Vipimo asilia vya Kiswahili
Vipimo asilia vya Kiswahili ni vipimo vya kihistoria vilivyotumiwa na Waswahili kwenye mwambao wa Afrika ya Mashariki katika karne kabla ya ukoloni na vinavyotumika hadi leo kutegemeana na mazingira.
Kwa jumla nafasi yake mara nyingi imechukuliwa na vipimo sanifu vya kimataifa kama mita na gramu, wakati mwingine pia na vipimo vya Kiingereza kama futi au inchi.
Asili ya vipimo vya kihistoria
haririKote duniani watu walianza kutumia vipimo wakati jamii zilianza kuwasiliana na vikundi nje ya ukoo, kuwa na biashara ya kubadilishana bidhaa. Kubadilishana bidhaa kwa bidhaa au bidhaa kwa pesa fulani kulihitaji namna ya kulinganisha na ndiyo asili ya vipimo vilivyokubaliwa kati ya watu. Katika mazingira ya kijadi vipimo hivyo viliweza kuwa tofauti kati ya mahali na mahali.
Mbinu hizo zinapatikana kote duniani: kama ni Asia, Ulaya au Afrika. Ushuhuda wake unapatikana katika matini za kale, kama vile vigae vya mwandiko wa kikabari ya Babeli au vipimo katika Biblia. Katika nchi na milki ambako serikali ilitawala maeneo makubwa kulikuwa na jitihada za kusanifisha vipimo kwa urahisi wa biashara na mapato ya kodi.
Watu walitumia vitu vilivyopatikana kirahisi katika mazingira yao, kama vile sehemu za mwili kwa vipimo yva urefu au mbegu wa mimea kwa vipimo vya uzito.
Vipimo kutokana na tabia ya mwili
haririVipimo kutokana na tabia za mwili vinapatikana kila mahali ambako watu wanakutana. Hata kama tofauti ziko kati ya watu warefu na wafupi kwa kawaida watu wanaelewa hali iliyo kawaida katika mazingira yao. Kwa hiyo umbali wa njia ulipimwa mara nyingi kwa kuhesabu hatua; kama njia ilikuwa ndefu kwa kuhesabu idadi ya siku za safari. Hapo iko msingi wa vipimo kama futi (urefu wa wayo) na maili (umbali wa hatua 1,000; "maili" inatokana na namba ya Kilatini "mille"= elfu).
Kwa kutaja ukubwa au urefu wa kitu watu walitumia urefu wa kidole, mkono na mguu, pia umbali kati ya mikono au vidole.
Vipimo vya uzani kutokana na tabia za mimea
haririMazao mara nyingi yalipelekwa sokoni kwa kuyahesabu moja-moja au kwa kutumia mjao wa chombo kilichokuwa kawaida, jinsi ilivyo siku hizi kwa kutumia "debe" kama kipimo cha sokoni. Kwa bidhaa zenye thamani kubwa watu walitafuta vipimo kamili zaidi na hapo mahali pengi duniani walitumia mbegu fulani au hasa punje za nafaka (ngano, shayiri, mchele) kama msingi.
Kwa mfano huko Uingereza sheria ilitangazwa mnamo mwaka 1303 kuwa "Imekubaliwa kwa milki yote kipimo cha kifalme kuwa penni moja ya Kiingereza .. itakuwa na uzani wa punje 32 za ngano kavu; penni ishirini zitakuwa aunsi moja, na aunsi kumi na mbili ni pauni."
Ila tu matumizi ya uzani wa idadi ya punje za nafaka kama msingi wa vipimo vya uzito ni ya kale sana. Kipimo cha uzani wa Mesopotamia ya Kale ilikuwa shekel iliyopimwa kama 180 punje za nafaka, na shekel 60 kuwa pauni moja. Mfumo huu unapatikana pia katika vitabu vya Biblia ya Kiebrania (Agano la Kale). Huko Uhindi msingi wa vipimo hivi ulikuwa punje ya mchele.
Mara nyingi vipimo vilienea kutoka maeneo ambako uchumi na biashara zilistawi kwa maeneo jirani yaliyopokea vipimo vya majirani mara nyingi pamoja na majina yao. Hapo ni sababu ya kwamba vipimo asilia vya Kiswahili vinatumia mara nyingi majina yenye asili ya Kiarabu na Kihindi, ilhali vipimo sanifu vya kisasa vina asili katika lugha za Ulaya kama Kilatini na Kigiriki.
Vipimo vya urefu
haririKwa vipimo vidogo vya urefu upana wa kidole wanda na umbali kati ya vidole vilitumiwa, ama morta baina ya kidole gumba na kidole cha shahada au shibiri baina ya kidole gumba na kidole cha mwisho. Sehemu kubwa zaidi zilitajwa kwa ziraa (sawa na mkono) yaani umbali kati ya ncha ya kidole cha kati na kisugudi. Hapo Waswahili walitofautisha baina ziraa konde (kutoka kisugudi hadi mwisho wa konde = ngumi) na ziraa kamili (kutoka kisugudi hadi ncha ya kidole cha kati)[1].
Kwa urefu zaidi au umbali kuna wari inayolingana na ziraa 2 na pima ambalo ni umbali kutoka kidole cha mkono mmoja hadi kidole cha mkono mwingine mikono inaponyoshwa kukingama mwili.
