikuwa hodari sana kutazama nyota na kutambua mabadiliko yake katika mwendo wa wakati. Hali hii haieleweki kwa urahisi na watu wa leo, waliozoea nuru ya taa za umeme, wakitumia wakati wa usiku kutazama TV au kompyuta. Lakini kwa watu wa kale - jinsi ilivyo hadi leo kwa watu wengi vijijini au porini - nyota na Mwezi vilikuwa taa, hasa wakati wa usiku.

Uhusiano ulioonekana kati ya mabadiliko ya nyota na mabadiliko ya majira yalianzisha elimu ya kalenda pamoja na unajimu na astronomia.

Kwa wazee hao ilionekana kama nyota fulani inatawala majira, hali ya hewa na hivyo maisha ya binadamu kwa sababu maisha ya jamii yalitegemea majira na mwendo wa mvua, ukame, baridi au joto. Hapo ni asili ya kuziangalia nyota kama miungu au pepo wenye uwezo fulani. Hasa tabia ya hali ya hewa ya kuchelewa au kuwahi kidogo ilijenga imani ya kwamba kuchelewa kwa mvua ni dalili ya hasira ya mungu yule anayeonekana katika nyota fulani.

Horoskopi

Kati ya mbinu za unajimu zinazojulikana sana duniani ni horoskopi.

Tangu zamani watu walitazama nyota zilizoonekana pamoja kama kundinyota kama nukta angani na kuwaza kuwa na mistari kati yake, hivyo kuona picha ya watu, wanyama au miungu. Ni hasa makundinyota 12 ya aina hii yaliyorudia kila mwaka kukaa juu kwenye anga wakati wa mwezi fulani. Makundinyota hayo yalichukuliwa kama "watawala" wa kipindi ambako zilionekana juu angani wakati wa usiku na kwa pamoja zinafanya "zodiaki" yaani ufuatano wa makundinyota yaliyoaminiwa kuwa muhimu.

Unajimu unafundisha kwamba kila kundinyota huwa na tabia fulani na mtu mtu aliyezaliwa "chini" ya nyota hizi anapokea tabia za pekee kulingana na nyota zake. Hayo makundinyota ya zodiaki yaliunganishwa na athari iliyoaminiwa kutokea kwa sayari ambazo zilipewa pia tabia zake.[1] Hayo yote ni mfumo usioeleweka kirahisi na kuwa msingi wa horoskopi.

Hadi leo chini ya vichwa kama "Nyota zinasema" magazeti mengi huchapisha namna za utabiri wa kila wiki kwa watu kufuatana na tarehe zao za kuzaliwa.

Ukristo unatazama mafundisho hayo kama ushirikina na matumizi ya horoskopi kama dhambi dhidi ya amri ya kwanza ya Mungu.

Marejeo

  1. Ijue nyota yako na tabia zako hapa, mfano wa tovuti ya mnajimu, iliangaliwa Januari 2019

Viungo vya nje

  Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  NODES
Done 1
see 1