Waswahili wa kale walitumia pia hatua kwa kupima umbali lakini hizi hazikusanifishwa zaidi.
Vipimo hivi vilisanifishwa kati yao jinsi inavyoonyeshwa katika jedwali ya chini. Vipimo vya sentimita ni vya takriban maana vipimo asilia viliweza kuwa tofauti kati ya mahali na mahali.
Kipimo asilia | Jina mbadala | Sawa na | inalingana takriban na |
---|---|---|---|
Wanda | (upana wa kidole) | mnamo milimita 18, karibu cm 2 | |
Morta | morita, futuri | takriban sentimita 20 | |
Shibiri | shubiri | wanda 9 | takriban sentimita 22 - 23 |
Dhiraa | ziraa, mkono | shubiri 2 | sentimita 44-46 |
Wari | ward, wara[2] | ziraa 2 | sentimita 90 - 91 |
Pima | wari 2 | mnamo sentimita 180 (mita 1.8) |
Vipimo vya umbali
haririHakuna vipimo vya umbali zaidi ya kutaja muda wa mwendo. Steere anataja mifano aliyokuta Zanzibar mnamo 1875: "Umbali hukadiriwa kulingana na mwendo wa wastani katika saa moja. kwa hiyo Dunga iliyopo katikati ya kisiwa cha Unguja kwa umbali wa takriban maili 12 inaelezwa kuwa na mwendo wa masaa manne; Kokotoni kwenye ncha ya kaskazini cha kisiwa, kwa umbali wa labda maili 20, kuwa na mwdno wa masaa sita. Barani wanahesabu kwa mwendo wa siku moja, kipimo cha labda maili 20.[3]
Vipimo vya masi au uzito
haririKipimo asilia | Jina mbadala | Sawa na | inalingana takriban na |
---|---|---|---|
Wakia | aunsi | sarafu 1 ya reale | gramu 28 |
Ratili | ratli, pauni | wakia 16 | gramu 450, karibu nusu kilogramu |
Mani | Man | ratili 3 | karibu kilogramu moja na nusu |
Frasila | ratili 35 | takriban kilogramu 16 |
Vipimo vya mjao
haririVipimo vya mjao vilihitajika katika biashara hasa kwa nafaka. Kipimo cha kimsingi kilikuwa pishi, Pishi 1 iligawiwa kwa visaga 2 au vibaba 4.
Pishi 60 ziliitwa jizla 1, iliyoitwa pia mzo.[4] Kulikuwa pia na kipimo cha fara kati ya pishi na jizla lakini fara ilikuwa na maana tofauti kati ya mahali na mahali na tena kati ya bidhaa; katika kusini ilimaanisha pishi 12, kwenye pwani la Kenya matumizi ilikuwa tofauti.[5]
Pishi ililingana takriban na lita 2.5 - 3 lakini jinsi ilivyo katika mazingira ya kimila vipimo vilitofautiana kati ya mji na mji au soko na soko.[6]
Kipimo asilia | Jina mbadala | Sawa na | inalingana takriban na |
---|---|---|---|
Kibaba | kiasi juu ya ½ lita | ||
Kisaga | vibaba 2 | lita 1¼ - 1½ | |
Pishi | visaga 2 au vibaba 4 | lita 2½ - 3 | |
Fara | pishi 6- 12[7] | ||
Jizla | mzo | pishi 60 | lita 150-180 |
Tanbihi
hariri- ↑ linganisha Sacleux, makala "ziraa". KKK/SED makala "dhiraa" haitofautishi vile bali inataja tu "~konde" bila maelezo zaidi.
- ↑ Sacleux 1939, uk. 1017
- ↑ Steere, Handbook uk. 455
- ↑ Sehemu hii kuhusu vipimo asilia vya mjao inafuata maelezo katika kamusi ya Velten, Suaheli Wörterbuch Teil I, Suaheli - Deutsch, Berlin 1910, uk 358 ("pima")
- ↑ Sacleux uk. 215
- ↑ Kamusi ya Kiswahili Sanifu inataja kibaba kuwa "kipimo cha ujazo cha takriban gramu 700", kwa hiyo pishi 1 = vibaba 4 = gramu 2800. Haisemi ni gramu za nini; mahindi huwa na gramu 800 kwa lita moja, unga huwa na gramu ~500 kwa lita. Sacleux katika kamusi yake (dictionnaire Swahili Francais, 1939) anataja pishi kuwa sawa na nusu galoni ya Kiingereza yaani takriban lita 2.25. Velten katika kamusi yake (Suaheli Wörterbuch I. Teil, 1910; "pima") anataja pishi kuwa na takriban lita 4 akirejea kibaba kuwa kama lita 1; hapa ni juu mno kwa sababu kibaba kipo chini ya lita 1. Inawezekana ya kwamba tofauti kati ya kamusi zilizotajwa zinatokana na mahali tofauti ambako waandishi walikusanya habari zao.
- ↑ Krapf 1882, uk. 62 anataja pishi 10 kwa fara 1, "especially when measuring lime"; Sacleux uk. 215 anataja pishi 9 kwa fara huko Pemba kwa ajili ya mchele, anataja pia pishi 10 kwa fara kwa chokaa huko Mombasa, lakini pishi 6 kwenye fara kwa kupima chokaa Malindi